Leo nimeona niandae makala kuhusu namna mwenye nyumba
anavyoweza kusimamia kwa mafanikio mradi wa ujenzi wa nyumba yake. Baadhi ya wazazi wa familia changa wanaanza
ujenzi bila kuwa na
uzoefu wowote na wakati mwingine baba yuko na pilika za
kutafuta riziki ya familia wakati mama akiwa ndio msimamizi wa ujenzi huo.
Hivyo basi kwa kuliongelea hili litawasaidia wale wanaojenga kwa mara ya kwanza
na pia wale wenye mpango wa ujenga siku za mbeleni.
Nimeongea na mhandisi wa majengo
bwana Kassim Ally na hapa anatujuza kama ifuatavyo. Wakati wa kufanya kazi
kubwa ya ujenzi wa nyumba ya kuishi, mambo kama wauzaji wa vifaa bora, gharama
na muda ni mambo yanayotakiwa kutiliwa maanani. Ingawa kuwa na uwezo wa
kufikiria mbele katika kila hatua ya ujenzi ni lazima, kazi yenye mafanikio
inahusisha pia ushauri wa malighafi zinazotakiwa kwa hatua hiyo.
Kila mmoja ambaye ameshawahi
kujenga au kusimamia kazi ya ujenzi anajua ni kwa namna gani ilivyo na
changamoto nyingi. Hivyo basi kusaidia kuwezesha mradi ufanikiwe, hapa ni
kanuni 5 za namna ya kusimamia ujenzi wa nyumba ya kuishi ili kuhakikisha unapata
matokeo uliyoyataka.
1. Andaa mipango mapema
Ujenzi usiokuwa na
mipango iliyoandaliwa ni moja ya changamoto kubwa kwenye ujezi wa nyumba za
makazi. Ingawa dharura bado inaweza kuwepo lakini mambo mengi yanaweza kukamilika
kirahisi pale kunapokuwa katika mipango ya mapema. Mambo kama hali ya hewa ya
wakati wa ujenzi ni lazima yafikiririwe vinginevyo yanaweza kusababisha gharama
za ziada kwa kusababisha mradi kuchelewa. Kimsingi kila kitu ambacho kinaweza
kukwamishwa ujenzi lazima kifikiriwe kwanza.
2. Pitia bajeti yako kila wakati
Katika ujenzi wowote
uwe mdogo au mkubwa, ni vyema kuwa na pesa ya kutosha hadi kumaliza hatua fulani.
Kabla hujaanza kuongea na mafundi, unapaswa kujua hali yako kipesa na uhakika
wa wapi unapata hela ya nyongeza endapo utakwama. Mara nyingi miradi ya ujenzi
inaishia kuongezeka bajeti ya kati ya asilimia 10 hadi 15, ni lazima kila siku
uweke jicho kwenye hela uliyonayo na matumizi yanayotakiwa.
3. Chagua watu sahihi
Hakikisha unampata
fundi mkuu aliye sahihi. Anatakiwa aijue bajeti yako kwani ana uwezo wa kukupa
mbadala na ushauri uli ufanye matumizi ya busara.
4. Mfanye kila fundi ajue kifuatacho
Kama tunavyojua ujenzi
unapitia hatua mbalimbali, na ili kuondoa lawama au hasara inayoweza
kusababishwa kati ya fundi wa nyuma na anayemtangulia ni vyema kuhakikisha kuna mawasiliano na kila
fundi aliyeko eneo la ujenzi. Kunapokuwa na mawasiliano kati ya mafundi
kunasaidia kushughulikia mapema na mara moja tatizo ambalo limejitokeza.
5. Amini dhamira yako na furahia nyumba yako mpya
Ujenzi wa nyumba ya
kuishi bila shaka ni ujenzi wako wa kwanza kusimamia hadi kukamilisha. Unaweza
kuwa umechoshwa na maelezo mengi na michakato uliyopitia. Cha muhimu ni kwamba
wakati unafanya maamuzi yoyote juu ya nyumba yako hiyo, amua kile ambacho
unaamini kuwa ni sahihi kwako.
Safari ni ndefu na
bila shaka unataka kuhakikisha unafurahia matunda yake.
Nishirikishe ulivyosimamia mradi wa ujenzi kwa mafanikio. Mawasiliano 0755200023.
No comments:
Post a Comment