Monday, February 15, 2016

Faida za kumshirikisha msanifu wa majengo kwenye nyumba unayotaka kujenga



Kununua ardhi na kutaka kuanza kujenga nyumba yako bila shaka ni hisia nzuri. Je, kuna kitu kizuri zaidi ya kubuni na kupamba nyumba yako mwenyewe?

Bila shaka hamna! Ukimiliki nyumba unajisikia ni kama huhitaji kitu kingine zaidi katika maisha yako. Mahitaji makuu ya msingi ya binadamu  ambayo ni chakula, mavazi na malazi yanapatikana pale ambapo kuna
nyumba.
Lakini kuna kitu unachotakiwa ujue kwamba pale unapotaka kujenga nyumba ni muhimu kuwa na ramani inayotoka kwa msanifu wa jengo. 

Unajiuliza kwanini? Msanifu wa majengo kazi yake ni kuchukua mawazo yako wewe unayetaka kujenga na kuyabadilisha kuwa mchoro unaokubalika kwenye ujenzi. Bwana David Sembuyagi ambaye ni msanifu wa majengo anatupa faida za kumshirikisha msanifu ili akuchoree  ramani kabla ya kujenga nyumba .

Sio rahisi wewe unayetaka kumiliki nyumba kuweza kuibuni mwenyewe - Kuna vitu vingi vidogo na vikubwa ambavyo unapaswa kuvitilia maanani. Hata kama una kipaji cha ubunifu, bado unahitaji mtu ambaye anaweza kukuchorea ramani ya nyumba nzima kitaalam. Kumbuka kitu kimoja, ni gharama kubwa mno na pengine huwezi kuja kuvunja nyumba nzima kwa ajili uliijenga vibaya!

Mtaalam huwa anatumia uzoefu wake - Kama uko kwenye nyanja nyingine hutegemewi kuweza kusanifu ramani ya nyumba kitaalama kwa namna ambapo msanifu mtaalam angefanya. Ana uzoefu wa kutosha na uwezo wa kufanya kazi yako bila wewe kuwa na wasiwasi wowote  ambapo itakusaidia kupunguza msongo wa mawazo mbeleni!

Huwa gharama zao sio kubwa sana, kama ndio wasiwasi wako - Labda uwe muflisi kabisa, vinginevyo una gharama kidogo ya kulipa kwa ajili ya ramani. Habari njema ni kwamba baadhi ya hawa wataalam wako tayari kukufanyika kazi yako kwa bei ya makubaliano.

Kama hutaki msanifu akuchoree ramani basi walau mwache akuongoze -Kuna baadhi ya watu ambao ni wasumbufu kiasi kwamba wanaweza kubuni nyumba nzima peke yao. Kama wewe ni mmoja wao, mtumie msanifu akuongoze kwa jambo hilohilo. Mpe nafasi atumie utaalam wake kukuwezesha kupata nyumba sahihi.
Unapata mtu wa kumshirkisha ndoto yako - Ile tu msanifu kukusikiliza, halafu kukubunia ramani, inakupa hali ya kujiamini!

Mwisho kabisa  ni kwamba kisheria unapoanza ujenzi unatakiwa kuwa na kibali. Kibali hakipatikani bila kuwa na ramani ya jengo.


Vivi ni mshauri wa mapambo ya nyumba.  Je kuna lolote linakutatiza kuhusu namna ya kupendezesha nyumba yako? Nijulishe 0755 200023

Nifuate instagram: vivimachangehomes

No comments:

Post a Comment