Marumaru
za aina ya mosaic ni marumaru ndogondogo ambazo mara nyingi ni za pembe nne na
ukubwa wake huwa ni inchi 2 kushuka chini. Tuungane na
fundi James Urio ambaye
anatujuza namna ya kutumia marumaru hizi ndani ya nyumba zetu.
Anaanza
kwa kusema kuwa watu wengi wanaogopa au hawajui namna ya kutumia marumaru za
mosaic kwenye nyumba zao na badala yake zinaonekana zaidi zikiwa zimewekwa
kwenye majengo makubwa ya hadhara hasa bafuni na kwenye nguzo. Hii inasikitisha
kwakuwa hizi marumaru zinaweza kutumika kuongeza rangi na mvuto kwenye chumba
chochote ndani ya nyumba zetu. Zinapotumiwa kwa usahihi zinaweza kufanya sehemu
iwe kitovu cha chumba.
Jambo
la msingi katika kutumia marumaru za mosaic ni kuchagua za rangi sahihi kwa
eneo unalotaka kuziweka. Fikiria kwa makini ni nini lengo la chumba hicho na
utagundua kuwa kupendezesha ndani ya nyumba yako kwa marumaru za mosaic ni
rahisi sana. Cha muhimu ni kufurahia wigo mpana uliopo wa marumaru hizi na pia
uwezekano wa kuziweka kwa kuchanganya rangi zaidi ya moja. Zina uwezo mkubwa wa
kubadilisha sehemu kupata hisia unayotaka kwahivyo usizichukulie poa.
Bafuni
ni sehemu namba moja ya kuweza
kupendezesha kwa marumaru za mosaic kwasababu ni nadra sana kukosea kwenye eneo
hili la nyumba. Zinaongeza hisia za asili bafuni kama vile unaogea nje kwenye maporomoko ya maji yaliyozungukwa
na mawe. Chagua rangi za asili kisawasawa, na utakapoongezea pazia lenye
michoro ya asili pia itasaidia mno kuleta hisia za asili utakayopata wakati
ukioga kwenye bafu lako hilo. Rangi za kijani na udongo ni za hisia za asili,
kwa maana hiyo mosaic za kijani kilichokolea zinafanya sehemu zilizowekwa
ionekane zaidi ya nyingine.
Marumaru
za mosaic kwa eneo la bafuni unaweza kuzitumia ukutani, pembeni ya sinki la
kuogea na pia sakafuni. Pia kwa kuchanganya za rangi zaidi
ya moja utatengeneza muonekano wa kuvutia na unapotumia za rangi ya bluu kwenye
sakafu ya bafu hakika panapendeza.
Jikoni ni eneo lingine maarufu unaloweza
kusisitiza uzuri wake kwa kutumia marumaru za mosaic. Unaweza ukaziweka kwenye
eneo la kati ya kaunta na makabati ya juu, rangi za marumaru utakazochagua
ndizo zitafanya jiko livutie.
Sakafu ya marumaru za mosaic inaweza
kuwekwa katika chumba chochote mbali na bafuni, kwa mfano, mosaic za rangi
mbili tofauti zitavutia kwenye korido.
Inawezekana baadhi ya wenye nyumba
wasipende rangi za kuwaka na nzito, ila haimaanishi kwamba hawawezi kuweka
marumaru za mosaic. Kitakachosaidia ni uchaguzi na uchanganyaji wa rangi, kama
unataka rangi za kiume basi chagua nzito na nyeusi lakini hakikisha kuwa kuna
mwanga wa kutosha.
No comments:
Post a Comment