Kuna
namna nyingi za kuongeza mvuto ndani ya nyumba zetu na tunapotaka kufanya hivyo
kwa kuweka maua ya ndani, mara nyingi
tunaenda moja kwa moja kwenye vesi za maua za meza ya kahawa au ya chakula. Ila
vyungu vikubwa vya maua vya kuweka sakafuni ni njia ya ajabu ya kuchangamsha
kona iliyozubaa au kusahaulika na kuigeuza mara moja kuwa kivutio namba moja
cha jicho ndani ya chumba. Kutokana na
kuwa na vyungu vya aina, mitindo na
ukubwa tofauti tofauti kuna uwezekano wa kupamba tofauti katika sehemu tofauti
za ndani.
Vyungu
vikubwa vya sakafuni vya maua vinawezekana kuwekwa kwenye chumba chochote na
vikaendana na mandhari nyingine iliyopo ndani vilevile.
Unaweza
kukifanya chungu kukaa kama kazi ya sanaa tu, kwa maana ya kwamba sio lazima
uweke maua ndani ili kupendezesha, badala yake chenyewe unakigeuza ndio pambo
na kinapendeza kabisa. Kwahivyo yote kwa yote inategemea lengo lako la kuweka
hicho chungu kwenye chumba husika.
Vyungu
vikubwa vya maua vya sakafuni vinapendezesha maeneo mbalimbali ya sebule,
chumba cha kulia chakula, eneo la ngazi na hata eneo la kuingilia. Vipo vyungu
ambavyo ni vya kutunza kwa uangalifu kama vile kioo na vipo vigumu, vipo vya
rangi, maumbo na ukubwa mbalimbali kadri ya uwezo wako wa unachotaka. Hakuna
kikomo na hii inavifanya kufiti kwenye nyumba yoyote, kama sehemu unayotaka
kukiweka kuna uwazi mkubwa basi unaweka kile kikubwa kabisa. Haijalishi sehemu
ikoje lazima kuna chungu ambacho kitapafaa.
Unaweza
kutumia vyungu viwili vikubwa vya sakafuni kama njia ya kuonyesha mgawanyo wa
chumba ikiwa ni pamoja na kuviweka jirani na taa za vivuli za kusimamisha
sakafuni.
Unaweza
ukachangamsha rangi ya chumba kwa kuongeza chungu cha maua cha sakafuni chenye
rangi ya tofauti. Hivi ndio vile vitu ambavyo vinatengeneza mvuto. Kwa wale
ambao hawapendi rangi kali wanaweza kuweka vyungu vyenye rangi zilizopoa
zinazooana na za kuta. Ukiweka maua marefu kwenye chungu yanakifanya nacho
kionekane ni kirefu.
Kuweka
vyungu vya maua vya sakafuni eneo ambalo ni karibu na mchoro wa ukutani
unaoendana nacho inaleta muonekano wa kuvutia. Ni uwezo wako tu wa kufikiri ili
kutengeneza uwiano. Vyungu vinafaa kwa aina yoyote ya upambaji ambapo wale
wanaopamba kwa mtindo wa kisasa wanatumia vyungu vyenye kuta laini na rangi
kali kama vile chungwa, kijani na nyekundu wakati wale wanaopamba kiutamaduni
wanaweza kuchagua vile ambavyo vina kuta na muonekano wa rafu huku rangi zake
zikiwa ni zile zilizopoa.
Vyungu
vikubwa vya maua vinakupa pia uwezo wa kuwa na muonekano wa rangi za asili
ndani ya nyumba yako. Rangi hizo ni pamoja na rangi ya mimea ambapo mingi ni ya
kijani na pia rangi ya udongo. Kama tujuavyo si kawaida kupaka kuta zote za
ndani ya nyumba rangi ya kijani au ya udongo. Badala yake unaweza kutumia
vyungu vya rangi hizo ili kuleta muonekano wa rangi za asili ndani ya nyumba pale
unapohitajika kufanya hivyo. Pia weka miti ya bamboo ndani ya vyungu vyako
katika nia ileile ya kuongeza uasili.
Vyungu
vikubwa vya maua vinapowekwa sakafuni katika hali ya ubunifu, vinasaida kujaza
sehemu zilizo na uwazi mkubwa. Uzuri wa vyungu hivi ni kwamba una uwezo wa
kuvihamisha toka sehemu moja hadi nyingine ili kubadili muonekano wa chumba
kirahisi kabisa.
No comments:
Post a Comment