Kwa
wengi tumezoea kuona rangi ya kijivu ikiwa imepakwa kwenye maeneo kama kuta za
viwandani, mahospitalini, shuleni na zile sehemu nyingi ambazo kuzipendezesha
sio muhimu. Wengi hawafikirii kuwa rangi hii inaweza kupambwa nyumbani na
ikavutia sana. Kijivu mara nyingi inaendana na mazingira na kuna njia nyingi unazoweza
ukaitumia kupendezesha nyumba bila kuzidisha au kuigeuza kama eneo lililofifia.
Vilevile kijivu
inafaa kupakwa ndani na nje ya nyumba.
Rangi
ya kijivu ina jamii kadhaa ndani yake. Ikielekea kwenye uzito kwa mfano kijivu
cha moshi wa taka zinazochomwa, inaweza kuchosha na pia inaweza kukaa
kimuonekano wa maeneo ya biashara zaidi kuliko nyumbani. Fikiria chumba chenye
kuta za rangi ya kijivu hiki, kinakuwa kama stoo au gereji ambapo mvuto sio
kigezo mahali hapo.
Habari
njema ni kwamba kuna jamii za rangi ya kijivu ambazo zinakuja kwa kasi na zina
muonekano wa kuvutia mno. Kijivu chepesi ukutani kwa mfano, ni rangi ambayo
haiwezi kupitwa na wakati. Ukitumia kijivu hii unaweza ukawa na kijivu kizito
kwenye vitu vingine kama vile zulia au sofa ili kuleta mchanyato fulani mzuri kati
ya hizi kijivu mbili.
Kijivu
chepesi pia kinaendana na rangi nzito kama vile rangi za kahawia, njano ya dhahabu
na damu ya mzee ambayo pia inaitwa burgundy. Rangi hizi zinashirikiana kwa
uzuri sana na kijivu chepesi ambapo unaweza kuzitumia kwenye pazia na vitupio vya
mapambo kama vile, mito, michoro ya ukutani na fremu za picha.
Baraka
na laana ya kijivu ni kwamba inapendeza zaidi ikikaa kama background na pia
ikionekana kwa wingi. Kwa hivyo kama kuna fenicha au kitu unataka kiwe kivutio
cha chumba basi paka ukuta wako kijivu chepesi au kuwa na zulia la kijivu nzito.
Yaani vile vitu vikubwa vikubwa vipe rangi ya kijivu, kwa mfano sofa za kijivu
na kadhalika. Kijivu ni chepesi kutazama machoni na huwa hakina tabia ya ‘kufunika’
rangi nyingine. Kwa hivyo endapo una vitu unavyotaka viwe kivutio cha chumba
basi paka kuta kijivu ili vionekane kirahisi.
Kwahivyo
kama unataka kutumia kijivu lakini hutaki nyumba yako ionekane kama godown au
chumba cha daktari basi tumia kile chepesi ukutani ukichanganya na vitupio
vyenye rangi nzito kama nilivyoainisha hapo juu. Huku ukiambatanisha kijivu
kizito kwenye vitu kama zulia.
Kwenye
rangi za jamii ya kijivu unaweza kupata yoyote kuanzia nyepesi inayokaribia na nyeupe
kabisa hadi nzito inayoelekea kwenye weusi.
Ukijipanga
utagundua kuwa kijivu ni rangi yenye mvuto kwa kupendezesha nyumba yoyote ile.
Kumbuka tu kuwa usizidishe na tumia pamoja na rangi nyingine pia.
Vivi
anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755
200023
No comments:
Post a Comment