Bafu
ni chumba kidogo ambacho kinaweza kusababisha shida kubwa kama hutachagua rangi
kwa umakini. Rangi hiyo inaweza kuwa ni ya marumaru za ukuta na sakafu, ya
dari, rangi ya pazia au hata ya sinki la kuogea au ya bafu la kupachika. Ni
rahisi kuchagua rangi isiyo sahihi kutokana na mawazo ya kizamani ya kwamba
bafuni ni mahali pasipokuwa na sababu ya kupendezeshwa.
Endapo
rangi isiyo sahihi itatumiwa bafuni inaweza kusababisha kusiwe na
mvuto na wewe
ukaenda mle kwa kujilazimisha tu.
Ili
uweze kuchagua rangi sahihi kwa ajili ya bafu lako kwanza inakubidi ufahamu
changamoto za chumba chenyewe hata kabla ya kuwa na hiyo rangi unayofikiria.
Kama bafu lina dirisha dogo sana au pia hapo dirisha lilipo linapakana na
kivuli chochote kiwe ni cha mti au nyumba nyingine, uhafifu wa mwanga wa jua
utagusa rangi yoyote unayotaka iwepo bafuni.
Upungufu
wa mwanga wa asili inamaanisha kuwa utatakiwa kuchagua rangi ambayo itasaidia
kuongeza mwanga bafuni. Wengi tukisikia rangi za kuongeza mwanga tunaenda moja
kwa moja kwenye nyeupe. Sio lazima kuwa na bafu jeupe ili kuongeza mwanga
endapo ni hafifu, rangi yoyote ambayo sio ya giza au nzito inafaa kuongeza
mwanga pale taa zinapokuwa zimewashwa.
Ni kawaida kukutana na
marumaru nyingi za bafuni zikiwa na rangi ya bluu, mantiki tu ni kwamba rangi
ya bluu ni eneo la maji, na kwenye picha na mionekano mingi maji yanawakilishwa
na rangi ya bluu. Sio lazima uamue kuchagua bluu kulingana na imani hii.
Bafu linaweza kuhisiwa
baridi au lisilochangamka kutokana na kuzidiwa na rangi zilizopoa, kuanzia
rangi za bomba ambazo nyingi ni silva ya kungaa, vioo vya kujitizama na hata
vya bafu la kupachika na mng’ao wa marumaru zote hizi zinatakiwa kuwa na
uwiano.
Bafu linatakiwa
kujenga hisia za joto na burudani kwahivyo rangi kama za krimu, kijani laini,
kijivu chepesi ni kati ya ambazo zinaweza kukupa hisia hizo.
Kuwa makini usije ukazidisha
rangi. Kama bafu zima litaonekana kung’aa sana unaweza kutamani kutoka mbio
pale macho yanapokutana nalo.
Unaweza kutumia rangi
nzito kama vile rangi ya chungwa, damu ya mzee au udongo kwa vitu vingine vya
bafuni kama mataulo, ndoo ya uchafu, kitenga cha kuhifadhia tishu au pia vesi
ya maua.
No comments:
Post a Comment