Kwa wenye nyumba wengi na hata wale wanaotarajia kumiliki
nyumba zao wenyewe, marumaru bado
zinabaki kuwa chaguo namba moja kutokana na mtindo wake ambao ni rahisi kwa
matumizi, bei nafuu na hata upatikanaji katika rangi na maua mbalimbali. Iwe
unaweka marumaru jikoni ukuta mzima hadi kufikia dari au hadi mahali fulani
hapo kati, kutumia moja wapo kati ya aina za marumaru kutalipa jiko lako
muonekano wa kuvutia.
Jiko lina sehemu nyingi ambazo marumaru zinaweza kuwekwa.
Itapendeza kama utatumia marumaru ambazo ni sahihi kwa kila eneo. Unaweza
kutumia marumaru sakafuni, ukutani na vilevile kwenye kaunta.
Moja kati ya vitu muhimu kukumbuka kuhusu marumaru za jikoni ni kuweka zile
ambazo hazipitishi maji.
Marumaru/vigae visivyokuwa na ukanda wa kioo na pia
mbao zikiwekwa jikoni katika maeneo yanayogusa maji zinaweza kuharibika haraka
kwa namna mbalimbali kama vile kuwa na madoa. Nimeshirikiana na
muuzaji wa duka
la marumaru jijini Dar salaam bwana Huruma Ally kukujuza aina tofauti zifuatazo za marumaru zilizopo sokoni
ambazo zinazofaa kwa jikoni:
Marumaru za Seramiki
Marumaru za seramiki ni maarufu sana na zimesambaa maeneo
mengi. Ni nzuri kimuonekano na kwa matumizi pia. Hii ndio sababu wenye nyumba wengi
wanachagua kuzitumia ndani ya jiko. Marumaru hizi zinahimili joto, ni imara na
zinapatikana kwa mitindo na rangi mbalimbali. Marumaru za seramiki zinaweza
kutumiwa kwenye sakafu, ukutani na kaunta.
Marumaru za Poselini
Ingawa marumaru za seramiki na poselini zote
zimetengenezwa kwa udongo uliochanganywa na malighafi nyingine, hizi za
poselini ni ngumu na imara zaidi kuliko za seramiki. Na wakati zile za seramiki
zinaweza kubadilika rangi baada ya kukanyagwa sana, hizi za poselini unene wote
wa marumaru ni rangi moja kwa maana ya kwamba hazibadiliki na wala hazionyeshi
alama za kukwaruzika. Marumaru hizi zinapatikana kwa rangi za mfumo
usiong’aa wa mati na wa kung’aa wa
polishi. Gharama ya marumaru za poselini huwa ni kubwa kwa mara 2 zaidi ya
zile za seramiki. Sawa na seramiki, marumaru za poselini unaweza kuzisimika
popote jikoni.
Marumaru za kioo
Hizi nazo ni madhubuti na imara kama za poselini.
Zinatabia ya kuonekana mithili ya kioo na hata ukiwa unazitizama unajiona picha
yako kama kivuli. Zinafaa yale maeneo ya kuweka madoido kama vile eneo la
kupakulia chakula.
Marumaru
za jiwe
Marumaru
za jiwe ni sahihi kwa muonekano wa kifahari. Ni za gharama japo za bei nafuu
zipo pia. Kama unataka marumaru za jiwe kwa
bei rahisi changua granite ila la gharama
chagua marble. Mwenye nyumba
asiyetaka jiwe lakini anataka muonekano wa kifahati eneo fulani la jiko basi
weka marumaru ndogondogo za mosaic
zile tunazoshuhudia zaidi kwenye kupamba nguzo.
Marumaru za plastiki
Hizi ni marumaru zinazotokana
na plastiki nene na ngumu, ni rahisi kusimika na ni bei rahisi sana. Zinafaa kwa
kuta za jiko lakini ni rahisi kukwaruzika na zinahitaji utunzaji wa karibu.
Kwenye
kuchagua hizi marumaru za jikoni ni vyema pia ujue unataka kuziweka kwenye
muundo upi. Kuweka kwa msharazi kunavutia eneo likiwa kubwa ila ukae ukijua
kwamba marumaru zinazofaa kwa uwekaji huu ni zile ambazo pande zote nne zinalingana.
Na pia uwekaji wa mshazari unachukua vipande vingi zaidi kwa asilima 10 ya
uwekaji wa kawaida. Inahitajika kazi kubwa zaidi hasa kukatakata kwa hivyo na
gharama ya mwekaji wa mtindo wa mshazari
unaweza kuongezeka.
Je msomaji wangu kuna mahali panakutatiza kuhusu muonekano wa nyumba na bustani? Tuwasiliane 0755 200023 na pia tembelea mshirikishe na mwenzio blog hii ili anufaike kama wewe. www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment