Kati ya vitu vyote unavyozingatia wewe mwenye nyumba wakati
unapotazama nyumba yako, kukagua, kusafisha na kupaka rangi paa linaweza kuwa
ni kitu cha mwisho. Nimeona watu wakipendezesha nyumba ndani, nje na bustani lakini
paa likisahaulika. Ingawa huenda paa si kipaumbele chako kati ya vitu
unavyotazama kwenye utunzaji wa nyumba, bado haimaanishi kwamba halitakiwi
kutunzwa na kuwa na muonekano wa kuvutia. Nyumba yako bila shaka ni
moja kati
ya rasilimali za thamani zaidi ulizonazo, unapaswa kuitunza kwa kuzingatia maeneo
yote yanayoihusu. Kuita wataalamu wenye uzoefu wa matunzo ya paa kila baada ya
kipindi ni jambo muhimu.
Mtaalam wa mambo ya paa bwana Philemon Nkane anatueleza
kwa kina kuhusu utunzaji wa paa. Anasema
kwanza kabisa ni vyema ifahamike kuwa utunzaji wa paa unahusisha pande mbili,
wa kwanza ni mwenye nyumba na wa pili ni mtaalam.
Umakini mkubwa
unatakiwa wakati wowote wa kufanya kazi kwenye paa. Kutembea juu ya paa ni hatari,
kwahivyo mwenye nyumba usie mtaalam wa kazi hiyo hutakiwi kupanda juu ya paa.
Vinginevyo unaweza kulitazama ukiwa eneo tambarare kama pale juu ya zege la
varanda. Laa kama haiwezekani kabisa basi muite mtaalam.
Zifuatazo ni dondoo za
jinsi ya kutunza paa ili lidumu muda mrefu:
Mwenye nyumba unatakiwa kuhakikisha kuwa matawi ya miti
yanapunguzwa kiasi kwamba hayafikii mfumo wa paa, kwani majani kudondoka na
kuozea juu kunachangia kuliharibu.
Mifereji ya maji ya mvua iliyopo kwenye paa na
inayolizunguka inapaswa kusafishwa na kuzibuliwa ili ibaki wazi kwani takataka
kusimama ndani zikiunganika na maji itasababisha mafuriko ya paa hivyo
uharibifu.
Ukarabati wa paa hasa la vigae ni muhimu sana kwani vipo
vinavyopata nyufa bila mwenye nyumba kuwa na habari. Kuviondoa mapema inasaidia
paa lisiingize maji na kuharibu dari hatimaye vitu ndani. Kama hujawahi kuita
mtaalam wa kukagua paa lako kwa zaidi ya miaka
8-10 ni muhimu kufanya hivyo ambapo huenda kuna marekebisho ya kufanyika
haraka.
Endapo paa limeota ukungu lisafishwe kwa dawa ya kuua fangas na
maji yenye msukumo mkubwa, na hata ikiwezekana lipake rangi upya. Waite
wataalam wanaohusika na kazi hii watakushauri.
Wakati wa kusimika vifaa kwenye paa kama vile vifaa vya umeme jua
au dishi la satelaiti hakikisha pamoja na wataalam hao, pia anakuwepo mtaalam
wa paa.
Muite mtaalam haraka sana pale unapohisi paa linavuja kwani dalili
ya kwanza ni kuona sehemu ya dari ikibadilika rangi na hapo ndipo marekebisho
yatahitajika haraka.
Paa linapokuwa salama mwenye nyumba naye anakuwa salama. Litunze lidumu.
Je unahitaji ushauri wowote tuchat kuhusu mapambo ya makazi yako, kuna mahali panakutatiza? Utalipia mara moja tu na tutachat hadi matatizo yako yaishe bila kujali itachukua muda gani. Unatakiwa kuwasiliana na mimi simu 0755 200023.
No comments:
Post a Comment