WAKATI siku za kupiga Kura ya Maoni zikikaribia,
imebainika kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wataipigia kura ya Ndiyo Katiba
Inayopendekezwa.
Aidha, imeelezwa mwito wa vyama vinavyounda umoja
wa Ukawa wa kususa kura ya maoni haujawavutia wananchi wengi, hivyo wengi
hawauungi mkono.
Hayo yamo katika taarifa ya matokeo ya utafiti
uliofanywa na taasisi ya Twaweza kati ya Januari 27 na Februari 17 mwaka huu na
kutolewa jana kupitia muhtasari wenye jina la “Kuelekea Kura ya Maoni ya
Watanzania kuhusu Katiba Inayopendekezwa.”
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo uliosambazwa
kwa vyombo vya habari na Mshauri wa Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande,
muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza
barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za
mkononi.
Muhtasari huu unajumuisha maoni ya wananchi wa
Tanzania Bara pekee juu ya Katiba Inayopendekezwa.
“Jumla ya wahojiwa 1,399 walipigiwa simu kati ya
Januari 27 na Februari 17, 2015. Matokeo mengine yanatokana na duru la 5 la
Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,708 kati ya Julai 16 na Julai 30, 2013)
na duru la 14 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,550 kati ya Februari 12
na Machi 4, 2014).“Takwimu hizi zimetumika kufuatilia mwenendo wa muda mrefu.
Ni muhimu kukumbuka kuwa mahojiano haya yalihusisha makundi yote ya wananchi wa
Tanzania Bara.
Hata hivyo, maoni ya wananchi yanaonesha wazi
mashaka yaliyopo katika mchakato mzima wa kuibadili Katiba, kwani mwezi mmoja
tu kabla ya siku ya kupiga kura, uandikishaji wa wapiga kura
haujakamilika.
Kutokana na hali hiyo, nusu ya wananchi (asilimia
47) wanafikiri uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya Katiba mpya, lakini idadi
ndogo (asilimia 30) inafikiri kuwa uchaguzi huo utafanyika chini ya Katiba ya
sasa.
Kuhusu Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba na
ushawishi wake kwa wananchi kususa kura ya maoni, utafiti huo umeonesha: “Kati
ya wananchi waliosikia minong’ono juu ya Ukawa kususa vikao vya Bunge la
Katiba, asilimia 66 wanapinga hatua hiyo.
Asilimia 68 wanapinga ushawishi kwa wananchi kususa
kura ya maoni na robo tatu (asilimia 75) ya wananchi wanasema hawatasusa kura
ya maoni.” Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema kuna “Kuna
mambo matatu yanayojitokeza kutokana na maoni haya ya wananchi.
Jambo la kwanza ni kwamba kura ya ‘Ndiyo’ kwa
Katiba Inayopendekezwa haina uhakika. Tofauti iliyopo ni finyu na wananchi
wameonesha kwamba kura hii inaweza kubadilika wakati wote katika mchakato
huu.
“Pili, kuna kilio kilicho wazi kuhusu umuhimu wa
Katiba kusisitiza masuala ya uwazi na uwajibikaji. Wananchi wameunga mkono kwa
nguvu zote vifungu vinavyoimarisha uwajibikaji. Changamoto kubwa zilizopo
katika upatikanaji wa huduma za kijamii na kuwepo kwa tatizo kubwa la rushwa
vyote vimekuwa na athari kubwa na wananchi wanatafuta njia za kuwawajibisha
viongozi kwa matendo yao.
“Tatu, wananchi hawajashawishika kuchukua hatua za
nguvu za kuleta mabadiliko. Mwito wa UKAWA wa kususa kura ya maoni haujawavutia
na wananchi wengi hawauungi mkono. Mambo haya matatu yatakuwa changamoto kubwa
kwa viongozi wa ngazi zote kuamini kwamba mawazo yao yanawakilisha maoni ya
wananchi.”
Elvis Mushi, Mratibu wa Sauti za Wananchi alitoa
maoni yake kuhusu matokeo hayo alisema: “Mashaka yaliyopo juu ya kukamilika kwa
mchakato wa mabadiliko ya katiba na kubadilika kwa mwenendo wa mchakato huo
kumesababisha mashaka kwa wananchi. Hali hii ndio inayosababisha maoni ya
wananchi kugawanyika katikati kuhusu masuala yote muhimu.”
Askofu afunda viongozi wa dini
Viongozi wa dini wametakiwa kufundisha amani na
upendo kwawaumini wao na si kuwahamasisha wananchi wasiipigie kura ya ndio
Katiba ijayo, kwani hali hiyo imeelezwa itasababisha nchi kutokea mitafaruku ya
wenyewe kwa wenyewe ikiwa hata viongozi wa dini nao watashiriki mambo ambayo
hayawahusu.
Hayo alisema Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentekoste
Tanzania, Erasto Ikongo na ambaye ni Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa
Kipentekoste Tanzania (PPT) alipokuwa anatoa tamko la kupinga kauli ya Jukwaa
la Wakristo Tanzania (TCF), kuhusu kushikilia msimamo wao wa kushinikiza
waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa kwa kudai kuwa katiba
hiyo imefika hapo ilipofika kwa njia ya ubabe na kukosa uadilifu.
Alisema viongozi wa dini wanatakiwa wabebe vitu vya
Mungu na kuongelea masuala ya Mungu na si kuzungumzia yale ambayo
hayawahusu.
“Viongozi wa dini waendelee kuhamasisha dini ili
nchi yetu ibaki kuwa na amani na utulivu kama ilivyo sasa na si kuingilia
masuala ya Katiba ambayo hayawahusu,” alisema na kuongeza kuwa, kama wao
walikuwa na nia na Taifa hili wangebeba hoja moja tu ya inayohusu Mahakama ya
Kadhi kwa vile ni suala la kidini na si kubeba hoja za Ukawa.
Pia, aliwataka viongozi wa dini wote waliokwenda
bungeni Dodoma warudi kwani wanahamasisha waumini ambao ni wabunge vitu ambavyo
vinaweza kupoteza amani nchini kwetu.
Awali, tamko la umoja huo lilitolewa juzi na kusainiwa na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa,
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maskofu wa KipentekosteTanzania
(CPTC), Askofu Daniel Awet na kusema wao hawana hasira kama ambavyo watu
wengine walivyotafsiri.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment