Hivi ulishawahi kukutana na zulia ambalo
unaona ni zuri mno kwamba halistahili kuwekwa nyumbani kwako? Au umependa rangi
na michoro yake lakini hujui uliweke wapi? Wengi wanadhani kwamba zulia ni
kwa ajili ya kupamba sakafuni tu. Leo hii nakufahamisha kuwa si kweli! Historia
inaonyesha kuwa kupamba ukuta kwa kutundika zulia ni utamaduni ulioanzia kwenye
makasri ya kifalme. Kazi za sanaa zinazoonekana kwenye zulia zilitambuliwa kama
ishara ya utajiri.
Zulia zuri kwa michoro na rangi linaweza kuwa silaha tosha
kwa kupendezesha kuta za ndani mwako.
Baadhi
ya washauri wa mapambo ya nyumba wameshagundua jambo hili na kuchukua hatua ya
kulitoa zulia sakafuni na kulihamishia ukutani. Unalitundika kama lilivyo
hakuna kuliwekea fremu. Chagua ukuta unaotaka kulitundika na liweke kwa jinsi
ambayo litaning’inia katikati ya ukuta huo.
Kwa
kawaida kupendezesha ukuta mkubwa na mpana inaweza kukuwia ngumu. Inawezekana
huna muda wa kutengeneza ukuta wa sanaa au hata pengine bajeti ni kubwa na njia
nyingine kama vile ya kubandika karatasi za ukutani ni kwamba yote haya
yanahitaji muda na hela ili kufanikisha. Badala ya kufuata njia
tuliyoizoea ya kutundika picha na sanaa za ukutani, tundika zulia la kuvutia na
utashangaa ni kwa jinsi gani litakamilisha ukuta mweupe. Kutokana na rangi
na michoro iliyoko kwenye mazulia, linapendeza pale linapokuwa limetundikwa
kwenye ukuta na chumba kikubwa. Zulia zuri linaleta muonekano wa kuvutia
ukutani kuliko hata ilivyo kwa sakafuni.
Linapokuwa
sakafuni, lengo la zulia ni kuleta mshikamano wa chumba, kuvuta pamoja michoro
na rangi kadhaa zinazoonekana kwenye fenicha na mapambo mengine yaliyopo
hapo lilipo. Kama ilivyo kwamba sanaa ndogo ndogo zenye kazi za kuwaka
zinasaidia kuchangamsha chumba chenye rangi na fenicha zilizopoa,
kutundika zulia ukutani kama mbadala wa hizo sanaa kunatimiza malengo
yote kwa kuua ndege wawili kwa jiwe moja huku ukiipa sakafu nayo nafasi
nyingine ya kupendezeshwa. Rangi zinaweza kuhitajika kwa ajili ya chumba fulani
kwahivyo zulia la ukutani litasaidia kutimiza lengo hilo bila kuongezea sanaa
nyingine zozote za ukutani.
Kama
ilivyo sakafuni, michoro ya zulia lililotundikwa ukutani inaweza vilevile
kutengeneza muendelezo wa kushirikisha muonekano wa vitupio vidogodogo ambapo
inaleta hisia za kuwa kitu kimoja kizima kilichokamilika. Kutundika zulia kwa
mtindo huu kunalipa jicho fahari ya kuliangalia.
Rangi
na michoro iliyopo kwenye zulia la kutundika ukutani hazina kikomo cha
kuoanisha na vitu vingine kama mito ya kwenye makochi au utepe wa mezani. Moja
ya faida kubwa ambayo zulia linatoa ni wigo mpana wa rangi au michoro ambapo
isingewezekana hivyo kwa sanaa yoyote ya ukutani.
Zulia
la kutundikwa ukutani lina uwezo wa kuunganisha rangi zote kuanzia nyeusi na
nyeupe kadri utakavyolichagua kuendana na mahitaji yako ya rangi na michoro
katika ukuta unaotaka kulitundika.
Zulia
unalotaka kutundika ukutani hata kama ni jipya hakikisha kuwa unalisafisha
kwanza. Usitundike zulia chafu.
No comments:
Post a Comment