Zamani kabla ya gharama ya mbao kuwa
kubwa zaidi na pia kabla ya ujio wa marumaru watu wachache waliokuwa na uwezo
wa kujenga nyumba bora waliweka sakafu ya mbao. Lakini pia kwa siku za karibuni
nimeshuhudia wasomaji wangu baadhi wakitaka kufahamu kuhusu sakafu ya mbao. Ni
kama vile imeanza kupata mvuto tena hasa kwenye sebule za nyumba za kisasa.
Nimeongea na
Patrick Joseph ambaye
ni fundi wa sakafu za mbao na anatujuza namna ya kutunza sakafu hii ambapo ni
swali namba moja linalowasumbua wengi wanaotamani kuwa na nyumba yenye sakafu
ya aina hii. Fundi anaanza kwa kusema kuwa sakafu ya mbao ni ngumu, imara na ya
kiwango ambayo inaweza kudumu miongo mingi kama itatunzwa ipasavyo. Hata hivyo
ukosefu wa matunzo na usafi unaweza
kusababisha sakafu hii kuharibika mapema hasa kwa kutengeneza madoa, mikwaruzo
na kupoteza mvuto. Zifuatazo ni dondoo
za kuzingatia ili kutunza sakafu ya mbao iwe unayo tayari au ndio unafikiria
kuwa nayo.
Mazingira: Mbao ni malighafi ya asili ambayo inaonyesha tofauti pale
inapokutana na joto kali sana na unyevunyevu mwingi kwa pamoja. Hali hizo mbili
zinapopita kiwango inaweza kusababisha mbao kupasukapasuka na kuoza.
Vilevile mwanga wa moja kwa moja wa
jua kutokea dirishani au kwenye mlango wa kioo unaweza kusababisha sakafu ya
mbao kupauka na kuchuja rangi. Epuka hali hii kwa kuhakikisha kuwa wakati jua
linalopiga moja kwa moja kwenye sakafu ya mbao pazia ziwe zimefungwa.
Uchafu: Mara kwa mara ni muhimu kufagia sakafu ya mbao kwa
kutumia ufagio laini, ili kuondoa chembechembe zote za uchafu ambazo zinaweza
kuikwaruza. Matumizi ya matandiko ya milangoni kwenye mlango wa nje na ya
kuingia kila chumba yatasaidia kupunguza kiasi cha chembechembe za uchafu
ambazo zinaweza kutua kwenye sakafu ya mbao. Vizulia vya kutupia navyo vinaweza
kutumika kwenye yale maeneo yanayopitiwa sana kama vile kwenye korido. Epuka
kutumia maji mengi au mara kwa mara kusafisha sakafu ya mbao. Safisha kwa
kutumia bidhaa zilizoidhiniswa kwa ajili ya mbao.
Vitamu tamu kama bazoka navyo ni vya
kuepuka kutafunwa ndani endapo una sakafu ya mbao.
Wanyama wa ndani: Baadhi ya watu wanapenda kufuga wanyama kama vile
mbwa, paka, sungura na kadhalika ndani ya nyumba zao. Paka au mbwa wa ndani
anapokuwa na kucha zenye ncha kali ni rahisi kusababisha mikwaruzo kwenye
sakafu ya mbao. Kama kweli ni furaha yako kufuga wanyama hawa ndani, basi uwe
unawakata kucha zao ili kuepuka hali hiyo.
Viatu: Viatu vya mchuchumio vyenye visigino visivyofunikwa na
plastiki vina uwezekano wa kukwaruza na kuharibu sakafu za mbao. Vivyohivyo kwa
viatu vilivyobeba mchanga. Unaweza kuhitajika kuweka kanuni ya kuvua viatu
mlangoni kabla ya kuingia ndani.
Fenicha: Fenicha nzito zenye miguu iliyochongoka zinaweza
kusababisha uharibifu mkubwa pale zinapoburuzwa kwenye sakafu ya mbao. Fenicha
zinatakiwa kubebwa wakati wa kuzihamisha na pia miguu yake kuwekewa kizuizi
laini chini ili isigusane moja kwa moja na sakafu.
No comments:
Post a Comment