Kupamba nyumba inaweza kuwa kazi ngumu na ya muda mrefu
kwa baadhi, ingawa pia wapo wanaoona ni kazi ya kuvutia na wanaifurahia.
Haijalishi wewe uko kwenye kundi gani lakini ni kwamba inaweza kukuchukua miezi
kupata pambo dogo tu kama vile picha unazotaka kutundika ukutani ambazo
unaamini utazipenda kuziangalia kila siku. Ukweli ni kwamba vitu vya nyumbani
vimetawanyika kwenye masoko mbalimbali na vingine ni vidogodogo kiasi kwamba vinachukua
muda mrefu kuvikusanya pamoja. Na vilevile inategemea na kipaumbele cha mwenye
nyumba kwamba ni nini anataka kwa uwezo na umuhimu wa kuwa nacho kwanza kabla
ya kingine.
Kwahivyo kazi ya kupamba inaweza kuwa ni ya kudumu au laa ikachukua
muda mrefu tu.
Mambo matatu muhimu sana katika
mapambo ya nyumbani ni
kupata vile vitu ambavyo unavipenda haswa, viwe katika ubora unaokubalika na viuzwe
bei ya kawaida unayoweza kuimudu. Kuna maeneo mengi wanauza au kutengeneza vitu
vya kuwa navyo ndani ya nyumba.
Unapoanza kupamba nyumba yako
hizi ni dondoo chache za kukuwezesha kufanya maandalizi:
Usijaribu kupamba vyumba vyote kwa wakati mmoja. Fikiria
kwanza picha halisi ya chumba kimoja jinsi unavyotaka kionekane. Huenda ni
chumba chako, au cha mtoto wa kiume, au wa kike, sebule, jiko, bafu, ofisi ya
nyumbani au hata chumba cha wageni. Kuna mawazo lukuki kama vile rangi, taa,
maua, karatasi za ukutani, mazulia na aina ya upambaji iwe ni wa kisasa au wa
saresare. Kwahivyo kuwa mbunifu, hapa ndipo mahali unapoweza kuleta uwakilishi
wako kwenye nyumba yako. Onyesha vitu unavyopenda.
Ukishakuwa na wazo tayari, chagua chumba kimoja na uanze
nacho na andaa orodha ya vitu unavyotakiwa kununua kwa ajili ya chumba hicho.
Je unataka kukipaka rangi upya? Kuongeza rangi ukutani kunaleta uhai wa chumba.
Anza na eneo kubwa la chumba halafu malizia na vitu vidogo vidogo kama vile saa
ya ukutani au taa za mezani.
Angalia bajeti yako. Je ni kiasi gani cha pesa uko tayari
kukitumia. Chukua muda kidogo kuwekea bei kila kifaa ambacho umeorodhesha ili
upate picha ni kiasi gani cha pesa unahitaji. Ukishajua hili itakupa moyo wa
kuanza zoezi la kupamba.
Kuwa na orodha yako kila wakati ukijua ni nini unachotaka
kununua na kipo kwenye hali gani. Tumeona vitu vya nyumbani vilivyokwishatumika
tayari iwe ni hapa nchini au nje ya nchi, japo vipo kwenye hali nzuri vikiuzwa.
Fungua macho yako wakati unaponunua.
Chukua muda kuangalia huku na kule kuona
ni nini kipo, kipo wapi na kwenye hali gani. Baada ya muda utakuwa umeshajua
kabisa ni nini unanunua wapi na kwa bei nzuri. Unaweza kununua vitu vyako kwa
kasi yako mwenyewe. Wakati mwingine hutakiwi kuwa na haraka kwa ajili kwenye
harakati zako unaweza kukutana na kitu ambacho kweli umekipenda sana na kinaweza
kukupa wazo jipya la kupamba.
Kusema kweli kupamba hakuna muda maalum ni kama vile ni
tendo endelevu. Jipe muda wa kutosha ili upate muonekano unaotaka.
Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023
No comments:
Post a Comment