Unapoanza
kupamba ndani ya nyumba iwe ni mbunifu au ni mwenye nyumba mwenyewe, anajiuliza
ni mtindo upi nichague? Je mandhari gani ninayotaka kutengeneza? Ni mtindo upi
utavutia kwenye hiyo nyumba? Iwe unapamba chumba kimoja au nyumba nzima maswali
haya yote yanaamua matokeo ambayo
baadaye utajisikia vizuri katika mazingira hayo.
Kwa
ujumla kuna aina 4 zilizo maarufu zaidi katika
mitindo ya kupamba ndani ya
nyumba. Hata hivyo mitindo mipya inabuniwa kila leo lakini kwa hii minne
utapata uelewa wa msingi na tofauti kati ya mtindo mmoja na mwingine
kimuonekano.
Huenda
wewe ni mbunifu na mteja wako anataka mtindo wa saresare, huwezi kumbadilishia
na kumfanyia wa kisasa kwa ajili anaamini anachokitaka ndicho ladha yake na
ndicho atakachoweza kuishi nacho vizuri. Ifuatayo ni mitindo mine maarufu
zaidi:
1. Mtindo wa kisasa (modern/
contemporary)
Tabia kuu za mtindo huu ni kuwa na vitu vichache
muhimu ambavyo kila kimoja kinatumika. Yaani kinachoangaliwa ni uwepo wa kitu
chumbani kwa ajili ya matumizi na sio kuwepo kama pambo pekee. Kuta hazipakwi
rangi nzito na msisitizo ni uwepo wa vitu vichache sana na upambaji wake ni
mrahisi. Eneo kubwa la chumba linakuwa wazi, safi na hakuna vitupio vidogodogo kama
kwenye mitindo mingine. Kitu chochote ambacho ni pambo tu na huwezi kukitumia
hakina nafasi kwenye mtindo wa kupamba kisasa.
Mtindo huu unatumika na kufaa zaidi kwenye vyumba/nyumba
ndogo. Kuna baadhi ya watu wanahisia kwamba kupamba kwa mtindo wa kisasa
kumerahisishwa sana na ni mtindo wa kichoyo. Ila watu wanaopenda utulivu na
hasa nyumba zenye watu wa makamo wanapendelea mtindo wa kisasa.
Sasa, ni
vyema kufahamu kuwa maneno haya mawili (modern na contemporary) yanatumika
kuelezea upambaji wa kisasa lakini kuna
tofauti ndogo sana kati yake. Upambaji wa contemporary
ni kwamba pamoja na vitu vichache ila ni vile vilivyoko kwenye chati kwa
kipindi hicho tu wakati upambaji wa modern
ni vitu vichache vilevile lakini
inawezekana visiwe kwenye chati kwa wakati huo.
2.
Mtindo
wa saresare (classic)
Mtindo
wa saresare unasisitiza mpangilio na uwiano. Tabia kuu ya mtindo huu ni kuwa na
eneo la kitovu cha chumba ambapo ndio macho yanaelekea ufikapo chumbani hapo,
kwa mfano eneo ilipo luninga. Baada ya kuwa na eneo hilo kinachofuata ni
kupamba kwa kugawa chumba pande mbili na kila kitu kwenye upande mmoja
kinafanana na upande wa pili. Vitupio vingi kama mito ya vitambaa vya pamba,
silki au velveti na picha za ukutani za
kanvasi vinatumika katika mtindo huu. Chumba kinakuwa sawasawa pande mbili kiasi
kwamba ungekigawa katikati, vitu vilivyoko upande mmoja ndivyo vitakuwepo
upande wa pili huku eneo la kitovu likiwa limeainiswa. Nyumba nyingi za kisasa
za Kitanzania zinaangukia kwenye mtindo huu.
3.
Mtindo
wa kiutamaduni
Katika
mtindo huu fenicha na mapambo ni mazuri na yana muonekano wa utamaduni wa watu
fulani ila mapambo si mengi. Sehemu kubwa ya mapambo kama pazia na michoro ya ukutani
ni ya kiutamaduni na fenicha zimekaa kisanaa zaidi.
4.
Mtindo
wa mchanganyiko
Katika
kutumia mtindo huu mpambaji au mbunifu anachanganya mapambo ya mitindo mitatu
ya juu na kutengeneza huu mtindo wanne.
Kazi
kwako mpambaji, naamini umenufaika kiasi cha namna ya kuweza kuchagua mtindo
hata mwenye nyumba akikuambia nataka unipambie kwa muonekano fulani kwa mfano contemporary basi huna haja ya
kubabaika tena. Kupitia makala hii yeyote anayetaka kupamba awe ni mpambaji
mtaalam au mwenye nyumba mwenyewe amejua kipi ni kipi na anaweza kuamua mtindo mmojawapo
kati ya hii huku akijua matokeo yataleta mandhari gani.
natfuta hizo vitambaa vya kanvasi kwa hapa dar ntapata wap?
ReplyDelete