Kwa
wengi wa Watanzania walioko mijini kununua vitu mitandaoni kunakuja kwa kasi
siku hizi. Imewarahisishia wanunuzi wengi
wasio kuwa na muda au uvumilivu wa kuzunguka kwenye maduka kununua vitu
mbalimbali na hapa nitazungumzia mapambo ya nyumbani. Uwepo wa mitandao kama
instagram, facebook, website na hata whatsapp umechangania kurahisisha manunuzi
mitandaoni kwani uzuri ni kwamba unanunua na kuletewa ulipo.
Hata
hivyo kila kitu kina changamoto zake na
hapa nimekuandalia mambo7 muhimu ambayo
unatakiwa kuyazingatia unapoamua kununua mapambo ya nyumbani mitandaoni.
Linganisha bei
kwa wauzaji zaidi ya mmoja
Unapokuwa
unalinganisha bei ya bidhaa hiyo hiyo kwa wauzaji zaidi ya mmoja kuna uwezekano
mkubwa wa kuikuta ikiwa katika bei ya chini kwa muuzaji mwingine. Hii
itakusaidia mwishoni kupata dili zuri.
Nunua kwa
muuzaji mwenye bidhaa nyingi
Biashara
nyingi hazikosekani wachuuzi kwahivyo zingatia kununua kwa wenye mali na sio
mchuuzi. Unaponunua kwa mwenye mali kuna uwezekano mkubwa wa kupata faida
kadhaa kama vile kubadilisha bidhaa na kuchukua nyingine kama utakuwa
hujaipenda au ina kasoro na pia kupata punguzo la bei.
Ulizia vipimo
halisi
Sio
wauzaji wote wa mitandaoni wanafahamu hasa bidhaa wanayouza. Kwa kawaida
mitandaoni tunanunua kwa kuona picha, na huwa mara nyingine zinadanganya.
Hakikisha muuzaji anakupa vipimo halisi vya bidhaa unayotaka kununua. Hakuna
kitu kinaudhi kama kunununua kitu mfano shuka au picha ya ukutani halafu ukaja kukuta
kuwa haina ukubwa wa kukidhi hitaji lako.
Kuwa makini na
rangi
Kamwe
usiamini rangi ya picha unayoona mtandaoni kwani inawezekana kabisa ikawa sio
sawa na ya bidhaa halisi. Usishangae kuletewa bidhaa ya rangi tofauti kabisa na
uliyotegemea kwahivyo ni muhimu kujiandaa kwa hali hiyo endapo itatokea
ufanyeje. Unaweza kumtaka muuzaji akuthibitishie rangi kabla hujanunua.
Fahamu kama
unaweza kurudisha
Pambo
fulani linaweza kuonekana kuwa na mvutio sana mtandaoni, hata hivyo ukajikuta
kuwa hujalipenda sana kwa uhalisia wake. Kama umenunua kwa muuzaji ambaye
haruhusu kurudisha ni kwamba utakuwa umepoteza hela yako.
Fahamu malighafi
iliyotengenezea bidhaa
Kwa
mfano bidhaa nyingi za mbao ngumu ni gharama sana. Unapotaka kununua mapambo
kama meza ya kahawa au kabati la luninga hakikisha kuwa hufanyi uamuzi kabla ya
kufahamu malighafi iliyotumika kutengenezea bidhaa hiyo.
Fahamu maingizo
mapya
Huenda
hujapenda bidhaa zilizopo kwa sana, ila uzuri ni kwamba karibia kila mtandao
una jinsi ya kumjulisha mfuatiliaji pale kunapowekwa ingizo jipya. Kama
unapendelea kufahamu kinachoendelea kwenye ulimwengu wa mapambo ya nyumbani
basi jiandikishe kwenye mitandao hiyo ili uhabarike kila wanapoweka ingizo
jipya.
Kununua
mapambo ya ndani mitandaoni inaweza kukurahisishia sana maisha kwani unaletewa
hadi ulipo. Cha muhimu ni kuzingatia dondoo hizi.
No comments:
Post a Comment