Tuesday, March 15, 2016

Namna ya kuweka mpangilio kwenye kabati la nguo


Kabati la nguo kwenze chumba cha kulala ni fenicha muhimu. Ingawa linajulikana kama kabati la nguo, linahifadhia vitu vingi mbali na nguo. Vitu hivyo ni pamoja na nguo zenyewe, viatu, masanduku, mabegi, vitupio vya urembo na vitu vingine vingi ndani za chumba chako hicho hivyo kukuwezesha kuwa na mpangilio wa vitu chumbani.

Kuna miundo miwili mikuu ya milango ya makabati ya nguo ambayo kutokana nayo unaweza kuongeza au kupunguza maeneo ya kuhifadhia. Makabati ya nguo yenye milango ya kufungua kwa kutelezesha ni mazuri pale ambapo chumba ni kidogo na hakuna eneo kubwa kuruhusu milango ya kufunguka kwa nje.  Wewe mwenye chumba cha hivi utafurahia zaidi kabati lenye milango ya muundo huu kwani utabakiwa na eneo kubwa chumbani. Kwa muundo wa pili wa makabati yenye milango ya kufunguka kwa nje yanakupa wigo mpana zaidi wa eneo la kuhifadhia ndani ya kabati hilo. Cha msingi kwa aina hii ya kabati ni chumba kuwa na nafasi ya kutosha kuruhusu milango kufunguka kwa nje na bado wewe au mwingine akaweza kupita na kupishana vizuri  kwa uhuru chumbani.

Kimsingi pangilia ndani ya kabati lako la nguo kama ifuatavyo:

·        Kwakuwa ndani ya kabati kuna vyumba/maeneo mbalimbali kama vile mashelfu ya juu na chini, madroo, fimbo ya kutundikia nguo na kulabu za kuning’iniza vitu. Kwenye shelfu za chini utahifadhia viatu endapo hujatundika mfuko wa viatu mlangoni mwa kabati hala pale milango ya kabati inapokuwa ni ile ya kufungua kwa kutelezesha. Tumia mashelfu ya juu kuhifadhia masanduku, mabegi na vile vitu ambavyo havitumiki mara kwa mara.

·        Jitahidi kutumia henga zinazofanana kwenye nguo zote ulizotundika. Lengo kuu ni matumizi sahihi ya nafasi na kufanya mpangilio uvutie.
·        Kama hazipo, weka kulabu (hooks) kwenye milango ya kabati kwa ajili ya kutundika mikanda, kofia, tai, skafu na mikoba. Hii ni kwa yale makabati yenye milango ya kufunguka kwa nje.
·        Panga nguo ndani ya kabati kwa makundi: Kundi la blauzi, jaketi, sweta, makoti,shati, suruali, suti, sketi, gauni, kaptula, fulana na kadhalika.
·        Tumia droo ndogo kuhifadhia soksi na nguo za ndani.

Kwa mpangilio huu hakika utalifurahia kabati lako la nguo kwani licha ya kuvutia ni kwamba litakurahisishia kupata kwa haraka na wepesi kile unachohitaji ndani ya kabati.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755200023

No comments:

Post a Comment