Huenda unapamba upya eneo la nje ya nyumba yako kwa
kuboresha vilivyopo, bila shaka unataka kupata muonekano mpya ambao utaupenda
bila kutumia gharama kubwa. Kwa kuwa na mito ya gharama nafuu unaweza
kutengeneza muonekano wa kuvutia unaoutaka.
Nakupa dondoo hatua kwa hatua za njia rahisi za kukuwezesha
kupata mito ya namna hiyo ili kuondoa ile ambayo imesinyaa au foronya
zimepauka, zimechakaa au
chochote kile kinachochangia usiipende tena mito yako
hiyo!
Kabla hujanunua au kutoa oda ya kutengenezewa mito yako,
au hata kutengeneza mwenyewe, unatakiwa kujua muonekano wa mwisho unaoutaka.
Angalia ile ambayo ulikuwa nayo tayari na uone
kama unahitaji kuiboresha ama kununua mingine. Kuboresha mito kuko kwa
aina mbili.
Aina ya kwanza ni kuboresha kwa kuongeza sufi ile mito iliyosinyaa
na aina ya pili ni kuboresha kwa kubadili foronya zilizochakaa.
Kuongeza sufi isikuogopeshe. Unaweza kununua mito mikubwa
ya mitumba (ambayo ni bei rahisi zaidi ya mipya) na ukatoa ile sufi yake
ukajazia kwenye mito yako unayotaka kuboresha kutoka kwenye kusinyaa.
Au
unaweza kuweka sufi kidogo iliyopo kwenye mito ya zamani eneo la katikati tu na
kwa nje ukazungushia godoro jembamba. Mbinu ni nyingi, angalia mito yako halafu
fanya maamuzi sahihi.
Mito ya bei rahisi ipo katika mifumo mingi. Unaweza kununua
godoro halafu ukalikatakata vipande kwa ukubwa wa mito unayotaka, ukashonea
foronya na ukapata mito ya kukalia juu ya viti vya chuma bila kuhitaji sufi
yoyote.
Unaweza kuchanganya mito midogo na mikubwa na pia unaweza
kuwa na ya maumbo mbalimbali na ikakuwakilisha kwamba unapendelea nini.
Vitambaa vya kushonea foronya za mito ya fenicha za nje
vipo vya aina nyingi kama ilivyo kwa sofa. Rangi na michoro ya kuendana na
mazingira ya nje zinapendeza zaidi. Rangi hizo ni zile za udongo na mimea na
maua yaliyopo kwenye eneo lako. Unaweza
ukaamua kutumia malighafi za kitambaa au mpira kutengenezea foronya hizo.
Uzuri
wa mpira ni kwamba ni rahisi kwa utunzaji iwe ni kufuta vumbi au maji kulingana
na mahali fenicha hizo zilipo.
Tengeneza mito ambayo utakuwa na stori ya kuielezea.
Inawezekana umeitengeneza kipindi ambacho kilikuwa na umuhimu fulani
kwako.
Nyakati hizi za digitali kila
kitu kinawezekana, unaweza kuweka picha au maandishi ya mahaba au imani kuelezea
kumbukumbu na hisia zako kupitia mito hiyo ya viti vya nje ya nyumba yako.
Ikiwa una eneo lolote linakutatiza kuhusu mapambo ya nyumbani kwako, wasiliana na mimi 0755 200023
Nifuate Instagram: vivimachangehomes
No comments:
Post a Comment