Zaidi ya uzuri uliotukuka, sakafu ya marumaru ina faida kuu
ya kuwa ni rahisi kusafisha na kutunza pia. Ni sakafu imara na pia chaguo la wengi
wenye nyumba za kisasa. Wapo wanaochagua kuwa na sakafu hii kwenye nyumba nzima
na wapo ambao wanaiweka sehemu chache kama vile katika vyumba vya jiko, bafu na
maeneo mengine ya nyumba ambayo yanaweza kuloa maji kirahisi wakati wowote.
Kwenye vyumba vingine watu hao wanatumia sakafu za aina nyingine kama vile
zulia na mbao.
Marumaru
zenyewe zimetengenezwa kwa jinsi ambayo hazinyonyi uchafu ila
changamoto kubwa
iko kwenye yale maeneo yanayounganisha marumaru moja na nyingine hatimaye
kufanya muonekano wa sakafu. Sakafu ya marumaru ikisafishwa vizuri inaweza
kuonekana kama mpya hata baada ya miaka mingi. Pamoja na kwamba sakafu hii ni
rahisi kusafisha, tuangalie mbinu za kufuata huku tukikumbuka pia hatupaswi
kuzidisha kiwango cha kusafisha.
Fagia
kila siku. Hii inasaidia kuondoa uchafu wa juujuu kama vile mabaki ya vyakula
au kutokana na viatu vilivyoingizwa ndani vikiwa na chembechembe za uchafu
kwenye soli zake.
Unapaswa
pia kufagia kabla ya kudeki. Pitisha dekio au mopu sakafuni baada ya kuwa
imeshafagiliwa.
Deki
sakafu kwa maji safi yenye sabuni kidogo na tambara au kama unatumia mopu iwe safi pia. Kama sakafu haina madoa ambayo
yanahitaji usafi wa kusugua, kutumia mopu na tambara inatosha kuifanya iwe
safi. Safisha tambara au mopu mara kwa mara unapokuwa unasafisha sakafu toka
chumba au eneo moja hadi lingine. Kwa mng’ao wa kutosha angalau safisha sakafu
yako ya marumari kwa maji kila siku.
Kausha
sakafu. Baada ya kuwa umetumia maji na mopu iliyoloa, sasa ni wakati wa kutumia
mopu kavu pekee kwa lengo la kukausha sakafu ili hata uchafu wowote ukiwa
umeingia usigandie kwenye maji. Uchafu ukiruhusiwa kubaki kwenye maeneo
yaliyoloa unaweza kung’ang’ania na kugeuka mara moja kuwa mgumu kusafisha
wakati unaofuata.
Vilevile
kukausha sakafu ya marumaru baada ya kuideki ni muhimu sana kwa usalama wa wanafamilia
wasiteleze kwani haina kawaida ya kuonyesha kirahisi kuwa sehemu fulani ina
maji.
Hata
baada ya kumaliza zoezi hili endapo kuna chochote kimemwagika sakafuni ni vyema
kukisafisha hapohapo. Kwa ajili kadri uchafu unavyobaki pale ndivyo unavyozama
kwenye maungio ya marumaru na kutengeneza doa eneo hilo. Baadhi ya vimiminika
kama vile chai ya rangi, kahawa au soda nyeusi pale zinapomwagika sakafuni na
kukaa muda bila kusafishwa zinachangia sana kuharibu uzuri wa marumaru.
Vivyohivyo
ikiwa umedondosha nyama mbichi, iokote mara moja, weka sabuni na maji na
pasafishe.
No comments:
Post a Comment