Ubao
wa kichwani ni kile kipande cha fenicha ambacho kiko kichwani mwa kitanda.
Unapotaka kuwa na kitanda cha kuvutia, ubao wa kichwani ndio sehemu pekee
kwenye fremu ya kitanda panapokupa nafasi ya kufanya hivyo. Ingawa sio kila
kitanda kina ubao huu ila kilicho nao sio siri kwamba kinavutia kuliko kisicho
nao. Makala hii itakujuza aina mbalimbali za mbao za kichwani na jinsi ya
kuchagua ambao utaongeza mvuto wa chumba cha kulala.
Zaidi
ya kufanya kitanda kivutie, ubao wa kichwani unakiongezea thamani. Pia ubao huo
unaweza kutumika kuendana na mtindo na
muundo wake ulivyo. Kwa mfano, watu wanaotaka kukaa wakiwa kitandani, ubao wa
kichwani unasapoti mgongo nyuma ya mito. Na pia zipo mbao za kichwani ambazo zimetengenezwa
kwa mitindo mbalimbali kama vile kuwekewa shelfu za vitabu na vitu vya mapambo
au hata eneo juu ambalo unaweza kuwekea kikombe na miwani ya kusomea. Mbao
ndefu za kichwani zinaweza kupigiliwa kulabu za kutundikia nguo za kulalia au
taulo. Nyingine zimewekewa taa kwa ajili ya kusomea unapokuwa kitandani.
Mbao
za kichwani zinatofautiana kuendana na malighafi na umbo. Ni vyema ukafahamu za
mitindo na miundo mbalimbali ili wakati unapotaka kutengenezewa au kununua
kitanda uchague chenye ubao ulio sahihi kwako. Pia ni vyema ujue kuwa ubao
unaweza kuwa umejishika moja kwa moja kwenye kitanda au umejitenga ambapo
unakuwa umesimama toka sakafuni au umepachikwa ukutani eneo kilipo kitanda.
Mbao
za kichwani zilizotengenezwa kwa malighafi ya mbao ndio za kisasa zaidi, zina
namna nyingi ya kupendezeshwa na zinaweza kupakwa rangi tofauti tofauti. Ubao wa namna hii unaweza kuongezewa sponji
na kitambaa na hata kuwekewa vishimo vidogo vingi ambavyo tunasema ni vifungo
yote hiyo ikiwa ni kuufanya uvutie.
Vivyohivyo ubao wenye michoro unafanya kitanda kivutie zaidi pale
kinapotandikwa kwa kuoanisha matandiko yenye rangi na michoro hiyo.
Kuna
maumbo mengi ya mbao za kichwani kwahivyo haijalishi kuwa kwa vile kitanda ni
cha pembe nne basi na ubao utatakiwa uwe ni wa pembe nne. Kitanda kinaweza
kuwekewa ubao wa umbo lolote liwe ni pembe tatu, duara au pembe sita. Na hata
upana wake unaweza kuzidi ule wa kitanda. Ila inashauriwa ni vyema ukubwa wa
ubao wa kichwani uendane na ukubwa wa chumba, vinginevyo unaweza kuonekana kukizidi
nguvu pale utakapokuwa mkubwa sana huku chumba kikiwa kidogo.
Bila
shaka unaweza kupata ubao wa kichwani wa mtindo na muundo unaotaka kutoka kwa
mafundi vitanda waliobobea. Uzuri mmoja wa kutengenezesha kitanda ni kwamba una
wigo mpana wa kubuni, kuchagua na kuonyesha ubao wa kichwani unaotaka
utengenezewe kwenye kitanda chako.
Nifuate instagram @vivimachange
No comments:
Post a Comment