Je wewe ni mzazi na una lundo la midoli kila
mahali kwenye nyumba yako? Kama unahisi swali hili linakugusa basi sio wewe
peke yako mwenye changamoto hii. Ni asili kwa mzazi kupenda kumnunulia mwanae
midoli na michezo mbalimbali ya kidigitali na elektroniki inayoendana na
wakati, na hasa kwenye siku ya kuzaliwa au sikukuu ndipo inakuwa mingi zaidi.
Nimeshuhudia
nyumba zenye watoto ambapo midoli na
michezo imesambaa kila mahali, sio tu
inaonekana kama janga ndani ya nyumba, bali pia ni hatari kwani unaweza
ukaikanyaga kwa bahati mbaya ikakuangusha au hata kukutegua mguu.
Maisha
yetu ya mchakamchaka hayatoi muda mwingi sana wa kuweka mpangilio ndani ya
nyumba zetu. Na kazi hiyo saa nyingine inachosha manake unakusanya midoli na
hapohapo watoto wanairudisha tena walikoitoa, usicheke! Najua wazazi na walezi
wengi hii inawachosha.
Kuna
suluhisho rahisi la changamoto hii ya kuhifadhi midoli na michezo ya watoto kwa
kuwa na vifaa vya kukuwezesha kuweka mpangilio, ambapo wanao watakuwa sehemu ya
sebule na kuifurahia lakini sio kuiteka
yote kwa kusambaza midoli na michezo yao kila mahali. Kuleta uwiano huu
unahitaji vifaa kadhaa vya fenicha ambavyo huenda baadhi tayari unavyo.
Tenga
eneo la kabati linaloweza kuhifadhi mrundikano wa midoli hiyo ambapo likiwa
limefungwa haionekani. Linaweza kuwa kabati kubwa au hata fupi tu. Ukishakuwa
na eneo hili basi ndani yake weka vikap au vitenga vidogo dogo kwa ajili ya
watoto kuwekea ile midoli na michezo wanayotaka kuchezea kwa wakati huo.
Kama
umewachunguza watoto kwa karibu ni kwamba hawachezei midoli yote kwa wakati mmoja, huwa wanachagua kadhaa. Kwahivyo wape
maelekezo kuwa wanayotaka kuichezea ndio waweke kwenye vikapu, kama ni mtoto zaidi
ya mmoja kila mmoja awe na kikapu chake. Mingine ibaki kabatini. Uwe tu na
vikapu vya kutosha kwenye kabati hata kama hawavitumii kwa wakati huo, ila
wawekee kanuni kuwa kila mmoja awe na kikapu kimoja kwa wakati mmoja.
Mara
wanapomaliza kucheza kila wakati uwe unawasisitiza kurudisha midoli yote kwenye
vikapu na kuimimina kabatini, watakaporudi tena kwenye michezo watachukua
vikapu vitupu wachambue tena upya wanayotaka.
Nakushauri
pia ni muhimu kuwa na kabati la luninga lenye nafasi kwa ajili ya kuhifadhi midoli
na michezo midogogogo.
Ukiwa na sehemu hii inakusaidia kuondoa mrundikano wa
midoli sebuleni au chumba cha luninga. Kama huna kabati la namna hii na tayari
ulishasimika luninga yako ukutani ni rahisi kutengeneza fenicha ndogo ya bei
nafuu na ukaiweka chini ya dirisha au kwenye kona kwa ajili ya kuhifadhia midoli
hiyo. Na fenicha ya namna hii iwe na muonekano wa kitoto ndipo watapenda zaidi
kuitumia.
Angalia
ndani ya nyumba yako kwa jicho la ziada. Kama midoli na michezo imesambaa kila
mahali kama vile ni darasa la chekechea, inawezekana ni muda unaotakiwa kufanya
mabadiliko. Unaweza ukawa na nyumba nadhifu yenye mpangilio na watoto wenye
furaha na michezo yao kwa wakati mmoja. Ikiwa hivi bila shaka utafurahia
unapoishi.
Vivi ambaye ni mshauri wa mapambo ya nyumba, simu 0755
200023
ni follow instagram @vivimachangehomes
No comments:
Post a Comment