Kuna
vingi vya kuchagua pale ambapo unaamua
kupamba nyumba yako kwa jinsi unayotaka wewe. Aina na mitindo mbalimbali ya fenicha, pazia
na mazulia zipo sokoni za kumfaa kila mmoja na vivyo hivyo kwa vitambaa vya
sofa.
Baada
ya kusema hayo, kutokana na kuwa na machaguo mengi inaweza kukuwia vigumu
kuchagua kitambaa sahihi cha sofa kwa ajili ya
nyumba yako kutokana na wigo mpana
wa rangi na michoro ambayo ni pamoja na maua. Kuamua kama uchague kitambaa
kisicho na michoro au chenye michoro ni jambo linalotatiza wengi. Dondoo zifuatazo zitakusaidia kufanya uamuzi
sahihi:
·
Kitu
cha kwanza ni kufikiria mazingira ya chumba ambacho unaenda kuweka sofa zako
ili kuona kama zenye michoro au za rangi moja ndio zitafaa zaidi. Sofa zenye
michoro zinapendeza kwenye chumba ambacho kina rangi moja. Rangi moja tunayosema ni pamoja na ukutani na
pazia. Si kwamba zinafanana ila ni kuwa rangi za vitu hivyo hazina michoro. Kwa
kawaida chumba cha rangi moja huwa kinapooza, kwahivyo kwa kuweka sofa yenye
michoro, bila shaka utakuwa umekichangamsha na vilevile kulifanya sofa kuwa
kitovu cha chumba.
·
Wakati
huohuo michoro mingi inaweza kutoa matokeo ya chumba kuonekana hakijatulia.
Kwahivyo kama una pazia zenye michoro, zulia lenye michoro na pengine karatasi
za ukutani zenye michoro nazo, kwenye chumba cha namna hii ni muhimu kuwa na
sofa za rangi moja na hii itasababisha macho kuelekea kwenye vitu vyenye
michoro badala ya kwenye sofa. Michoro kila mahali inaweza kuharibu muonekano
wa chumba na kumpa aliyepo hisia za uchovu. Huenda ulishawahi kuingia kwenye
nyumba fulani na kutokana na rangi na michoro iliyopo ukajisikia
vibaya/kuchefukwa na uchovu hata ukamuomba mgeni wako mkae nje kutokana na hali
hiyo ya ndani. Kama ilishawahi kukutokea basi utakuwa unaelewa ninachosema.
·
Inawezekana
ukawa na vitu vingine vyenye michoro na hapohapo ukapenda kuwa na sofa zenye
michoro. Inawezekana kabisa kuchanganya michoro, kwa mfano unaweza kuwa na
pazia za michoro ya nyeusi na nyeupe na ukalandanisha michoro hii kwa kuwa na
sofa za michoro ya kijivu na nyeupe.
·
Dondoo
ya mwisho ni kwamba michoro mara zote inatakiwa iendane na ukubwa wa kitu
michoro hiyo iliyopo. Sofa kubwa zinapendeza na michoro mikubwa, wakati sofa ndogo
zikipendeza na michoro midogo.
Ninaamini
kwamba dondoo hizi zitakusaidia unapochagua kuwa na kitambaa cha sofa cha rangi
moja au chenye michoro.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi Obed ili kukuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755
200023
No comments:
Post a Comment