Saturday, August 27, 2016

Njia za kupendezesha coffee table


Meza ya kahawa ni kitovu cha sebule wakati watu wanapokuwa wameketi kwenye sofa zinazoizunguka. Huenda unataka kuboresha muonekano kwa kupitia meza hii. Sio siri kuwa wengi tumezoea kupendezesha meza ya kahawa kwa njia moja tu ya maua tena ni yale ambayo si hai. Makala hii itakujuza njia nyingi unazoweza kutumia ili
kupendezesha meza ya kahawa ya pembe nne.

Kwanza kabisa unapaswa ufahamu kuwa katika kupamba meza ya kahawa lazima uweke uwiano wa vitu unayotaka kupambia. Hakuna kitu kinachoonekana kwa haraka kuwa ni mrundikano kama kuweka vitu vingi vidogodogo pamoja. Vilevile ukisema uipambe meza kwa kutumia mapambo makubwa tu inaweza kuonekana imeelemewa na isivutie. Kuwa na uwiano kwenye mapambo yako ya meza ya kahawa kutatofautisha namna unavyosambaza mapambo yenyewe na weka yale yanayoendana pamoja.

Zingatia mapambo marefu na mafupi. Vitu vinapokuwa vyote vina urefu sawa hakuna ambacho kinaonekana kuzidi kingine. Ili kuleta mvuto changanya mapambo yenye urefu unaotofautiana.

Unaweza kupendezesha meza ya kahawa kwa kuigawa maeneo tofauti. Hii itakusaidia kufahamu ni wapi pa kuanzia kwahivyo kukurahisishia. Igawe kwa kutumia utepe na kama ni kubwa kiasi na tepe zina upana mdogo, tumia mbili na hapo utakuwa umetengeneza sehemu nne ambazo utaamua kila moja unaipamba vipi.

Pendezesha kwa vitu vya msimu, mfano wakati wa masika maua mengi yanachanua bustanini, kata machache  na kuyaweka juu ya meza ya kahawa. Au ni msimu wa matunda kama machungwa, macheza au maepo, chukua kadhaa yaweke kwenye bakuli juu ya meza ya kahawa kwa siku chache halafu yatoe yaliwe. Kwenye maeneo ya baridi matunda haya yanaweza kukaa hadi wiki bila kuharibika.

Unaweza ukaamua pia kwenda na kijani kwa kupendezesha katikati ya meza ya kahawa kwa mmea mdogo ambao hauhitaji matunzo makubwa.

Pendezesha meza ya kahawa kwa kutumja sinia. Yapo masinia mazuri mno na mengine ni ya mbao yaliyochongwa kwa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba hata zaidi ya kupendezesha linatumika kuwekea mapambo vidogodogo ili kuyawezesha kuondolewa kirahisi wakati meza inapotumika kuburudisha. Zaidi ya hapo, sinia hilo linaweza kutumia kubeba vitu kama rimoti za luninga na redio, funguo na kuvifanya vitu hivi kuwa hatika hali ya mpangilio badala ya kuonekana kama vinaelea mezani.

Unapopendezesha meza ya kahawa weka vitu ambavyo vina rangi za kuwaka zaidi ya meza yenyewe.  Meza ya rangi nyeupe au ileile ya malighafi iliyoitengenezea kwa mfano mbao, ipambe kwa vitu vya rangi kali. Meza yenye muonekano wa mbao au rangi nyeusi inapendeza ikiwekwa mapambo ya rangi za silva, kraisto na glasi kwani zinaruhusu meza ing’ae.

Pendezesha meza ya kahawa kwa vitu binafsi vilivyobeba historia yako. Kwa mfano kazi yoyote ya sanaa uliyonunua wakati ulipotembelea sehemu fulani ya dunia au kitabu ulichosoma kikabadilisha maisha yako na pia wapo ambao wana vitabu vyao walivyoandika wenyewe.  Zaidi ya kuwa na shelfu la vitabu inawezekana kuwa na vitabu hivi maalum kwa ajili ya juu ya meza ya kahawa tu. Vitu hivi zaidi ya kukumbusha jambo fulani pia vinasaidia kuanzisha mazungumzo na mgeni wako au kumpa shughuli ya kufanya (kubeba kitabu na kuanza kukisoma) unapokuwa unamwandalia chochote.

Kuweka mishumaa midogodogo iliyo kwenye bakuli, au mmoja mkubwa au kutandika kitambaa kinachotokana na kazi za mikono kama vile kikoi na batiki ni njia nyingine pia ya kupendezesha meza ya kahawa.

nifollow instagram @vivimachange


No comments:

Post a Comment