Friday, September 26, 2014

---nitavukaje--Kutoka ualimu wa kuajiriwa hadi kujiajiri kwa kufungua media company

Leo katika mfululizo wa stori zangu za kukuwezesha kuvuka kutoka daraja ulilopo kwenda la juu nimeongea na entrepreneur  Fred Kirya ambaye alikuwa mwalimu hapo kabla lakini sasa ana media company. Nikamuuliza amevukaje? Akaniambia alivyokuwa mwalimu alijishughulisha pia na kuandaa program za vijana walioathirika na mambo mbalimbali, watukutu na hata wanajeshi waliotoka vitani halafu vichwa vikavyatuka kiana. Kutoka huko baadhi wa vijana walioweza kuachana na hali hizo wakawa wanaenda kuongea kwenye vituo mbalimbali vya redio. Hapo ndipo Fred alipojenga interest na media na akafungua media company yake ambayo anarekodi nyimbo za kwaya, singles za wasanii, program za watoto na vipindi vya vijana kwenye vituo vya redio. Fred anasema kwa kufanya kazi kwenye kampuni yake mwenyewe ana furaha ya kufanya anachokipenda, kuwa makini zaidi kwa mfano matumizi na utunzaji wa vifaa vya kazi na kubwa zaidi financially amekuwa na wise spending...... Kaa standby kusoma stori nyingine itakayofuata...

usisahau kuwekea mbolea bustani yako kwenye vuli hii

Mvua za vuli zimepamba moto kabla ya kuingia kwenye masika. Ukiweka mbolea kipindi hiki ikakutana na masika yanayokuja itasaidia mno kuboresha bustani yako.


Thursday, September 25, 2014

my article for newspaper: jiko safi ukiendelea kupika


Baadhi ya siku unaweza kushangaa kama kupika kunalipa kwa nguvu yote inayotumika. Kweli, unaweza kuweka mlo kabambe mezani, lakini jiko lako likaishia kuwa chafu mno kwa, mrundikano wa vyombo vichafu. Unaweza ukawaza kuwa inaenda kuchukua muda mwingi kusafisha kuliko kula!

Kanuni kuu ya jiko kuwa safi wakati ukiendelea kupika, ni kuanza na jiko safi. Kwa njia hii uchafu unaokuogopesha ni ule unaotengeneza wakati wa kupika tu. Kwa mazoea wengi wanajitahidi kuacha jiko safi kabla ya kwenda kitandani kila ifikapo usiku. Vyombo visafi vinawekwa kabatini, vile vichafu vinaoshwa, viporo vinawekwa kwenye vikontena na kuwekwa ndani ya jokofu, ndoo ya uchafu inamwagwa na kwa namna hiyo hakuna uchafu unaobaki jikoni.
.
Siri ya kufanya jiko liwe safi wakati unapoendelea kupika ni kuosha kadri vinavyochafuka. Nadhani hakuna njia nzuri zaidi ya kusisitiza hili. Kama wali unaendelea kuiva kwa dakika 20, una muda wa kusafisha. Kama kuna muda wa kusubiria chakula kiive, basi kuna muda wa kusafisha. Inashangaza jinsi tunavyodharau hizi dakika 10 (au zaidi!) ambazo zingeweza kurahisisha kazi yetu ya kusafisha hapo baadaye. Safisha kwanza, na utakuwa na muda wa kupumzika na kufurahia chakula chako baadaye.

Pimia vyakula ndani ya sinki, na rudisha kila kitu mahali pake baada ya kukitumia ili kaunta isishamiri vitu. Jitihidi kuwa unafanya maandalizi yanayotakiwa kabla ya kuwasha jiko. Kama unatumia kikombe au kijiko cha kupimia, hakikisha unakisuuza papo kwa hapo mara baada ya kukitumia. Futa vyakula kwenye kaunta kila vinapowagika, hii itasaidia kuzifanya kaunta zako zisiwe vululu vululu na kukusababishia kazi kubwa ya kusafisha baadaye. Hii pia inasaidia kuwa na eneo la kutosha kufanyia kazi. Nyanya ndio kiungo kinachochafua zaidi kaunta. Haiepukiki kupata matone ya nyanya ukutani na hata juu ya stovu. Kufuta punde kwa kitambaa cha unyevu kunasafisha mara moja, kwa ajili tone halijakomaa. Kwa chakula ama kiungo chochote kile kilichomwagika jikoni mwako safisha kabla hayijakaukia kwenye eneo husika. Itasaidia kuokoa muda na machukizo baadaye.

Hifadhi vifaa na vyakula unavotumia mara kwa mara maeneo ya karibu na safisha makabati yako ya jikoni na jokofu kwa msimu. Kwa namna hii hutakuwa na haja ya kuondoa vitu vyote kabatini kwa ajili ya kutafuta kitu kimoja unachohitaji.

Wakati unapopika tumia vyombo vichache. Kwa mfano, wakati unapotaka  kumenya viazi badala ya kumenyea maganda kwenye chombo, tumia mfuko au gazeti mbapo utabeba na kutupa moja kwa moja kwenye ndoo ya taka na hivyo kupungukiwa na chombo cha kuosha.

Kwa siku zile ambazo una muda mchache sana, pika vyakula rahisi ambavyo havihitaji kutumia sufuria na vikaangio vingi. Fanya mapishi ambayo chakula zaidi ya kimoja kinapikiwa kwenye sufuria moja, mifano ni mchemsho na mbogamboga.

Endapo utakuwa na mapishi kwa ajili ya wageni kadhaa nyumbani, basi gawa kazi yako. Fikiria ni nini unaweza kuandaa usiku mmoja kabla ya ugeni wako. Hii itasaidia kufanya maandalizi na kujikuta baada ya tukio ukiwa na vyombo vichache vya kusafisha. Kama utapika maharage kwa mfano, unaweza kuyasafisha na kuloweka usiku. Halafu unayaacha yamekaa kwenye jokofu, hadi kesho yake wakati wa kuyapika.

Kupunguza mrundikano kwenye kaunta inafanya wepesi wa kusafisha jiko lako. Unavyokuwa na vitu vingi kwenye kaunta ndivyo inavyokupasa kuvisogeza vyote kabla ya kusafisha na hii inakupa kazi kubwa. Baadhi ya watu kanuni ni kuwa, hakuna kifaa chochote kukaa juu ya kaunta vinginevyo kiwe ni kile tu kinachotumika kila siku kwa mfano kipashio cha chakula. Vingine vyote kama visagio na kadhalika vinahifadhiwa kabatini hadi wakati wa matumizi ndipo vinapotolewa. Usipende vijiko na visu vyako vikae juu vikibeba mafuta mafuta na vumbi. Viweke kwenye droo lililo karibu na stovu, ili unapovihitaji iwe rahisi kufungua na kuchuka. Havina haja ya kuwa juu ya kaunta na kula eneo lako la kazi.

Hizi ni baadhi ya njia za kukuwezesha kuweka jiko safi wakati ukiendelea kupika. Je, wewe msomaji wangu ni kwa namna gani unaweka jiko lako safi wakati ukiendelea kupika? Nitafurahi kusikia toka kwako!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

--vuka--kutoka architect muajiriwa hadi kujiajiri

Vijana wetu wengi mara wanapomaliza chuo wanaanza kusaka ajira. Wengi wanashindwa kuamini kuwa wanaweza kujiajiri kwa kufanya kile ambacho tayari wameshakuwa na ujuzi nacho. Leo nimechat na Caleb ambaye ni architect, nikamuuliza ni kwa vip ameweza kujiajiri. Alichoniambia ni kuwa mara baada ya kumaliza chuo aliajiriwa kwa miaka miwili. Wakati huo alikuwa anafanya vikao na wateja wake binafsi nyakati za jioni baada ya kazi za mwajiri wake. Mambo yalivyochanganya akajiajiri. Nikamuuliza maana ya mambo kuchanganya ni nini? Akasema alipata mradi wa mwaka mmoja kwenye kazi yake hiyo ambapo alijiaminisha kuwa akijiairi wakati wa mradi huo itakuwa ni wakati muafaka kwani hata kwa miaka miwili mbele asingepata mradi, mwingine mkubwa bado angeweza ku survive kwa zile kazi ndogondogo. Anasema ana uhuru zaidi wa binafsi na kipesa alivyo sasa kuliko alivyokuwa ameajiriwa. Umepata cha kujifunza hapo? Nawe waweza vuka ulipo kwenda upande wa pili ulio bora zaidi.

Tuesday, September 23, 2014

-vuka---kutoka daraja la uzururaji hadi fundi mechanic

nimekutana na hii nikaipenda na nikaamini ni daraja ambalo vijana wengi wangeweza kuvukia. unaweza ukadhani walivyolifumua fumua gari wapo Japan kumbe ni hapa hapa TZ...
hii ni chasis mpya baada ya gari kufumuliwa na ile ya zamani kuondolewa. Inaoshwa ipakwe rangi ndio kijumba cha gari kipachikwe.
chasis la zamani lililoondolewa kwa ajili gari lilikuwa limepata ajali na hivyo chasis kupinda.

kijumba kikisubiri chasis ikamilike ili kipachikwe.

----vuka----

friends,
as nina spirit ya biashara nimependa kuweka "nitavukaje" ambacho ni kijisegement kitakachokupa hadithi fupi sana ya mafanikio itakayokutia moyo na hata kuweza kukupa wazo la biashara. karibu...

Monday, September 22, 2014

vitu hivi vitaiongezea bedroom yako mashiko...

1. ki carpet...chochote kile ili mradi miguu isipate ubaridi na ugumu

2. mito ya kumwaga...

3. sehemu ya kukaa ambayo sio kitandani

4. vitu/picha unazopenda zinazokupa kumbukumbu nzuri

5. ugiza giza...bedroom ikiwa nyeupe saana mashiko yanapungua, weka pazia ambazo zinaua mwanga kiaina

Thursday, September 18, 2014

my article for newspaper: vifaa vya msingi jiko dogo la kisasa


Huenda pengine ndio unaanza maisha ya kujitegemea au ya ndoa, unahitaji kuwa na vifaa vya msingi jikoni vya kuanzia kwa miezi michache ya mwanzo—hata miaka michache. Au labda ni mzazi unayetaka kumsaidia huyo kijana wako, binti au rafiki namna ya kuanza maisha. Pia kama ni bibi harusi mtarajiwa makala hii inakuhusu. Nimefanya kazi kubwa ya kutafiti katika maduka ya vifaa vya jikoni na kukuandalia orodha ya vifaa vya msingi kabisa vinavyotakiwa kuwepo jikoni kwa ajili ya kukuwezesha kuandaa chakula katika maisha yako hayo mapya.

Nia hapa ni kuonyesha orodha ya vifaa vya kawaida kabisa vya msingi vya jiko dogo la kisasa.
Ni rahisi kuangukia kwenye ushawishi wa muonekano lakini kitu kimoja cha kujua kwa kweli ni kuwa hauna haja ya kuvunja benki ili kuwa na vifaa vya jikoni vya kiwango.  Orodha hii ya vifaa vya msingi jikoni inaweza kubadilika kutokana na hitaji la mhusika. Pia vyombo vya mezani kama vile sahani vijiko na glasi vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi na kwa sababu hiyo sijaviorodhesha hapa. Kwa hivyo vifaa vya msingi vya jiko dogo la kisasa ni kama vifuatavyo:

Visu

Kisu kikali cha mpishi ni moja kati ya vifaa muhimu zaidi jikoni, na kama utanunua kilicho sahihi kitatumika kwa miaka mingi. Nunua visu vya jikoni ambavyo havishiki kutu.

Ubao wa kukatia

Ubao sahihi wa kukatia utafanya visu vyako vidumu, na rahisi kusafishika. Kuna aina nyingi za mbao hizi kama vile plastiki, miti na hata glasi.

Kifungulia chupa na makopo (opener)

Nunua ambayo unaweza kufungulia chupa na makopo ya aina tofauti tofauti. Nzuri ni ile iliyo rahisi kwa matumizi.

Kisaga vyakula (Blender)

Kama kawaida nunua ambayo ni rahisi kutumia na yenye kazi nyingi tofauti ambapo utaweza kusaga vyakula vyako na kutengeneza juisi.

Vikaangio na masufuria

Iwe uko singo au ni wanandoa wapya kwa kuanzia unahitaji vikaangio japo viwili na sufuria nne hadi sita. Sokoni vikaangio na sufuria zipo zilizotengenezwa kwa material nyingi mno. Nunua ambazo hazing’ang’aniani na chakula (nonstick).
Stovu
Watengenezaji wengi wameunganisha stovu na tanuri ukinunua mbayo unaweza kutumia nishati zaidi ya moja itakuwa ni busara zaidi.

Jokofu
Kwa maeneo mengi ya nchi yetu walau inahitajika kuwa na jokofu kwa ajili ya kuhifadhia chakula kisiharibike. Kwa kuanzia si mbaya ukawa nalo dogo kwenye jiko lako hili la kuanzia maisha.

Kipasha chakula (Microwave)
Hiki kinafanya kazi kubwa ya kupashia na hata kupikia baadhi vya vyakula. Habari njema ni kuwa zipo za bei rahisi kabisa. Ni rahisi kutumia na wengi wanapendelea kuziweka juu ya kaunta ya jiko. Huna haja tena ya kupashia chakula kwenye sufuria.

Kikausha mikate (Toaster)

Hiki nacho kwa wengi wanaopendelea kula mikate iliyokaushwa huwa wanakiweka juu ya kauta.
Mabakuli/Vikontena
Wanasema mapishi ni sanaa, sio? Kuwa na mabakuli na vikontena ndani ya jiko lako la kuanzia maisha vitakusaidia katika maandalizi ya mapishi na hata vikontena vitakusaidia kupashia na pia kuhifadhia vyakula kwenye jokofu.

Kindoo cha uchafu
Unapoandaa chakula na kuosha vyombo lazima utahitaji hiki kindoo kwa ajili ya kuwekea uchafu. Ni muhimu kiwe kile cha mfuniko wa kujifunga chenyewe.
Jiko lenye vifaa vya msingi vinavyopaswa kuwepo jikoni ni rafiki kwa mpishi. Unapokuwa na vifaa sahihi na unajua jinsi ya kuvitumia, unaweza kuelekeza akili yako kwenye chakula unachoandaa. Kama nilivyosema awali vifaa hivi vinaweza kuongezeka kutegemea na mhusika na mazingira unaweza kuwa na vifaa hivi vya msingi jikoni kwa kuanzia na baadaye ukaongeza kidogo kidogo kwa kadri ya mahitaji yako. Mpishi mzuri anatumia vifaa tofauti tofauti na mwishoni anapata vile hasa anavyohitaji.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Tuesday, September 16, 2014

pambo hili lina faida lukuki...

Pambo hili na jamii yake linafaa kuwekwa ukutani na mlangoni kwa ajili kwa umbo lake huwa linakuwa flati upande mmoja na kitumbo upande wa pili. Ndani kuna nafasi kiasi kwamba likiwa kama pambo; wakati huohuo unaweza kuhifadhi vitu vidogo dogo kwama vile dawa zilizo kwenye pakiti, uzi na kadhalika. Laa kama unataka kusisitiza pambo lako basi weka maua ya artificial badala ya vikorokoro kama huyu hapa kwenye picha alivyoweka. Lilivyotengenezwa material yake sio nzito. Unaweza kulitumia miaka nenda rudi. Linapatikana kwenye maduka yanayouzwa mapambo ya ndani. Perfecto!



Thursday, September 11, 2014

my article for newspaper: Jinsi ya kupata kizulia sahihi cha jikoni


Wengi tutakubaliana kuwa zulia la ukuta kwa ukuta sio sahihi kuwekwa jikoni, ila kizulia cha kutupia kina faida kadha wa kadha jikoni. Kizulia hiki kinasaidia kuepusha miguu na sakafu ya baridi na kinaongeza rangi, hata kiwe kidogo namna gani. Yote kwa yote sababu kuu yaweza kuwa ni kwa ajili ya burudani ya miguu na kuiepusha na baridi. Kama unaweza kusikia baridi ya kukera kwenye nyumba yako mwenyewe basi ni ukakasi. Kuweka kizulia jikoni kunakamilisha sakafu na mvuto wa jiko. Vinginevyo uwe unapenda sana rangi kiasi kwamba umepaka kabati zako za jikoni rangi ya kung’aa kama vile pinki, kijani ama nyekundu.

Kizulia cha kutupia kinaweza kuleta rangi bila kukufanya utumie hela nyingi, kama hii ndio sababu ya kuamua kuweka kizulia jikoni hapa basi ni dondoo chache za kukusaidia kupata kilicho sahihi.
Kuchagua kizulia sahihi kwa ajili ya jiko, ni vyema kufahamu nia yako kuu ya kuamua kukinunua. Inaweza kuwa ni kwa ajili ya kuepusha miguu na ubaridi wa sakafu au kuongeza staili, rangi na mvuto kwenye sakafu ya jiko. Pia fikiria ukubwa na umbo la kizulia ambacho kitafaa zaidi kwa nafasi iliyopo. Usisahau kuzingatia vifaa vilivyotumika kutengenezea kizulia utakacho na kufahamu ni utunzaji kiasi gani utakaohitajika. Chagua kizulia ambacho hakitelezi (hakikimbii sakafu) kwa ajili ya sababu za kiusalama.

Hasa kama sakafu ya jiko lako ni laini, yakung’aa na inayoteleza, ni muhimu sana kuchagua kizulia chenye mnato/mpira kwa chini kinaposhikana na sakafu. Mpira huo utasaidia kizulia kikae mahali pamoja kisihame hame kinapokanyagwa, ambapo kinaweza kusababisha mtu kuanguka.

Chagua mahali sahihi pa kuweka kizulia chako cha jikoni. Ni wapi unapotumia muda mwingi unapokuwa  jikoni? Pengine ni mbele ya sinki, kwa hiyo ni kuwa utachagua kuweka kizulia eneo hili. Au labda una eneo kubwa la kutembea kwenye sakafu ya jikoni. Basi angalia mahali hapo kati unapoweza kutupia kizulia chako ili kilete burudani ya miguu maeneo kadhaa. Vile vizulia vyembamba virefu vinafaa zaidi wa jiko lenye sakafu ndogo.

Kama lengo lako kuu la kuhitaji kizulia jikoni ni kuondoa ubaridi na kuleta nesa nesa ya miguu, basi unene wa kizulia unahusu. Utahitaji mbonyeo kati ya sakafu ngumu na miguu yako kwa burudani. Ulaini wa kizulia pia unaepusha miguu yako na baridi la sakafu ya marumaru au mbao au hata saruji. Hakuna anayetaka kuwa kwenye maumivu wakati akiosha vyombo!

Chagua manyonya sahihi, iwe ni sufi au pamba. Kizulia ambacho kinasafishika kirahisi kwa sabuni na maji. Urahisi wa kusafisha ni lazima ukumbukwe kwenye kuchagua kizulia cha jikoni, hasa kwa vile vinavyowekwa chini ya sinki au mbele ya stovu au jokofu. Vizulia vya sufi vinaweza kuwa chaguo sahihi kimuonekano ila kwa kawaida vinashika madoa kirahisi na vinahitaji usafishaji wa kitaalam kwahivyo ni vyema kuweka vizulia vya aina hii kwenye vyumba vingine nyumbani ila sio jikoni au chumba cha kulia chakula, anasema muuzaji Aisha Mbegu. Vizulia vya kufumwa kwa mimea ya asili kama vile katani au majani ya baharini vinaweza kuwa chaguo sahihi kwa ajili ya kuweka chini ya meza ya kulia chakula, kwa ajili kwa kawaida ni rahsisi kuvifuta na kusafisha hata kwa kufagia.

Haijalishi utaamua kuchagua kizulia cha jkoni kilichotengenezwa kwa vifaa vya aina gani, kuchukua kipimo cha eneo unalotaka kuweka kizulia ndani ya jiko lako itakusaidia kupata kilicho sahihi. Wakati wa kuamua aina za vizulia, jitahidi kutafakari rangi, na ni kwa namna gani ukubwa  na muundo utakavyogusa muonekano mzima wa jiko lako.

Wacha kizulia chako kitengeneze stori. Chagua ambacho kitaongeza uzuri kwenye jiko lako. Sakafu za jiko huwa zinapooza, kizulia kinaweza kuongeza uchangamfu na ladha binafsi kwa kuunganisha rangi za jiko pamoja. Kama nilivyosema kabla, chagua kizulia kitakachoongeza rangi, ambapo ni rahisi kubadilisha kizulia ili kuondoa muonekano wa jiko utakapochoka zile rangi zake za kudumu ulizozizoea.

Hongera kwa kufanya eneo kla sakafu ya jiko lako kuwa na mvuto, nesanesa na budurani! Utakapoweka kizulia cha jikoni hutatamani kukiacha.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Wednesday, September 10, 2014

kwanini ni muhimu kufua carpet kwa sabauni na maji ya pressure

ninapata amazing deal ya kufua mazulia ya manyoya kwa ajili wateja wengi wanayaleta kutokana na kuwa yananuka vibaya. Carpet linapokuwa na harufu mbaya kwa kuwa labda limemwagikiwa vimiminika pengine ni wakati wa sherehe au maisha ya kawaida ya kila siku na pilika za watoto, kusafisha kwa vacuum cleaner au form cleaner haitawezekana kuondoa harufu mbaya ya zulia la manyoya likiloa linavyonuka.

Kinachotakiwa kufanyika ni kuniletea carpet lako kwa kuwa tuna pressure washer ya kuweza kulipiga maji, kuweka detergent na kulisugua hadi mabaki yote ya vyakula (eg ubwabwa wa sikukuu) na vimiminika vyote vitoke. Baada ya hapo tunaanika kwenye jua kali kwa siku mbili na zulia lako linakuwa tayari kama jipya. Kuamua kufua zulia kwa maji inaweza kuchangiwa pia na uchafu mwingine wowote kama vile vumbi na tope.

Karibu sana ian car wash tung'arishe tena carpets zako. Tuwasiliane 0755200023
carpets zilizofuliwa, kukauka na kukunjwa

mteja yuko tayari kupelekewa carpets zake kwenye gari

hizi nazo ni za mteja mwingine zinamsubiri

 hizi hazijakaula hivyo tumetandaza ndani tuanike tena kesho


Monday, September 8, 2014

---vitu vizuri---getting better with age

2014, uso unaonekana tight

2014, hapa ni kama vile my face is dropping! heeee he, in my mid 30's

2002, 12 years before nilikuwa hivi; ni nini siri ya kutoruhusu makunyanzi kuja fastaaa. enjoy your monday gators....

Thursday, September 4, 2014

my article for newspaper: kuepusha wadudu ndani ya nyumba

Wakati baadhi ya watu wanaogopa wadudu, wengine wanaweza kuwa wanavutiwa nao. Lakini kitu kimoja ambacho wengi tutakubaliana ni kuwa wadudu makazi yao sio ndani ya nyumba. Si tu kuwa wanaleta mazingira hatarishi kiafaya, bali pia, ni rahisi tu ya kuwa wanaudhi, kuanzia mbu wanaokupigia mziki masikioni mwako, kukuuma na kukusababishia maradhi hadi kwa nyigu anayeweza kukusababishia kidonda.

Hata yule mende wa kawaida anaweza akasababisha mzio hasa kwa watoto, anasema dokta Emil.
Kuepusha wadudu ndani ya nyumba inaweza kuwa ni vita vilivyoshindikana. Bahati nzuri ni kuwa, kwa kufahamu ni nini kinachovutia wadudu ndani ya nyumba yako, unaweza kuanza kufanya mabadiliko ambayo yatawakimbiza kimya kimya.

Kama ilivyo kwa binadamu, wadudu nao wanahitaji chakula, maji na makazi ili kuishi. Kwa kukata usambazaji wa chakula chao na kuvuruga maeneo yao ya kujifisha, unaweza kupunguza tatizo la kuwa na wadudu ndani ya nyumba yako. Kata chanzo chao cha chakula kwa kuhakikisha kuwa vyakula vyote vinawekwa kwenye kontena zilizofungwa vizuri. Mabaki ya vyakula ndani ya nyumba yatupwe eneo moja tu ambalo ni ndoo ya uchafu  yenye mfuniko wa kujifunga wenyewe iliyopo jikoni. Ndoo hii imwagwe na kusafishwa kila siku baada ya kuosha vyombo vya chakula cha usiku. Futa michuzi na mabaki yoyote yanayoweza kuwepo maeneo ya wazi ndani ya nyumba. Osha vyombo punde mara baada ya kutumika. Pipa linalomwagwa uchafu nje nalo liwe na mfuniko.

Usisahau vyakula vya wanyama waliopo nyumbani kwako. Kwa mfano unafuga mbwa na una vyakula vyake vya unga umehifadhi stoo, unga huu unaweza kuvuta mende na sisimizi. Unaweza kuweka dawa za kuzuia wadudu kwenye stoo yako ya chakula cha wanyama unaofuga.
Vifaa vyote vya kuhifadhia mabaki ya vyakula ndani na nje ya nyumba viwe vinasafishwa kwa dawa za kuua wadudu mara kwa mara.

Kama vile mlango uliolokiwa unavyoweza kuwaweka wavamizi nje, mlango uliozibwa sahihi unaweza kuwazuia wadudu wasiingie ndani. Kuepusha wadudu wanaotambaa kuingia ndani kwa kupitia sehemu ya wazi mlangoni, weka kizuizi cha mpira au brashi chini ya mlango. Vizuizi hivi vinapatikana kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi, anasema mseremala Simon.

Kumbuka kuwa mbinu zote hizi za kuziba chini ya mlango hazitafanikiwa kama mlango wenyewe utaachwa wazi. Kama una watoto ambao wanasahau kufunga mlango, fikiria kusimika vifunga mlango.
Wenye nyumba wengi wanategemea hewa safi ya nje iingie ndani kupitia milangoni na madirishani. Hii inaweza kuwa majaribu hasa wakati wa kiangazi. Bahati mbaya ni kuwa kiangazi ni wakati mbaya kwa vile mbu na wadudu wengine wengi wanavamia ndani ya nyumba. Kufurahia raha ya hewa safi bila kupata bughudha ya wadudu weka wavu wa kuzuia wadudu kama mbu kwenye madirisha na milango.

Eneo la nje ya nyumba linaweza kuwa linasababisha wingi wa wadudu ndani ya nyumba yako. Endapo mioto ya asili ni mingi na iko karibu sana na ukuta wa nyumba basi tegemea kuwa na mazalia makubwa ya wadudu na hivyo uwezekano wa wengi kujaribu kukimbilia ndani. Hii pia itakufanya hata wewe mwenye nyumba kushindwa kufurahia kukaa kuburudika nje ya nyumba yako, kwa hivyo njia nzuri ya kuepusha wadudu ndani ya nyumba ni kuhakikisha wanaondoka pia kwenye maeneo ya nje ya nyumba.

Majani yaliyorundikwa, matofali yaliyopangwa kwenye yadi yako na hayatumiki tena na mashimo ya maji taka yanafanya makazi ya wadudu mbalimbali. Maeneo haya ni sehemu za kujificha kwa wadudu kama mende nyoka na wengine wengi na hata panya. Mashimo ya maji taka yawe na mifuniko iliyoziba vizuri na mrundikano mwingine wowote uondolewe na utashangazwa ni kwa jinsi gani wadudu watakimbia na mazingira yako yatakavyovutia.

Baadhi ya wenye nyumba wanapendelea kutumia dawa za kupulizia kwa ajili ya kuua wadudu kama mbu na mende. Haijalishi ni njia ipi unatumia ili kuepusha wadudu kufanya makao ndani ya nyumba yako; njia kuu ya kuwafanya wakimbie ni kukata “mirija” wa kile kinachowavutia. Hii inamaanisha ni pamoja na kuondoa mrundikano, vyakula na vyanzo vya maji. Bila kuwa na rasilimali hizi, wadudu watakimbia kwako kuelekea nyumba ya pili na kukuacha ukiwa na amani.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com


Monday, August 25, 2014

...marvelous monday...

marafiki zangu wa kweli wamerudi shule...


ukiniuliza best skill yangu ni ipi nitakujibu cleaning..yani iko moyoni. i love to make things and places spotless...

Thursday, August 21, 2014

my article for newspaper: makosa wakati wa kununua sofa


Makosa makubwa ya kuepuka wakati wa kununua sofa
Moja ya umuhimu wa makala kama hii ni kusaidia wadau kuchagua kilicho chema kwa ajili ya nyumba zao. Sofa ni fenicha ambayo muda mwingi wa maisha ya nyumbani unakuwa pale hivyo inatakiwa ikidhi viwango vya nyumba na maisha unayoishi. Kuhakikisha unapata sofa sahihi, epuka makosa haya makubwa unayoweza kufanya wakati wa kuinunua. Habari njema ni kuwa makosa haya yanaweza kuepukwa kama kutafanyika maandalizi kabla ya manunuzi. Makosa haya makubwa basi, ni yapi ambayo mara kwa mara wanunuzi wanayarudia?

Kusahau kupima ukubwa wa sebule yako

Unatakiwa kujua ukubwa wa chumba kabla ya kukua sofa ili kuwa na uhakika kuwa fenicha hiyo mpya itafiti. Usikimbilie kununua fenicha kabla ya kuwa na uhakika wa ukubwa wa chumba, zingatia itakavyokaa kwa kujali milango na madirisha.

Kama eneo husika kuna mwanga mwingi unaoingia zingatia rangi ya kitambaa kwani vipo vinavyopaushwa na jua. Sofa inatakiwa iendane na ukubwa wa chumba, isiwe kubwa sana wala kiduchu. Usitegemee kumbukumbu wakati ukiwa kwenye chumba cha maonyesho ya sofa, huwa inadanganya kuona kuwa sofa ni ndogo kwenye chumba hicho kwani eneo ni kubwa, pia sofa iwe na uwiano na fenicha nyingine sebuleni.

Kutokuwa makini na rangi
Je unafahamu kuwa rangi ya sofa inayoonekana kutokuwa na nguvu kwenye chumba cha maonyesho inaweza kuwa kinyume kwenye sebule yako? Nenda na mto wa sofa unaoupenda na kuutupia kwenye sofa unayotaka kununua ili kuona itakuwaje ndani mwako.

Mvinyo mwekundu unaenda kumwagika kwenye sofa zako, kama una wanyama wa ndani kama paka nao wanaenda kufanya mambo kwenye sofa yako, mwenza na watoto wanaenda kula bisi kwenye sofa zako; hata uwakataze mara ngapi. Kwa kuwa maisha halisi yanaendelea kila siku, unahitaji sofa ya kuweza kubeba madhila yote haya.

Kuchagua aina mbaya ya kitambaa cha sofa ni kosa la gharama. Chagua rangi na aina ya kitambaa kutokana na jinsi sofa inavyoenda kutumika. Kama sebule inatumika sana na ukanunua sofa ya kitambaa laini au rangi za mwanga, inaenda kuharibiwa hata kabla hujaifurahia. Rangi ya sofa iendane na fenicha, samani, rangi ya ukuta na taa.

Rangi nyeupe, maziwa au nyingine ya mwanga isiwe chaguao lako kama kwenye makazi yako kuna uwezekano wa tope na mikono michafu kufikia sofa. Siku zote chagua rangi ambayo unaipenda na unaweza kuishi nayo, usichague kwa kuangalia mitindo ya nyakati. Utaishi na hiyo rangi uliyochagua kwa miaka.

“Siwezi kukuambia ni mara ngapi nimefanya kazi na wateja ambao wanataka kubadili kitambaa cha sofa zao ambacho bado kiko vizuri bali ni kwa sababu tu wameichoka rangi yake”, anasema mtengeneza sofa Hamis Rajabu. Bahati mabaya ni kuwa haichukui muda kuchoka vitambaa vya maua maua, vyenye mistari mikali na vile vya rangi za giza, anasema Hamis. Ushauri wangu ni kuwa, chagua rangi ya kitambaa ambayo itashirikiana na rangi nyingi. Kama unapenda rangi nilizosema zinachosha mapema basi weka japo kwenye kiti kimoja cha pembeni lakini siyo kwa sofa nzima, anashauri Hamis

Kutokuomba ushauri kwa wauzaji
Ongea na watu wanaouza watakupa mawazo ambayo yatakupelekea kufanya maamuzi ya busara. Hata hivyo unamuizi wa mwisho ni wako ila unapenda kuwauliza wataalam usikie wanasemaje.

Kutofikiria sofa ina burudiko kiasi gani 
Utakubaliana na mimi kuwa mara nyingi unaweza kushindwa kupata usingizi kitandani, ila ukija kwenye sofa ukaegesha aidha ukiangalia muvi au kusoma kitabu haraka sana unapata usingizi. Ni muhimu kuwa sofa unayotaka kununua ikawa ya matumizi na burudani.

Kununua sofa kabla ya kuijaribu
Kama ambavyo sofa haitakiwi kuwa ndogo sana au kubwa sana kwenye chumba, vilevile isiwe ndogo sana au kubwa sana kwako. Kama ni mrefu, hakikisha ukikaa miguu yako itakaa vizuri. Kamwe usinunue sofa kabla ya kuijaribu, ikalie, ilalie, ijaribu kwa kila namna ambayo utaitumia nyumbani. Kama unapenda kupata usingizi wa mchana kwenye sofa hakikisha mikono yako iko vizuri kwenye sofa unayotaka kununua.

Haya ni makosa makubwa ya kuepukwa wakati wa kunua sofa. Endapo utafanya makosa haya utaishia kutoridhika  na sofa uliyonunua.
Tukutane wiki ijayo!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Tuesday, August 19, 2014

Thursday, August 14, 2014

my article for newspaper: maeneo tunayosahau kusafisha

 
Wakati ukiwa unasafisha makazi yako mwishoni mwa wiki hii, kumbuka kufanya usafi wa uhakika. Mara nyingi huwa tunasafisha maeneo na vitu vinavyoonekana. Makala hii itakujuza baadhi ya sehemu na vitu ambavyo kwa wengi ni rahisi kusahaulika kusafishwa na mwishoni utasema, ee kweli hapa huwa sisafishi.

Tunakumbuka kusafisha ndani ya jokofu, lakini je juu na chini yake? Ndani ni kwasababu huenda kila tunapofungua mlango wa jokofu harufu mbaya na macho yanatuashiria kuwa sasa ni wakati wa kusafisha. Juu ya jokofu kunabeba vumbi ambalo sio rahisi kuliona vinginevyo uwe ni mrefu sana. Nyuma na chini ya jokofu vile vile kunaweza kuwa kumebeba vumbi sawa na lile la juu. Na chini sio vumbi tu hata mabaki ya vyakula vinavyodondoka kwenye sakafu ya jikoni. Kinachotakiwa ni kusimama juu ya kiti na kusafisha juu  wakati kwa chini unachotakiwa ni kuomba mtu wa kukusaidia kulisogeza ili usiharibu sakafu yako kwa kuburuza. Jokofu likishakuwa limesogezwa, ni kiasi cha kufagia na kudeki.  Baada ya hapo lirudishe mahali pake.

Tunategemea feni majumbani mwetu kwa ajili ya kuleta mpepea wa ubaridi. Kwa kadri feni inavyotumika, ndivyo inavyojaa vumbi. Feni hasa za darini ni maarufu kwa kujaza tabaka la vumbi. Njia rahisi ya kuzisafisha ni kufuta kwa kutumia ufagio uwe wa kawaida au wa buibui uliofungiwa kitaulo kilicholoa kwenye brashi zake. Kulingana na majira na matumizi, feni zisafishwe walau mara moja hadi mbili kwa mwezi .

Ni kichekesho cha muda mrefu kuwa ndani ya nyumba sofa ndio eneo linalomeza vitu vidogodogo. Kwa sababu hii mito ya sofa (ile ya kukalia na kuegemea) inapaswa kuondolewa na ndani ya sofa kusafishwe. Japo kwa nyumba nyingi ndani ya sofa ni rahisi kusahaulika kusafishwa hadi pale vitu kama hereni, kalamu ama opener inapopotea ndio eneo hili linakumbukwa kua huenda mtoto kaficha humo. Kulingana na aina na ukubwa wa familia yako pengine huhitajiki kusafisha ndani ya sofa mara kwa mara. Usafi huu ujumuishe na kufua foronya za mito, ni kazi rahisi japo huwa inasahaulika.

Ndoo za taka za ndani ya nyumba zinaashiria kuwa zinahitajika kusafishwa ila pipa la nje linakosa kiashiria hiki kutokana na eneo lililopo. Ukiona jirani anaanza kuguna kila unapofungua pipa lako la nje la taka basi ni wakati wa kufikiria kulisafisha kiaina. Kwa kawaida mapipa ya taka ya nje yanahitaji kutupiwa jicho la usafi zaidi wakati wa kiangazi kuliko wa masika.

Kama una taa za vivuli ndani ya nyumba yako, kumbuka kusafisha kile kifaa kinachosababisha kivuli. Kuendana na jinsi kilivyotengenezwa iwe ni kwa kitambaa, kioo au plastiki zinaweza kusahaulika kufunguliwa na kusafishwa.

Majani ya mimea iliyooteshwa ndani ya nyumba husahaulika kufutwa vumbi. Haishangazi kukuta mmea wa ndani iwe ni nyumbani au mgahawani ukiwa na majani yaliyojaa vumbi.
Vipasha vyakula (microwave) vinachafuka sana ndani kwa kuwa wengi wanapasha vyakula ambavuo havijafunikwa. Uchafu huu wa matone ya michuzi unaorukia kwenye kuta za microwave hubaki na kukaukiana na ajili unapata moto kila vyakula vingine vinapopashwa. Haishangazi kukuta microwave ambayo kwa jinsi ilivyo ndani unapata ukakasi kupashia chakula.

Ingawa wengi hawana taabu ya kukumbuka kusafisha vioo iwe ni vya madirisha au vya kujitazama, kioo cha luninga ni eneo ambalo kwa wengi linasahaulika kusafishwa. Endapo luning hii inatumiwa na watoto wadogo ni rahisi kuona alama za vidole kwenye kioo pale inapokuwa imezimwa. Chukua muda kufuta vumbi luninga yako weekend hii ili kufanya kioo king’ae tena.

Vumbi linajikita kwenye vitabu. Chukua dasta kufuta vumbi vitabu vyako.

Ingawa tunaweza tusione uchafu na utando ulio kwenye vitasa vya milango ya nyumba zetu lakini upo. Na tunapovisafisha tunaweza tusihisi tofauti, lakini unajisikia vizuri kushika kitasa kisafi. Na zaidi ya yote kukinga nyumba yako na vijidudu vinavyotoka kwenye mikono michafu inayofungua milango kwa kushika vitasa hivi.
Ni nini na wapi unapofikiri watu wengi wanasahau kusafisha? Je kuna popote nimesahau?


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Wednesday, August 13, 2014

bafu la wenza...

kwenye sanitary ware zetu hili sijaliona bado...au mdau wewe umelifuma wapi hili bongo?


Friday, August 8, 2014

wakati wa SNAPSHOTS...




house tour: Here's the $20M SoCal Mansion Kim and Kanye Just Bought

hebu tusafishe macho mdau tuone mambo hapa...
 wenye nyumba, kim & kanye
 ukifungua geti unakutana na muonekano huu wa mbele
 yasemekana ina vyumba 8 vya kulala
 vegetable garden nayo haijakosekana
 floor ni ya mbao...huenda baby north atalala hapa
kanye naye atakuwa anajilia raha za kisamaki hapa kwenye hii pool

Thursday, August 7, 2014

my article for newspaper: kusafisha vifaa vya kusafishia


Jinsi ya kusafisha vifaa vya kufanyia usafi

Hatusafishi vifaa vyetu vya kusafishia sio? Hata ukikataa, kubali tuu kuwa wengi hawasafishi. Wengi tunajua umuhimu wa kusafisha na kutunza vitu….ila vifaa vyetu vya kusafishia mara nyingi vinasahaulika. Haijalishi wewe ni msafi kiasi gani, haiwezekani kuweka nyumba safi kama vifaa vyako vya kusafishia havisafishwi! Makazi ya vijidudu vingi ni kwenye maeneo machafu. Angamiza vijidudu kwa kusafisha sponji na vifaa vyako vingine vya kusafishia!

Kwa sababu tu kinatumika kusafishia sio kuwa kinajisafisha chenyewe. Kiukweli vifaa vya kusafishia vinaweza kuwa makao ya uchafu, vijidudu, tope na harufu kama havitunzwi vizuri. Jinsi vifaa vinavyotunzwa ndivyo hela yako ya kununua vipya itakavyobaki mfukoni. Ufagio mchafu unachafua zaidi sakafu na pia uchafu huo unaweza kukwaruza sakafu yako. Mashine ya kusafishia kwa upepo ambayo haijasafishwa haifanyi kazi yake vizuri. Weka vifaa vyako katika hali ya usafi ili kuwa na matokeo mazuri.
Kuna ule usafi wa kawaida wa kusafisha vifaa vya kusafishia japo kwa sabuni na maji na kuviacha vikiwa safi tayari kwa kuanza usafi mwingine. Brashi za kusafishia bafuni zishafishwe kwa dawa za kuua vijidudu japo mara moja kwa mwezi. Brashi za kusugulia zaweza kusafishwa kwa maji na sabuni ya kawaida. Brashi zenye taka zilizojishikilia waweza kuchukua kijiti na kuondoa taratibu taka zote ziwe ni tope au nyuzi nyuzi.
Ndoo zako za kupigia deki usiziache zikiwa na uchafu wa aina yoyote hata kama ni maji yaliyotumika tayari. Ziache zikiwa kavu aidha kwa kuzigeuza juu chini.

Sponji la kuoshea vyombo uwe unaliosha kwa maji ya moto walau kila juma. Ikiwezekana hata kulichemsha jikoni itakubwa bora zaidi, wengine wanaenda hatua ya mbali zaidi ya kuliweka kwenye kipasha vyakula (microwave).  Ila kama utafanya hivi hakikisha sponji limeloa chepechepe kabla ya kuliweka kwenye microwave. “Asimilia 70 ya bacteria huishi kwenye sponji chafu”, anasema dokta Mbuya.

Tokea ukiwa mdogo, kulikuwa na kitambaa cha kufutia vumbi nyumbani. Ukichukua kitabu chenye vumbi unachukua kitambaa unakifuta. Vitambaa hivi vya kufutia vyumbi ambavyo wengi wetu wanaviita dasta vinapaswa kufuliwa kiumakini kama tunavyofungua nguo nyingine. Tofautisha kati ya vile vyenye uchafu mkubwa wa kudiriki kutengeneza utando na vile vyenye uchafu mwepesi.

Vichwa vya mop na madekio mengine vinapaswa kusuuzwa baada ya kufanyika usafi na kuachwa vikauke. Kabla ya kusuuza hakikisha kuwa unaondoa udongo wote, mchanga na hata majani yanayoweza kuwa yamejishikilia ndani. Sio sawa baadhi walivyozoea kuacha dekio linakanyagiwa mlangoni. Pale ni sehemu ya kuweka tandiko la mlangoni na sio dekio. Sabuni ya kawaida ya kufulia inatosha, huhitaji kuweka dawa za kusafishia kwenye vifaa hivi. Ila ni muhimu vikuke kwani vinaweza kutoa harufu ya uvundo.

Kusafisha mifagio..mmh ni wachache wanaofikiria kufanya hivyo! Unaweza kufungua ile sehemu ya brashi ukaitenganisha na fimbo na ukaiweka kwenye ndoo ukasafisha na brashi zako nyingine za kusafishia. Jambo la kuzingatia ni kuondoa matope kwanza kwa kuwa sehemu ya ufagio ya brashi ni maarufu kwa tope na uchafu uliojizunguishia kwenye vibrashi vyake.

Mashine za kusafishia kwa upepo zinatofautiana kiumuundo ila kuna dondoo kadhaa za kukuwezesha kuisafisha. Tafuta kama una kitabu ulichonunulia kitakuongoza jinsi ya kuisafisha. Hakikisha unamwaga mfuko wa kukusanya vumbi mara kwa mara. Kutegemea na jinsi unavyotumia mashine yako fua mfuko wa vumbi kila baada ya miezi mitatu. Uanike ili ukauke kabisa kwani ukiiurudisha ukiwa na unyevu utasababisha vumbi kufanya tope na hivyo kuiharibu mota kwa kuilazimisha ifanye kazi kubwa ya kusukuma kushindana na ukuta wa tope. Kama unasikia harufu ya vumbi inatoka ndani ya mashine yako ni kwa kuwa mfuko wa vumbi umejaa.

Ingawa hutumii mashine yako ya kufulia kwa kitu kingine zaidi ya nguo bado kuna wakati inakubidi ufungulie maji kuisafisha yenyewe bila kuweka nguo ndani.

Tumejuzana namna ya kusafisha vifaa vya usafi ambavyo tunatumia mara kwa mara nyumbani. Inaweza kuwa shughuli sahihi ya kufanya kwa muda wowote wa ziada ulio nao weekend hii!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

alhamisi ya rasha rasha...

rasha rasha za leo za hapa na pale za kupunguza vumbi kwa tuliopo mazingira ya vumbi. hali ya hewa si joto wala baridi ni safi kabisa...


Thursday, July 31, 2014

my article for newspaper: kusafisha bafuni


Hakuna anayetaka kusafisha bafuni, lakini ukisafisha kila unapotumia, kazi inakuwa na maumivu kidogo kuliko kuacha hadi wakati wa usafi mkubwa. Makala hii itakujuza ni jinsi ya kuweka kuta, bafu, sinki, bomba, eneo la kuogea na bakuli la choo nadhifu kila wakati.
Unapoanza kusafisha bafuni, kwanza ondoa vitu vyote vya kuhamishika kama vile vizulia, tenga la nguo chafu, kimeza au kikabati na kindoo cha taka.
Hakikisha kuwa dirisha liko wazi ili hewa ipite kuondoa hewa nzito.

Baada ya hapo ondoa buibui kwenye kona za dari ikifuatiwa na kufuta vumbi mlango kwa nje na ndani. Kwa ujumla wakati wa kusafisha chumba anzia juu kushuka chini. Ruhusu taka za vumbi na buibui zimwagike sakafuni kwa ajili utasafisha mwishoni. Kitambaa cha kufutia kinafaa sana kwa kazi hii japo pia waweza kutumia fagio.

Mimina blichi ama sabuni za kusafishia kwenye bakuli la choo na iache iondoe uchafu taratibu.

Weka dawa ya unga wa kusafishia zile sehemu ambazo zina uchafu. Kama kuna uchafu umejijenga kwenye lile eneo la kuogea, sinki ama pembeni na bomba weka unga wa kusafishia halafu sugua taratibu kwa brashi. Ukiacha unga huu ukae kati ya dakika 10 hadi 15 wakati ukifanya jambo jingine itaruhusu kulainisha uchafu. Hakikisha unasoma maelezo ya dawa ya kusafishia ili kuwa na uhakika unatumia kiasi sahihi ambacho hakitaharibu maeneo yako. Pia ni vyema kujaribu dawa eneo dogo kabla ya kusafishia eneo kubwa.

Paka sabuni au dawa nyingine za kusafishia kwenye kuta za bafu kama ni za marumaru. Kwa kutumia sponji ama brashi sugua sehemu uliyoweka sabuni. Isuuze vizuri kuondoa michirizi yoyote michafu na kama ukuta ni wa karibia na sinki ama bakuli la choo ukaushe kwa taulo. Ukuta wa sehemu ya kuogea unaweza kuuacha bila kuukausha. Ni vyema kuvaa glovu wakati wa kusugua kwani baadhi ya madawa na sabuni zinaweza kuchubua ngozi.

Safisha bomba la kuogea ambalo sio siri kuwa wasafishajiwengi huwa hawakumbuki kusafisha. Bomba inatumika tu kusafishia kwingine ila yenyewe inasahaulika kusafishwa. Ni kama msemo wa mshumaa kujiunguza kumulikia wengine! Kwa sababu hiyo utakuta kwenye bomba na vichwa vyake kunakuwa na uchafu wa sabuni zilizogandian. Hali huu huweza ikasababisha makazi ya vijidudu.

Pazia la bafuni huwa linaandamwa na ukungu eneo linalogusana na sakafu. Ni vizuri zaidi ukalifungua na kulifua kwenye maji ya moto kwa kiasi kidogo cha sabuni na blichi. Kumbuka adui nambari moja wa ukungu ni blichi. Kiasi kidogo kitaondoa uchafu bila hata kusugua.

Angalia eneo la sinki na sugua mabaki ya sabuni na dawa za mswaki kwa sabuni kidogo pamoja na sponji au brashi. Mswaki wa zamani unaweza kutumika kuondoa uchafu kutoka eneo la kati  ya bomba na mishikio yake. Kuwa makini kuwa brashi la kusugulia bakuli la choo lisitumike kusugulia  sinki. Hii inaweza kusambaza maradhi kwa kuruhusu vijidudu vya kwenye choo kuingia kwenye sinki la mswaki. Kuzuia hali hii isitokee, brashi la bakuli la choo liwe la peke yake. Ni muhimu kutumia blichi kusafishia bafuni ili kusaidia kuua vijidudu.

Safisha kioo kwa kutumia ama maji na taulo au dawa ya kusafishia vioo na taulo.

Safisha nje ya choo ukianza na ile sehemu ya juu ya kuvuta maji, taratibu endelea kusafisha eneo lote la nje ya choo ambalo ni pamoja na mfuniko na eneo la chini ya pale pa kukalia na futa kwa taulo. Kumbuka kitaulo hiki kimetengwa kwa kusafishia choo pekee.
Sugua ndani ya bakuli la choo kwa brashi yake halafu vuta maji. Huna haja ya kusugua kwa nguvu nyingi. Acha sabuni na dawa ya kusafishia ikufanyia kazi hiyo.

Sasa ni wakati wa kusafisha sakafu ukinanzia na zile sehemu zilizojifisha hadi zile za wazi. Safisha mavumbi yote na uchafu wote ulio chini na pale eneo la choo lilipounganika na sakafu. Eneo hili kwa kawaida huwa ni chafu sana na lile bomba la nyuma linajaa mavumbi. Malizia kwa kusuuza kwa maji masafi kuondoa sabuni itakayoweza kubaki na kusababisha utelezi.

Subiri kidogo sakafu ikauke ndipo urudishe vile vitu ulivyoondoa awali.
Ili kuweka bafu lako katika hali ya usafi na kupunguza kutumia nguvu kubwa ya kusafisha unatakiwa uwe unasafisha maeneo mbalimbali ya bafu mara baada ya kuyatumia. Kwa mfano safisha bakuli la choo kila baada ya kulitumia, vile vile eneo la kuogea pamoja na sinki. Hata kama sehemu hizi hazionekani kuchafuka safisha tu kwani madini yaliyoko kwenye maji nayo yaweza kufanya alama. Kama utafanya hivi, usafi mkubwa utakuwa na maumivu kidogo kwani uchafu hautakuwa umejijenga.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com