Thursday, November 13, 2014

my article for newspaper: vioo vya mapambo

Boresha muonekano wa ndani ya nyumba kwa kuweka vioo vya mapambo.

Vioo vina kitu kwakweli ambacho ni maalum ndani yake. Vinakusaidia kukujulisha unaonekanaje na pia kukuwezesha kujiweka jinsi ambayo unataka uonekane. Zaidi ya haya maandalizi binafsi na kujiridhisha na muonekano wako kabla hujatoka, vioo vinasaidia pia kwenye kupamba ndani na hivyo kufanya muonekano wa nyumba kuwa maridadi na nadhifu zaidi kwa kila mgeni anayekutembelea.

Kama kuna pambo la ndani ambalo wenye nyumba hatakiwi kulikosa, basi ni kioo. Havitumiki tu kujiangalia unapoingia, bali vina mahadhi yake kwenye kuongeza staili ya chumba au muonekano wa kupagawisha kwa kumfanya mgeni kuduwaa. Sababu nyingine kuu hapa ni kuwa vioo vinaweza kuwa  na bajeti rafiki. Ni kweli kuwa kuna vioo ambavyo ni lazima viwepo nyumbani kwa matumizi kuwa watu wanahitaji ili kuhakikisha kuwa wanaonekana jinsi wanavyotaka kuonekana, lakini leo kwenye makala hii tunaongelea vioo kama mapambo ambavyo unaweka kwenye ukuta wa nyumba yako ili kuongeza staili na ukubwa.

Utagundua kuwa leo, sokoni kuna aina nyingi na tofauti za miundo na aina za vioo. Watengenezeaji wa vioo vya mapambo wanakuja juu kwa kuongeza ubunifu hasa wa fremu wanazofungia vioo hivi. Unaweza kuvipata vioo hivi vikiwa kwenye fremu ya kila malighafi unayohitaji kwa mandhari unaotaka kutengeneza.
Fremu nayo ni kigezo muhimu cha kioo kuwa kifaa cha mapambo. Unaweza kuagiza kioo kwa umbo unalotaka kwa mfano unaweza kuwa na kioo kwenye ukuta wa sebule ambacho kinatoa sura kwenye taswira nne kwa jinsi ambayo ukijitazama unaona uso nne zinazofanana.. Haijalishi staili unayotaka au bajeti uliyonayo, kuna uhakika wa kupata kioo ambacho ni sahihi kwa mradi wako.

Sababu ya kuweka vioo hivi ndani ya nyumba ni ukweli rahisi kuwa unataka kutumia ile hali ya kujiona ndani ya kioo kwa faida ya kimapambo. Baadhi wananunua vioo na kuvitundika kama sanaa nyingine za ukutani, kwa maana ya kuwa wanakitundika katikati ya picha na fremu nyingine, au wanakiweka kwenye ukuta ambao hauna kitu kingine ambacho kingefaa hapo. Hata hivyo unaweza kutumia vioo vya mapambo kuakisi mwanga na vifaa. Kwa mfano unaweza kuwa na ujia (corridor) ambao una mlango upande mmoja lakini mwingine hauna. Pambo lako hapo linaweza kuwa mmea wa kijani (uwe hai au mfu) pale kwenye ukuta usiokuwa na mlango pamoja na kioo. Kioo kitauakisi ujia kwa kuukuza uonekane mpana na mrefu. Kupamba kwa vioo kunafanya eneo dogo lionekane kubwa na mbinu hii inatumika na wataalam wengi wa ubunifu wa ndani nyumba.

Kupamba kwa vioo kunaongeza mwanga wa chumba. Chumba kilichopakwa rangi ya giza kinaweza kuonekana kidogo, kuongeza vioo kwenye kuta zake kutaboresha mwanga. Njia sahihi zaidi ya kuongeza mwanga wa jua bila kuongeza taa ni kufunga vioo vitazamane na madirisha. Vioo vinadaka mwanga wa jua toka dirishani na kuusambaza chumba kizima. Hii inaweza kuwa njia mojawapo pia ya kubana matumizi badala ya kuwasha taa mchana.

Kupamba kwa vioo vya mapambo hakuhitaji mtaalam. Mtu akiwa na vifaa vya toolbox anaweza kufunga vioo ukutani  na kutengeneza chumba chenye muonekano mzuri kwa gharama nafuu.
Chagua vioo vyenye maumbo ya kuvutia, pembe nne ni nzuri ila vioo vyenye maumbo yasiyozoeleka vinafanya umaridadi zaidi. Tafiti aina na maumbo mbalimbali ya vioo kabla hujamua ni vipi unataka.

Ili kukifanya chumba kisicho na uwiano kionekane kuwa nao, funga vioo vya mapambo ukutani. Vioo hivi viwekwe kuakisi vitu fulani kwenye chumba ili kufanya ionekane kama vitu hivi viko katika kila upande wa chumba, kwahivyo pale unapoingia uone kama chumba kina uwiano na ni kikubwa.

Baadhi ya wenye nyumba wanatamani waboreshe muonekano wa ndani wa nyumba zao. Marekebisho yana gharama kubwa, hata hivyo wewe mwenye nyumba usizime tamanio lako. Unaweza kunyanyua uso wa ndani ya nyumba yako kwa kutumia vioo vya mapambo badala ya marekebisho makubwa.. Mradi huu mdogo wa kunyanyua uso kwa kutumia vioo unaweza kukupa matokeo usiyotarajia. Kupamba kwa vioo ni moja kati ya njia nyepesi na rahisi za kuboresha muonekano wa ndani ya nyumba.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com



Saturday, November 8, 2014

tv cabinet ni moja kati ya post zangu iliyopendwa kuliko...

nakuongezea hapa dondoo chache za muhimu kabla hujanunua kabati la tv, twende kazi...
kabati hili ni moja kati ya fenicha ya msingi hapo sebuleni ambapo unakutana na marafiki zako, kula dinner na kuangalia tv. Wakati unapotaka kununua kabati la tv, ukubwa wa tv yako unahusu.
wakati wa kununua usifikirie tv tu. fikiria pia vitu vidogodogo ambavyo vinatakiwa kuwa hapo lakini vihifadhiwe, kwa mfano remote, kwahivyo nunua kabati lenye droo moja au mbili na hata likiwa pia na shelfu itakuwa poa zaidi.. kwahivyo kumbuka kuwa usifikirie tv tu.
la mwisho lakini si dogo unatakiwa uamue malighafi na rangi za kabati lako. kuna makabati mengi ambayo machoni yanavutia lakini kwa ubora si lolote si chochote. kwa swala la rangi hakikisha una research hadi uone kitu kinachokuvutia ndio ununue. Good luck!



super saturday na marafiki zangu wa ukweli...

hapa na pale leo na watu wangu wadogo...

 pozi la kibaunsa..sungusungu wangu
 pozi zikazidi hadi rafiki akalamba chini
akanyanyuka akijongea tartiiibu

Friday, November 7, 2014

njia rahisi kabisa ya kupamba sebule

kwa vile sebule ni sehemu muhimu ndani ya nyumba inahitaji kutupiwa jicho zaidi ya nyingine zote na ni lazima ipambwe kwa njia mbalimbali ili iwe na mvuto mbele ya kila mgeni anayekutembelea, na hii wala si ngumu.
kwanza kabisa weka fenicha zenye mvuto ambazo ni sofa, vimeza vya kando, kimeza cha kati, meza ya chakula na viti vyake.
weka taa maridadi na zenye mwanga wa kutosha kumulika sebule yote. weka taa za vivuli juu ya meza na sakafuni ili kuleta matokeo makubwa. kama wewe ni mshabiki wa wallpaper chagua ukuta wa tv ubandike, ning'iniza picha na fremu ukutani na hata vikapu vidogodogo vikiwa na maua ya kutengeneza.
weka vyungu vikubwa vya maua juu ya meza au sakafuni kwenye kona. weka kioo kikubwa katika ukuta wowote na upambe boda zake kwa fremu za kuvutia. unaweza pia kuweka sanamu kwenye kona na pembe za sebule yako.
mwisho kabisa usisahau kuweka pazia na fimbo za kuvutia.



Thursday, November 6, 2014

my article for newspaper: fenicha za kwenye bustani na varanda

Zingatia haya kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba


Fenicha za nje ya nyumba pia zinajulikana kama fenicha za kwenye bustani au varanda.  Aina hii ya fenicha huwa imetengenezwa kwa malighafi inayozuia maji kupenya, kwa kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya nje. Fenicha za  nje ya nyumba zimekuwa zikitumika toka enzi za himaya ya Roma.

Fenicha za nje ya nyumba  ni muhimu kwa mikutano wakati unapokuwa na kikundi cha watu kwa ajili ya siku maalum kama vile siku ya kuzaliwa na kadhalika. Hakuna kinachofurahisha zaidi kama kuwa na kiusingizi kwenye upepo mwanana wa kwenye varanda au bustani. Kuwa na chakula cha usiku na mwenzi wako wakati nyota ziking’aa angani inakuwa ni mahaba zaidi ya ndani ya nyumba.

Ila kuna jambo linalofanya aina hii ya fenicha kuwa tofauti na zile za ndani; malighafi ya fenicha za nje ya nyumba ni lazima iwe imara kwa sababu fenicha zitapambana na mvua kubwa, jua kali, upepo na baridi kali. Je hali ya hewa ya unapoishi ni joto na ukame, au unaishi karibia na pwani? Mvua ni za mara kwa mara? Haya yote ni maswali muhimu ya kupatikana majibu kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba. Hapa ni sababu, hali ya joto na ukame inafanya mbao kupasuka. Upepo mkali unaweza kufanya fenicha za aluminiam zipeperushwe.

Ndio maana ni muhimu sana kuhakikisha kuwa fenicha unazotumia kwenye mazingira ya nje ya nyumba ni sahihi kwa matumizi hayo.

Kwa malighafi, fenicha nyingi za kutumia nje ya nyumba zimetengenezwa kwa plastiki, mbao aluminiam na chuma cha pua. Amua ni malighafi ya aina gani unataka kwa ajili ya fenicha zako za nje. Vitu vitatu ambavyo vitakusaidia kuamua ni hali ya hewa, utunzaji na muonekano. Baadhi ya malighafi kama vile aluminiam hazihitaji utunzaji wa kina. Chuma cha pua kinaweza kudumu kwa muda mrefu sana na kinamudu joto na unyevu. Hapa ni muhimu kufahamu kuwa fenicha za nje za mbao sio imara kama nyingine, kwa hivyo inatakiwa kuziweka dawa mara kwa mara, anasema mseremala Rajab Hamis.Bottom of Form

Fenicha za nje ya nyumba zinakusaidia kuongeza ukubwa wa makazi yako, unapata eneo zaidi la kupumzika hasa wakati ule ambao jua sio kali sana au mvua sio nyingi. Kwa hivyo fenicha hizi zinakamilisha ahadi ya mapumziko, burudani na raha kwa ujumla. Uchaguzi wa fenicha za nje unazingatia hatua zilezile za kununua fenicha za ndani. Japo kunahitajika umakini wa ziada kwa ajili ya tofauti  kati ya fenicha hizi mbili.

Fikiria ni eneo kiasi gani ulilonalo na lina umbo la namna gani. Je ni varanda ndefu na nyembamba au ni fupi pana? Tumia eneo na umbo la varanda au bustani yako kufahamu ukubwa wa fenicha zako za nje. Hakikisha unaacha nafasi ya kutosha kati ya fenicha zako ili uweze kupishana kirahisi. Tumia utaratibu ule ule wa kupanga fenicha za ndani. Kwa eneo dogo meza za ukubwa wa kwenye mgahawa na stuli zitafaa zaidi kwani zitachukua nafasi ndogo.

Ni wapi utakapoweka fenicha zako za nje, je kwenye bustani yako kuna eneo la kukaa ambalo lina paa? Na pia je fenicha zako zitakaa juu ya sakafu laini ya udongo na majani au zitakaa juu ya sakafu ngumu? Hii itakusaidia kuchagua malighafi ambayo itaoana na mazingira yako.

Hakikisha kuwa ukikalia fenicha zako unapumzika vyema. Hata kama viti haviji na mito unaweza kutengenezesha mito yako mwenyewe na uwe unaihifadhi ndani majira ambayo hutumii fenicha za nje. Jaribu fenicha za nje kabla ya kununua na hata kuzilaza kwa jinsi ambayo ungetaka viwe kama vitanda vya mchana.

Yote hayo yakiwa yameshasemwa bajeti yako ndio itaamua ni nini unachoweza kununua. Siwezi nikasisitiza ni kwa namna gani ni muhimu kununua fenicha imara zaidi unazoweza kumudu. Kama uchumi unagomba, bado kuna namna unayoweza kupata fenicha za nje zilizo imara kwa hela uliyonayo. Unaweza kupata fenicha za nje nzuri na imara kwa bei nafuu kabisa kwa kununua zile zilizotumika. Fenicha zinazouzwa kwenye minada ya wafanyakazi wa kimataifa wanaomaliza muda wao na hivyo kurejea kwao, ukizifanyia maboresho kidogo na kuzisafisha zinaonekana kama mpya, na huwa hizi zinakuwa na ubora unaokubalika. Unaweza pia kufikiria kubadilisha mito na makusheni kwa ajili ya kuhuisha fenicha za nje za zamani.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Thursday, October 30, 2014

My article for newspaper: Kupamba ndani nafuu na haraka

Njia za gharama nafuu na haraka za kubadilisha muonekano wa ndani ya nyumba yako.


Watu wengi wanafikiria kuwa kupamba ndani ya nyumba ni jambo kubwa na ambalo linahitaji hela nyingi. Lakini hii sio kweli, mtu anaweza kutafiti njia za kupamba nyumba kwenye mitandao au majarida ya mapambo ya nyumbani  na kuona ni njia zipi zinazoweza kumfaa kwa gharama aliyo nayo. Makala hii ni mojawapo ya vyanzo vitakavyokupa mawazo ya njia rahisi na za haraka zaidi za kupamba ndani ya nyumba yako kwa namna maridadi kabisa.

Kabati la mapambo ni njia mojawapo ya gharama nafuu na ya haraka ya kupamba ndani ya nyumba. Kabati hili unaweza kulitengenezersha kwa fundi kwa mtindo unaotaka wewe mwenyewe iwe ni kwa sehemu kubwa kuwa ni kioo kitupu au mchanganyiko wa mbao nusu na kioo nusu. Linaweza kuwekwa sehemu ya kona ya chumba.
Linapokuja swala la mapambo ya kabati la mapambo, eneo la ndani ndio la kujali zaidi. Pamoja na mtindo wa kabati husika vioo pamoja na taa ya ndani ya kabati vinamaliza kila kitu! Mapambo ya aina mbalimbali huwekwa ndani ya kabati hili na kuleta muonekano wa kuvutia. Na pia wengine hupendelea kuweka glass za kifahari za mvinyo za aina ya crystal na hii inalipendezesha mno kabati kwa kweli. Tunu sio kitu ambacho umenunua karibuni kwa hela nyingi. Ni kitu ambacho kina thamani kwako zaidi ya pesa inavyoweza kununua. Inaweza kuwa ni sanaa uliyopewa toka kwa bibi na imepitia vizazi kadha wa kadha hadi kukufikia wewe au inawezekana ni kitu kilichokuwa sehemu ya maisha yako ya utotoni au kitu maalum ulichopewa na mtu maalum. Ukizungusha macho yako kukitazama kinakupa burudiko la nafsi.

Ndani ya kabati la mapambo waweza weka pia mdoli wako ambao unadhani ni wa kipekee na unafaa kuwepo hapo. Pia waweza weka vitu mbalimbali kutoka sehemu tofauti za dunia. Zingatia kua huna haja ya kusongamani kila sanaa uliyonayo kwenye kabati lako la mapambo. Hakikisha unaacha nafasi kati ya kitu na kitu ili isilete muonekano wa mrundikano. Chochote ambacho unadhani kitafanya kabati lako lipendeze waweza weka humo.

Njia nyingine ya kupamba ndani kwa gharama nafuu na kwa haraka ni kwa kutumia maua ya kutenengeneza (maua mfu). Maua na mimea inafanya muonekano wa mahali uwe wa kuvutia. Mtu anaweza kuweka mimea na maua kadhaa ya kutengeneza katika sehemu tofauti tofauti za nyumba yake. Staili na rangi ya maua na mimea hii iendane na rangi ya chumba cha nyumba. Maua hayo yanaweza kuwekwa sakafuni au juu ya meza vilevile.

Mtu anaweza kutumia vibebeo vya mishumaa kupambia nyumba yake na ikaonekana maridadi. Unaweza kutafuta aina mbalimbali ya vibebeo hivi kwenye maduka ya mapambo ya ndani na unaweza kuchagua vya mbao au vya kioo.

Mito ni njia nyingine ya kupamba kwa gharama nafuu na kwa haraka. Unajisikia burudani ukiwa na mito ya staili na maumbo mbalimbali. Unaweza kutupia mito kadhaa ya  mapambo kwenye seti zako za sofa ambapo zitaleta matokeo makubwa na itakuwa vyema zaidi kama ukitumia mito ya rangi nyekundu na ya chungwa.

Badilisha muonekano wa madirisha kwa kubadilisha pazia na fimbo. Hii sio usumbufu kama ambavyo unaweza kufikiri kwani kuna maduka mengi yanayouza pazia ambazo zimeshonwa tayari. Na kwa swala la fimbo zake kwa ajili tayari kuna vishikizo vilivyotobolewa,  ni kiasi tu cha kuondoa fimbo ya mtindo mmoja na kupachika nyingine ya mtindo tofauti bila ya kutoboa ukuta tena.

Hizo ni njia za gharama nafuu na haraka zaidi za kupamba nyumba yako. Jaribu mojawapo na utarudi kunishukuru. 


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Wednesday, October 22, 2014

...the Big Man is taking care of us...


yani huu mchakamchaka unanifanya nashindwa hata kuwa na muda wa ku post. napata ukakasi nikiona watu 100 hadi 200 wamenitembelea lakini sijaweka post mpya, najua kuwa siwezi kuwa na close friends 100 na kuendelea hivyo wote hawa ni watu wangu ambao mngependa kuona na kusoma chochote toka kwangu...hata hivyo msijali wapendwa..soon nitafanya mambo..echuuuuuuuu...

Monday, October 13, 2014

---vitu vizuri---Je, unatumia hii unaponyoosha nguo zako?

spray starch inakuwezesha kunyoosha nguo zako kirahisi zaidi, kwani inaondoa mikunjo iliyokomaa, inafanya nguo zisitepete, inazipa harufu nzuri na kuzifanya zionekane mpya kila wakati. Utakapoanza kuitumia kumbuka kurudi kunishukuru...auchiiiii


Sunday, October 12, 2014

...my gifts from the Big Man...

...tumeshakula dinner, tumeshavaa pajama...tunamshukuru Mungu atupe usingizi mwororo...

Thursday, October 9, 2014

my article for newspaper: umuhimu wa kuondoa mrundikano


Majira haya ya kipupwe upepo ni mwingi na kazi ya usafi inaongezeka kwa ajili takataka nyingi kwa mfano majani makavu na vumbi zinapeperuswa kila mahali na wengi wanaofanya usafi hasa wa nje ya nyumba wanalalamika kuwa mazingira yanachafuka muda mchache tu baada ya kusafisha. Wengi wetu wanaliona hili na huku jua likiwa kali. Haijalishi unajali mazingira kiasi gani bali kuwa eneo ambalo limesafishwa vizuri kunakupa hisia za ukaribisho na kuhuisha nafsi na ni muonekano chanya kwako. Kuwa mazingira safi kunaongeza nguvu chanya kwenye mwili na mazingira yako. Ukiweza kudumisha usafi kwa kipupwe hiki basi utakuwa umeweza kutengeneza nguvu hii.

Lengo ni kuishi burudani na mazingira yako, ili nguvu iliyopo kwenye mazingira hayo ifanye kazi upande wako kuliko kinyume chako. Kwa jinsi tunavyoguswa na mazingira yetu ndivyo pia tunavyoakisi maeneo haya.Wengi wetu tulishaingia ndani ya jengo au chumba na mara hiyohiyo tukajihisi kuchefukwa. Kinyume na hapo, vilevile wengi tulishaingia maeneo na kutufanya kujisikia burudiko na utulivu wa nafsi. Kuwa katika eneo safi na tulivu kunaleta uwiano na starehe ndani ya mazingira hayo.

Katika mazirngira kitu nambari moja kinachozuia utengenezwaji wa nguvu chanya ni mrundikano. Mrundikano unaweza kutufanya kujisikia kuelemewa, msongo, kuchanganyikiwa na kukwama. Mrundikano ni pamoja na kitu chochote ambacho hakipendwi tena au hakitumiki, hakiko kwenye mpangilio, vitu vingi mno kwenye eneo dogo, ujazo na ujazo, miradi ambayo haijakamilika, kila kitu kilichopo kwenye hali ya kuvugu na/au kila kitu kichafu.

Tembea kuzunguka nyumba yako – nje na ndani. Fungua milango ya makabati, angalia kila mahali. Je una mlima wa makorokoro nyuma ya nyumba yako?  Kwa sababu tu huuoni mrundikano huu kila siku, haimaanishi hauko pale! Vitu vinavyokuzunguka vinakusemea ulivyo iwe vinaonekana au havionekani. Kuepuka kuelemewa wakati ukiwa unajaribu kuondoa mrundikano ni vyema kufanya zoezi hilo hatua kwa hatua. Hatua ya kwanza ni kuigawa kazi kwenye mafungu madogo dogo. Chagua kabati moja au shelfu kama hatua yako ya kuanzia. Jipongeze pale unapomaliza. Halafu nenda eneo linalofuata.Unaweza ukawa na muda maalum wa kushughulikia eneo moja kwa siku. Jambo la muhimu ni kuwa weka mikakati ya kazi ambayo itawezekana. Kama ukisubiri muda wa kutosha kufanya kazi yote pamoja, hautakaa upatikane – na hicho ni kisingizio cha kutokuanza kabisa.

Wakati ukianza kazi yoyote ya kuondoa mrundikano, panga kuchambua vitu hapo hapo ulipo. Kusanya (au weka kwenye maboksi) vitu vya kundi moja; kwa mfano, vitu vya kutupa, vitu vya kupeleka stoo, vitu vya kugawa, vitu vya kuuza, vya kuweka masijala na kadhalika. Ukishakuwa umechambua, sasa ni wakati wa kupeleka kila kimoja kunakohusika (vya kuuza unaweza kuhifadhi stoo kwa muda!). Sasa tafuta makao ya vile unavyohitaji. Huenda ni wakati wa kununua mifuko au vikontena kwa ajili ya vitu hivyo. Ndiyo njia pekee kwamba ni vyema kununua vikontena baada ya kujua ni nini unataka kuweka ndani. Baadhi ya watu wanafanya makosa kwa kununua kontena kabla ya kuchambua vitu na  hii inafanya visiwe na ukubwa sahihi au pia navyo kuwa mrundikano vilevile.

Je, unakuwa na wakati mgumu wa kuachilia vitu? Unahifadhi vitu kwa labda “lolote litatokea”? Je, unahifadhi zawadi ambazo hujawahi kutumia kwa sababu hutaki kuwavunja moyo waliokupa? Je, unajisikia vibaya usipozungukwa na vitu vingi? Je, unahifadhi nguo ambazo hazikutoshi kwa miaka 10 kwa wazo kwamba utazivaa tena baada ya kupungua kilo 7? Je, umehifadhi vitabu vya hadithi ambazo huzikusisimui tena? Utakapojibu maswali haya kwa uaminifu utaanza kufahamu ni wapi mrundikano ndani ya makazi yako unapotokea.

Kuachilia vitu ambavyo hatuvitumii tena, hatuvihitaji wala hatuvipendi ni hatua muhimu ya kuondoa mrundikano na kuanza kusafisha. Inaweza kuwa ngumu sana kwa baadhi. Kama unahitaji msaada kwenye huo mchakato, shika kifaa ambacho kwa namna yoyote ile hakikusaidii tena, kiambie asante kwa namna ambayo wakati fulani kilikusaidia kwenye maisha yako, na baada ya hapo kiachilie. Kumbuka kua kuachilia vya zamani kunaleta nafasi ya vipya. Inaonyesha imani ya yatarajiwayo.
Kuna wengi wanaoweza kufaidika na usivyohitaji. Je ni vyema kushikilia kitu ambacho hutakaa ukitumie lakini unakiweka kwa kuwa nyanya yako alikupa miaka 15 iliyopita ,au ni busara kumpa mtu ambaye atakitumia na kukithamini? Kwa kuachilia vitu kwenda kunakohitajika, unaondoa mrundikano na unajisikia vizuri kwenye jambo hilo.

Kipupwe ni msimu mzuri wa kuondoa mrundikano. Kwa jinsi unavyyoondoa mrundikano kwenye mazingira yako ndivyo unavyotengeneza nguvu chanya kukuzunguka. Badilisha maisha yako kwa kuondoa mrundikano!

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

living heaven on earth..

kuna baadhi ya binadamu wenzetu kweli wanaishi....hebu cheki nyumba hii mpya ya actor Mark Wahlberg......ina ukubwa wa square foot elfu 30. Mark haishi peke yake ana mke na watoto wanne, kwahivyo kwa mahesabu ya haraka haraka kila mwana Wahlberg anamiliki square foot elfu tano...hapo bado uwanja eneo la nje ya nyumba.....je mdau, wewe pia ungependa kuwa tajiri ??



Tuesday, October 7, 2014

hawa wadudu hawa...watu na tamaduni zao na mapenzi yao kwakweli..

yani nisivyopenda kumfuga huyu mdudu hata nje sembuse kumweka ndani ya nyumba..jamani..haya maisha kweli kipenda roho.. poop yake kama ya binadamu..si unajua misosi yake ni kama ya mtu... ni ile ile. bottom line ni kuwa anayetaka kumfuga na awe tayari kufagia poop.
ukute imechanganyika na minyoo sasa...waweza taapika yani.

halafu sasa, wakianza kubweka usiku kucha wakiungana na wa huko nje ya fensi hata hakulaliki...hapo ni kabla hawajaleta viroboto...lahaula! niwe tu na ulinzi wa aina nyingine lakini sio huyu mdudu.
 ndani ya dabodeka mdudu katulia na kitabu chake pembeni
 madai eti anajenga bond na mwenye nyumba
mdudu anatumia mto kiubwete kabisa

Monday, October 6, 2014

--nitavukaje--kutoka muajiriwa kwenye NGO hadi ufugaji

Bw. Peter ana masters ya kilimo toka SUA, nimechat naye mawili matatu kuhusu kuvuka kwake toka kuwa mwajiriwa hadi kujiajiri. Ananiambia alikuwa ameajiriwa kwenye NGO lakini alifika mahali akajiuliza kuwa kwa nini asitumie elimu yake kujiajiri. Na hii ilitokana zaidi na rusha roho ya wafadhali ku withdraw na hivyo kutokuwa na uhakika wa ajira. Ameamua kutumia elimu yake ya kilimo kwa kufuga kuku, kwale, bata mzinga na bikini kwenye sehemu ya shamba lake la heka 2 alilonunua mpiji magohe ambapo ameligawa viwanja vinne. Kimoja ameweka makazi yake, cha pili ameweka nyumba za wapangaji, cha tatu ameweka mifugo yake (ambapo anasema kutokana na uzio anafuga free range system) na cha nne ameweka ofisi yake. Nikamuuliza kwale ni nini, akaniambia ni ndege wadogo ambao mayai yake yanatafutwa na wazazi wengi kwa ajili ya kuwapa watoto wao kuongeza grey matter ya kwenye brain, mayai hayo pia ni dawa na huwa yanaongeza hata kiwango cha CD4 kwa waathirika wa Ukimwi. Anasema yai moja la kwale ni sh 600. Anajivunia kujiajiri kwenye kilimo kwani anasema amekuwa na uhakika na kipato kwa mfano bata mzinga mmoja anamuuza hadi sh 100,000 wakati bikini ni sh 250,000.

Umehamasika na stori hii? Kaa standy kwa itakayofuata kukuwezesha  kukuvukisha au pengine kukupa wazo la biashara...

--vitu vizuri-- i cant believe it's October already!

October ndio hiyo na upepeo wake mkali, nimemtembelea rafiki yangu makongo nikakuta kaotesha apples na embe fupi kwenye nyumba yake mpya. Miche hiyo ya ameichukua SUA na ananiambia kwa mi apple inachukua miaka minne hadi mitano ndio uone tunda lake. 

Ninadhani ni vyema zaidi huyu kuotesha miche hii badala ya mti ni mti tuu kwani anafaidi vyote, muonekano wa apple nyekundu ambao ni kama maua, kivuli na tunda lenyewe..na nadhani hata ukiwa unafaidi kivuli likakudondokea kichwani halikuumizi bali ni kudaka na kuosha na kula. Heee he..nisisahau kukujuza kuwa kwenye kula apple usimenye matunda yake kwani utakosa zile fibers.
lazima umeze mate...

Friday, September 26, 2014

---nitavukaje--Kutoka ualimu wa kuajiriwa hadi kujiajiri kwa kufungua media company

Leo katika mfululizo wa stori zangu za kukuwezesha kuvuka kutoka daraja ulilopo kwenda la juu nimeongea na entrepreneur  Fred Kirya ambaye alikuwa mwalimu hapo kabla lakini sasa ana media company. Nikamuuliza amevukaje? Akaniambia alivyokuwa mwalimu alijishughulisha pia na kuandaa program za vijana walioathirika na mambo mbalimbali, watukutu na hata wanajeshi waliotoka vitani halafu vichwa vikavyatuka kiana. Kutoka huko baadhi wa vijana walioweza kuachana na hali hizo wakawa wanaenda kuongea kwenye vituo mbalimbali vya redio. Hapo ndipo Fred alipojenga interest na media na akafungua media company yake ambayo anarekodi nyimbo za kwaya, singles za wasanii, program za watoto na vipindi vya vijana kwenye vituo vya redio. Fred anasema kwa kufanya kazi kwenye kampuni yake mwenyewe ana furaha ya kufanya anachokipenda, kuwa makini zaidi kwa mfano matumizi na utunzaji wa vifaa vya kazi na kubwa zaidi financially amekuwa na wise spending...... Kaa standby kusoma stori nyingine itakayofuata...

usisahau kuwekea mbolea bustani yako kwenye vuli hii

Mvua za vuli zimepamba moto kabla ya kuingia kwenye masika. Ukiweka mbolea kipindi hiki ikakutana na masika yanayokuja itasaidia mno kuboresha bustani yako.


Thursday, September 25, 2014

my article for newspaper: jiko safi ukiendelea kupika


Baadhi ya siku unaweza kushangaa kama kupika kunalipa kwa nguvu yote inayotumika. Kweli, unaweza kuweka mlo kabambe mezani, lakini jiko lako likaishia kuwa chafu mno kwa, mrundikano wa vyombo vichafu. Unaweza ukawaza kuwa inaenda kuchukua muda mwingi kusafisha kuliko kula!

Kanuni kuu ya jiko kuwa safi wakati ukiendelea kupika, ni kuanza na jiko safi. Kwa njia hii uchafu unaokuogopesha ni ule unaotengeneza wakati wa kupika tu. Kwa mazoea wengi wanajitahidi kuacha jiko safi kabla ya kwenda kitandani kila ifikapo usiku. Vyombo visafi vinawekwa kabatini, vile vichafu vinaoshwa, viporo vinawekwa kwenye vikontena na kuwekwa ndani ya jokofu, ndoo ya uchafu inamwagwa na kwa namna hiyo hakuna uchafu unaobaki jikoni.
.
Siri ya kufanya jiko liwe safi wakati unapoendelea kupika ni kuosha kadri vinavyochafuka. Nadhani hakuna njia nzuri zaidi ya kusisitiza hili. Kama wali unaendelea kuiva kwa dakika 20, una muda wa kusafisha. Kama kuna muda wa kusubiria chakula kiive, basi kuna muda wa kusafisha. Inashangaza jinsi tunavyodharau hizi dakika 10 (au zaidi!) ambazo zingeweza kurahisisha kazi yetu ya kusafisha hapo baadaye. Safisha kwanza, na utakuwa na muda wa kupumzika na kufurahia chakula chako baadaye.

Pimia vyakula ndani ya sinki, na rudisha kila kitu mahali pake baada ya kukitumia ili kaunta isishamiri vitu. Jitihidi kuwa unafanya maandalizi yanayotakiwa kabla ya kuwasha jiko. Kama unatumia kikombe au kijiko cha kupimia, hakikisha unakisuuza papo kwa hapo mara baada ya kukitumia. Futa vyakula kwenye kaunta kila vinapowagika, hii itasaidia kuzifanya kaunta zako zisiwe vululu vululu na kukusababishia kazi kubwa ya kusafisha baadaye. Hii pia inasaidia kuwa na eneo la kutosha kufanyia kazi. Nyanya ndio kiungo kinachochafua zaidi kaunta. Haiepukiki kupata matone ya nyanya ukutani na hata juu ya stovu. Kufuta punde kwa kitambaa cha unyevu kunasafisha mara moja, kwa ajili tone halijakomaa. Kwa chakula ama kiungo chochote kile kilichomwagika jikoni mwako safisha kabla hayijakaukia kwenye eneo husika. Itasaidia kuokoa muda na machukizo baadaye.

Hifadhi vifaa na vyakula unavotumia mara kwa mara maeneo ya karibu na safisha makabati yako ya jikoni na jokofu kwa msimu. Kwa namna hii hutakuwa na haja ya kuondoa vitu vyote kabatini kwa ajili ya kutafuta kitu kimoja unachohitaji.

Wakati unapopika tumia vyombo vichache. Kwa mfano, wakati unapotaka  kumenya viazi badala ya kumenyea maganda kwenye chombo, tumia mfuko au gazeti mbapo utabeba na kutupa moja kwa moja kwenye ndoo ya taka na hivyo kupungukiwa na chombo cha kuosha.

Kwa siku zile ambazo una muda mchache sana, pika vyakula rahisi ambavyo havihitaji kutumia sufuria na vikaangio vingi. Fanya mapishi ambayo chakula zaidi ya kimoja kinapikiwa kwenye sufuria moja, mifano ni mchemsho na mbogamboga.

Endapo utakuwa na mapishi kwa ajili ya wageni kadhaa nyumbani, basi gawa kazi yako. Fikiria ni nini unaweza kuandaa usiku mmoja kabla ya ugeni wako. Hii itasaidia kufanya maandalizi na kujikuta baada ya tukio ukiwa na vyombo vichache vya kusafisha. Kama utapika maharage kwa mfano, unaweza kuyasafisha na kuloweka usiku. Halafu unayaacha yamekaa kwenye jokofu, hadi kesho yake wakati wa kuyapika.

Kupunguza mrundikano kwenye kaunta inafanya wepesi wa kusafisha jiko lako. Unavyokuwa na vitu vingi kwenye kaunta ndivyo inavyokupasa kuvisogeza vyote kabla ya kusafisha na hii inakupa kazi kubwa. Baadhi ya watu kanuni ni kuwa, hakuna kifaa chochote kukaa juu ya kaunta vinginevyo kiwe ni kile tu kinachotumika kila siku kwa mfano kipashio cha chakula. Vingine vyote kama visagio na kadhalika vinahifadhiwa kabatini hadi wakati wa matumizi ndipo vinapotolewa. Usipende vijiko na visu vyako vikae juu vikibeba mafuta mafuta na vumbi. Viweke kwenye droo lililo karibu na stovu, ili unapovihitaji iwe rahisi kufungua na kuchuka. Havina haja ya kuwa juu ya kaunta na kula eneo lako la kazi.

Hizi ni baadhi ya njia za kukuwezesha kuweka jiko safi wakati ukiendelea kupika. Je, wewe msomaji wangu ni kwa namna gani unaweka jiko lako safi wakati ukiendelea kupika? Nitafurahi kusikia toka kwako!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

--vuka--kutoka architect muajiriwa hadi kujiajiri

Vijana wetu wengi mara wanapomaliza chuo wanaanza kusaka ajira. Wengi wanashindwa kuamini kuwa wanaweza kujiajiri kwa kufanya kile ambacho tayari wameshakuwa na ujuzi nacho. Leo nimechat na Caleb ambaye ni architect, nikamuuliza ni kwa vip ameweza kujiajiri. Alichoniambia ni kuwa mara baada ya kumaliza chuo aliajiriwa kwa miaka miwili. Wakati huo alikuwa anafanya vikao na wateja wake binafsi nyakati za jioni baada ya kazi za mwajiri wake. Mambo yalivyochanganya akajiajiri. Nikamuuliza maana ya mambo kuchanganya ni nini? Akasema alipata mradi wa mwaka mmoja kwenye kazi yake hiyo ambapo alijiaminisha kuwa akijiairi wakati wa mradi huo itakuwa ni wakati muafaka kwani hata kwa miaka miwili mbele asingepata mradi, mwingine mkubwa bado angeweza ku survive kwa zile kazi ndogondogo. Anasema ana uhuru zaidi wa binafsi na kipesa alivyo sasa kuliko alivyokuwa ameajiriwa. Umepata cha kujifunza hapo? Nawe waweza vuka ulipo kwenda upande wa pili ulio bora zaidi.

Tuesday, September 23, 2014

-vuka---kutoka daraja la uzururaji hadi fundi mechanic

nimekutana na hii nikaipenda na nikaamini ni daraja ambalo vijana wengi wangeweza kuvukia. unaweza ukadhani walivyolifumua fumua gari wapo Japan kumbe ni hapa hapa TZ...
hii ni chasis mpya baada ya gari kufumuliwa na ile ya zamani kuondolewa. Inaoshwa ipakwe rangi ndio kijumba cha gari kipachikwe.
chasis la zamani lililoondolewa kwa ajili gari lilikuwa limepata ajali na hivyo chasis kupinda.

kijumba kikisubiri chasis ikamilike ili kipachikwe.

----vuka----

friends,
as nina spirit ya biashara nimependa kuweka "nitavukaje" ambacho ni kijisegement kitakachokupa hadithi fupi sana ya mafanikio itakayokutia moyo na hata kuweza kukupa wazo la biashara. karibu...

Monday, September 22, 2014

vitu hivi vitaiongezea bedroom yako mashiko...

1. ki carpet...chochote kile ili mradi miguu isipate ubaridi na ugumu

2. mito ya kumwaga...

3. sehemu ya kukaa ambayo sio kitandani

4. vitu/picha unazopenda zinazokupa kumbukumbu nzuri

5. ugiza giza...bedroom ikiwa nyeupe saana mashiko yanapungua, weka pazia ambazo zinaua mwanga kiaina

Thursday, September 18, 2014

my article for newspaper: vifaa vya msingi jiko dogo la kisasa


Huenda pengine ndio unaanza maisha ya kujitegemea au ya ndoa, unahitaji kuwa na vifaa vya msingi jikoni vya kuanzia kwa miezi michache ya mwanzo—hata miaka michache. Au labda ni mzazi unayetaka kumsaidia huyo kijana wako, binti au rafiki namna ya kuanza maisha. Pia kama ni bibi harusi mtarajiwa makala hii inakuhusu. Nimefanya kazi kubwa ya kutafiti katika maduka ya vifaa vya jikoni na kukuandalia orodha ya vifaa vya msingi kabisa vinavyotakiwa kuwepo jikoni kwa ajili ya kukuwezesha kuandaa chakula katika maisha yako hayo mapya.

Nia hapa ni kuonyesha orodha ya vifaa vya kawaida kabisa vya msingi vya jiko dogo la kisasa.
Ni rahisi kuangukia kwenye ushawishi wa muonekano lakini kitu kimoja cha kujua kwa kweli ni kuwa hauna haja ya kuvunja benki ili kuwa na vifaa vya jikoni vya kiwango.  Orodha hii ya vifaa vya msingi jikoni inaweza kubadilika kutokana na hitaji la mhusika. Pia vyombo vya mezani kama vile sahani vijiko na glasi vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi na kwa sababu hiyo sijaviorodhesha hapa. Kwa hivyo vifaa vya msingi vya jiko dogo la kisasa ni kama vifuatavyo:

Visu

Kisu kikali cha mpishi ni moja kati ya vifaa muhimu zaidi jikoni, na kama utanunua kilicho sahihi kitatumika kwa miaka mingi. Nunua visu vya jikoni ambavyo havishiki kutu.

Ubao wa kukatia

Ubao sahihi wa kukatia utafanya visu vyako vidumu, na rahisi kusafishika. Kuna aina nyingi za mbao hizi kama vile plastiki, miti na hata glasi.

Kifungulia chupa na makopo (opener)

Nunua ambayo unaweza kufungulia chupa na makopo ya aina tofauti tofauti. Nzuri ni ile iliyo rahisi kwa matumizi.

Kisaga vyakula (Blender)

Kama kawaida nunua ambayo ni rahisi kutumia na yenye kazi nyingi tofauti ambapo utaweza kusaga vyakula vyako na kutengeneza juisi.

Vikaangio na masufuria

Iwe uko singo au ni wanandoa wapya kwa kuanzia unahitaji vikaangio japo viwili na sufuria nne hadi sita. Sokoni vikaangio na sufuria zipo zilizotengenezwa kwa material nyingi mno. Nunua ambazo hazing’ang’aniani na chakula (nonstick).
Stovu
Watengenezaji wengi wameunganisha stovu na tanuri ukinunua mbayo unaweza kutumia nishati zaidi ya moja itakuwa ni busara zaidi.

Jokofu
Kwa maeneo mengi ya nchi yetu walau inahitajika kuwa na jokofu kwa ajili ya kuhifadhia chakula kisiharibike. Kwa kuanzia si mbaya ukawa nalo dogo kwenye jiko lako hili la kuanzia maisha.

Kipasha chakula (Microwave)
Hiki kinafanya kazi kubwa ya kupashia na hata kupikia baadhi vya vyakula. Habari njema ni kuwa zipo za bei rahisi kabisa. Ni rahisi kutumia na wengi wanapendelea kuziweka juu ya kaunta ya jiko. Huna haja tena ya kupashia chakula kwenye sufuria.

Kikausha mikate (Toaster)

Hiki nacho kwa wengi wanaopendelea kula mikate iliyokaushwa huwa wanakiweka juu ya kauta.
Mabakuli/Vikontena
Wanasema mapishi ni sanaa, sio? Kuwa na mabakuli na vikontena ndani ya jiko lako la kuanzia maisha vitakusaidia katika maandalizi ya mapishi na hata vikontena vitakusaidia kupashia na pia kuhifadhia vyakula kwenye jokofu.

Kindoo cha uchafu
Unapoandaa chakula na kuosha vyombo lazima utahitaji hiki kindoo kwa ajili ya kuwekea uchafu. Ni muhimu kiwe kile cha mfuniko wa kujifunga chenyewe.
Jiko lenye vifaa vya msingi vinavyopaswa kuwepo jikoni ni rafiki kwa mpishi. Unapokuwa na vifaa sahihi na unajua jinsi ya kuvitumia, unaweza kuelekeza akili yako kwenye chakula unachoandaa. Kama nilivyosema awali vifaa hivi vinaweza kuongezeka kutegemea na mhusika na mazingira unaweza kuwa na vifaa hivi vya msingi jikoni kwa kuanzia na baadaye ukaongeza kidogo kidogo kwa kadri ya mahitaji yako. Mpishi mzuri anatumia vifaa tofauti tofauti na mwishoni anapata vile hasa anavyohitaji.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Tuesday, September 16, 2014

pambo hili lina faida lukuki...

Pambo hili na jamii yake linafaa kuwekwa ukutani na mlangoni kwa ajili kwa umbo lake huwa linakuwa flati upande mmoja na kitumbo upande wa pili. Ndani kuna nafasi kiasi kwamba likiwa kama pambo; wakati huohuo unaweza kuhifadhi vitu vidogo dogo kwama vile dawa zilizo kwenye pakiti, uzi na kadhalika. Laa kama unataka kusisitiza pambo lako basi weka maua ya artificial badala ya vikorokoro kama huyu hapa kwenye picha alivyoweka. Lilivyotengenezwa material yake sio nzito. Unaweza kulitumia miaka nenda rudi. Linapatikana kwenye maduka yanayouzwa mapambo ya ndani. Perfecto!



Thursday, September 11, 2014

my article for newspaper: Jinsi ya kupata kizulia sahihi cha jikoni


Wengi tutakubaliana kuwa zulia la ukuta kwa ukuta sio sahihi kuwekwa jikoni, ila kizulia cha kutupia kina faida kadha wa kadha jikoni. Kizulia hiki kinasaidia kuepusha miguu na sakafu ya baridi na kinaongeza rangi, hata kiwe kidogo namna gani. Yote kwa yote sababu kuu yaweza kuwa ni kwa ajili ya burudani ya miguu na kuiepusha na baridi. Kama unaweza kusikia baridi ya kukera kwenye nyumba yako mwenyewe basi ni ukakasi. Kuweka kizulia jikoni kunakamilisha sakafu na mvuto wa jiko. Vinginevyo uwe unapenda sana rangi kiasi kwamba umepaka kabati zako za jikoni rangi ya kung’aa kama vile pinki, kijani ama nyekundu.

Kizulia cha kutupia kinaweza kuleta rangi bila kukufanya utumie hela nyingi, kama hii ndio sababu ya kuamua kuweka kizulia jikoni hapa basi ni dondoo chache za kukusaidia kupata kilicho sahihi.
Kuchagua kizulia sahihi kwa ajili ya jiko, ni vyema kufahamu nia yako kuu ya kuamua kukinunua. Inaweza kuwa ni kwa ajili ya kuepusha miguu na ubaridi wa sakafu au kuongeza staili, rangi na mvuto kwenye sakafu ya jiko. Pia fikiria ukubwa na umbo la kizulia ambacho kitafaa zaidi kwa nafasi iliyopo. Usisahau kuzingatia vifaa vilivyotumika kutengenezea kizulia utakacho na kufahamu ni utunzaji kiasi gani utakaohitajika. Chagua kizulia ambacho hakitelezi (hakikimbii sakafu) kwa ajili ya sababu za kiusalama.

Hasa kama sakafu ya jiko lako ni laini, yakung’aa na inayoteleza, ni muhimu sana kuchagua kizulia chenye mnato/mpira kwa chini kinaposhikana na sakafu. Mpira huo utasaidia kizulia kikae mahali pamoja kisihame hame kinapokanyagwa, ambapo kinaweza kusababisha mtu kuanguka.

Chagua mahali sahihi pa kuweka kizulia chako cha jikoni. Ni wapi unapotumia muda mwingi unapokuwa  jikoni? Pengine ni mbele ya sinki, kwa hiyo ni kuwa utachagua kuweka kizulia eneo hili. Au labda una eneo kubwa la kutembea kwenye sakafu ya jikoni. Basi angalia mahali hapo kati unapoweza kutupia kizulia chako ili kilete burudani ya miguu maeneo kadhaa. Vile vizulia vyembamba virefu vinafaa zaidi wa jiko lenye sakafu ndogo.

Kama lengo lako kuu la kuhitaji kizulia jikoni ni kuondoa ubaridi na kuleta nesa nesa ya miguu, basi unene wa kizulia unahusu. Utahitaji mbonyeo kati ya sakafu ngumu na miguu yako kwa burudani. Ulaini wa kizulia pia unaepusha miguu yako na baridi la sakafu ya marumaru au mbao au hata saruji. Hakuna anayetaka kuwa kwenye maumivu wakati akiosha vyombo!

Chagua manyonya sahihi, iwe ni sufi au pamba. Kizulia ambacho kinasafishika kirahisi kwa sabuni na maji. Urahisi wa kusafisha ni lazima ukumbukwe kwenye kuchagua kizulia cha jikoni, hasa kwa vile vinavyowekwa chini ya sinki au mbele ya stovu au jokofu. Vizulia vya sufi vinaweza kuwa chaguo sahihi kimuonekano ila kwa kawaida vinashika madoa kirahisi na vinahitaji usafishaji wa kitaalam kwahivyo ni vyema kuweka vizulia vya aina hii kwenye vyumba vingine nyumbani ila sio jikoni au chumba cha kulia chakula, anasema muuzaji Aisha Mbegu. Vizulia vya kufumwa kwa mimea ya asili kama vile katani au majani ya baharini vinaweza kuwa chaguo sahihi kwa ajili ya kuweka chini ya meza ya kulia chakula, kwa ajili kwa kawaida ni rahsisi kuvifuta na kusafisha hata kwa kufagia.

Haijalishi utaamua kuchagua kizulia cha jkoni kilichotengenezwa kwa vifaa vya aina gani, kuchukua kipimo cha eneo unalotaka kuweka kizulia ndani ya jiko lako itakusaidia kupata kilicho sahihi. Wakati wa kuamua aina za vizulia, jitahidi kutafakari rangi, na ni kwa namna gani ukubwa  na muundo utakavyogusa muonekano mzima wa jiko lako.

Wacha kizulia chako kitengeneze stori. Chagua ambacho kitaongeza uzuri kwenye jiko lako. Sakafu za jiko huwa zinapooza, kizulia kinaweza kuongeza uchangamfu na ladha binafsi kwa kuunganisha rangi za jiko pamoja. Kama nilivyosema kabla, chagua kizulia kitakachoongeza rangi, ambapo ni rahisi kubadilisha kizulia ili kuondoa muonekano wa jiko utakapochoka zile rangi zake za kudumu ulizozizoea.

Hongera kwa kufanya eneo kla sakafu ya jiko lako kuwa na mvuto, nesanesa na budurani! Utakapoweka kizulia cha jikoni hutatamani kukiacha.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Wednesday, September 10, 2014

kwanini ni muhimu kufua carpet kwa sabauni na maji ya pressure

ninapata amazing deal ya kufua mazulia ya manyoya kwa ajili wateja wengi wanayaleta kutokana na kuwa yananuka vibaya. Carpet linapokuwa na harufu mbaya kwa kuwa labda limemwagikiwa vimiminika pengine ni wakati wa sherehe au maisha ya kawaida ya kila siku na pilika za watoto, kusafisha kwa vacuum cleaner au form cleaner haitawezekana kuondoa harufu mbaya ya zulia la manyoya likiloa linavyonuka.

Kinachotakiwa kufanyika ni kuniletea carpet lako kwa kuwa tuna pressure washer ya kuweza kulipiga maji, kuweka detergent na kulisugua hadi mabaki yote ya vyakula (eg ubwabwa wa sikukuu) na vimiminika vyote vitoke. Baada ya hapo tunaanika kwenye jua kali kwa siku mbili na zulia lako linakuwa tayari kama jipya. Kuamua kufua zulia kwa maji inaweza kuchangiwa pia na uchafu mwingine wowote kama vile vumbi na tope.

Karibu sana ian car wash tung'arishe tena carpets zako. Tuwasiliane 0755200023
carpets zilizofuliwa, kukauka na kukunjwa

mteja yuko tayari kupelekewa carpets zake kwenye gari

hizi nazo ni za mteja mwingine zinamsubiri

 hizi hazijakaula hivyo tumetandaza ndani tuanike tena kesho


Monday, September 8, 2014

---vitu vizuri---getting better with age

2014, uso unaonekana tight

2014, hapa ni kama vile my face is dropping! heeee he, in my mid 30's

2002, 12 years before nilikuwa hivi; ni nini siri ya kutoruhusu makunyanzi kuja fastaaa. enjoy your monday gators....

Thursday, September 4, 2014

my article for newspaper: kuepusha wadudu ndani ya nyumba

Wakati baadhi ya watu wanaogopa wadudu, wengine wanaweza kuwa wanavutiwa nao. Lakini kitu kimoja ambacho wengi tutakubaliana ni kuwa wadudu makazi yao sio ndani ya nyumba. Si tu kuwa wanaleta mazingira hatarishi kiafaya, bali pia, ni rahisi tu ya kuwa wanaudhi, kuanzia mbu wanaokupigia mziki masikioni mwako, kukuuma na kukusababishia maradhi hadi kwa nyigu anayeweza kukusababishia kidonda.

Hata yule mende wa kawaida anaweza akasababisha mzio hasa kwa watoto, anasema dokta Emil.
Kuepusha wadudu ndani ya nyumba inaweza kuwa ni vita vilivyoshindikana. Bahati nzuri ni kuwa, kwa kufahamu ni nini kinachovutia wadudu ndani ya nyumba yako, unaweza kuanza kufanya mabadiliko ambayo yatawakimbiza kimya kimya.

Kama ilivyo kwa binadamu, wadudu nao wanahitaji chakula, maji na makazi ili kuishi. Kwa kukata usambazaji wa chakula chao na kuvuruga maeneo yao ya kujifisha, unaweza kupunguza tatizo la kuwa na wadudu ndani ya nyumba yako. Kata chanzo chao cha chakula kwa kuhakikisha kuwa vyakula vyote vinawekwa kwenye kontena zilizofungwa vizuri. Mabaki ya vyakula ndani ya nyumba yatupwe eneo moja tu ambalo ni ndoo ya uchafu  yenye mfuniko wa kujifunga wenyewe iliyopo jikoni. Ndoo hii imwagwe na kusafishwa kila siku baada ya kuosha vyombo vya chakula cha usiku. Futa michuzi na mabaki yoyote yanayoweza kuwepo maeneo ya wazi ndani ya nyumba. Osha vyombo punde mara baada ya kutumika. Pipa linalomwagwa uchafu nje nalo liwe na mfuniko.

Usisahau vyakula vya wanyama waliopo nyumbani kwako. Kwa mfano unafuga mbwa na una vyakula vyake vya unga umehifadhi stoo, unga huu unaweza kuvuta mende na sisimizi. Unaweza kuweka dawa za kuzuia wadudu kwenye stoo yako ya chakula cha wanyama unaofuga.
Vifaa vyote vya kuhifadhia mabaki ya vyakula ndani na nje ya nyumba viwe vinasafishwa kwa dawa za kuua wadudu mara kwa mara.

Kama vile mlango uliolokiwa unavyoweza kuwaweka wavamizi nje, mlango uliozibwa sahihi unaweza kuwazuia wadudu wasiingie ndani. Kuepusha wadudu wanaotambaa kuingia ndani kwa kupitia sehemu ya wazi mlangoni, weka kizuizi cha mpira au brashi chini ya mlango. Vizuizi hivi vinapatikana kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi, anasema mseremala Simon.

Kumbuka kuwa mbinu zote hizi za kuziba chini ya mlango hazitafanikiwa kama mlango wenyewe utaachwa wazi. Kama una watoto ambao wanasahau kufunga mlango, fikiria kusimika vifunga mlango.
Wenye nyumba wengi wanategemea hewa safi ya nje iingie ndani kupitia milangoni na madirishani. Hii inaweza kuwa majaribu hasa wakati wa kiangazi. Bahati mbaya ni kuwa kiangazi ni wakati mbaya kwa vile mbu na wadudu wengine wengi wanavamia ndani ya nyumba. Kufurahia raha ya hewa safi bila kupata bughudha ya wadudu weka wavu wa kuzuia wadudu kama mbu kwenye madirisha na milango.

Eneo la nje ya nyumba linaweza kuwa linasababisha wingi wa wadudu ndani ya nyumba yako. Endapo mioto ya asili ni mingi na iko karibu sana na ukuta wa nyumba basi tegemea kuwa na mazalia makubwa ya wadudu na hivyo uwezekano wa wengi kujaribu kukimbilia ndani. Hii pia itakufanya hata wewe mwenye nyumba kushindwa kufurahia kukaa kuburudika nje ya nyumba yako, kwa hivyo njia nzuri ya kuepusha wadudu ndani ya nyumba ni kuhakikisha wanaondoka pia kwenye maeneo ya nje ya nyumba.

Majani yaliyorundikwa, matofali yaliyopangwa kwenye yadi yako na hayatumiki tena na mashimo ya maji taka yanafanya makazi ya wadudu mbalimbali. Maeneo haya ni sehemu za kujificha kwa wadudu kama mende nyoka na wengine wengi na hata panya. Mashimo ya maji taka yawe na mifuniko iliyoziba vizuri na mrundikano mwingine wowote uondolewe na utashangazwa ni kwa jinsi gani wadudu watakimbia na mazingira yako yatakavyovutia.

Baadhi ya wenye nyumba wanapendelea kutumia dawa za kupulizia kwa ajili ya kuua wadudu kama mbu na mende. Haijalishi ni njia ipi unatumia ili kuepusha wadudu kufanya makao ndani ya nyumba yako; njia kuu ya kuwafanya wakimbie ni kukata “mirija” wa kile kinachowavutia. Hii inamaanisha ni pamoja na kuondoa mrundikano, vyakula na vyanzo vya maji. Bila kuwa na rasilimali hizi, wadudu watakimbia kwako kuelekea nyumba ya pili na kukuacha ukiwa na amani.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com