Thursday, February 12, 2015

Akiri kama angefahamu vituko vya mumewe asingekubali kuolewa naye

Mkazi wa mjini Namanyere mkoa wa Rukwa, Gilbert
Paul (37) aliyejiandalia maziko yake miaka 14
iliyopita, bado yu hai. Kwa sasa mtu huyo ameanza maandalizi ya
kuchimba na kujenga kaburi la gharama, ikiwa ni pamoja na kununua jeneza.
Paul, baba ya mtoto mmoja na mchoraji maarufu,
anasema hivyo kwa kuwa ana amani maisha ya duniani yana ukomo wake na ni ya kupita tu.
Aliyasema hayo juzi, akithibitisha kujichongea
msalaba mkubwa na kuutundika kwenye paa la
kibanda chake anamofanyia kazi zake.

Msalaba huo mweupe mkubwa, umeandikwa tarehe
aliyozaliwa ya Desemba 24, 1977, lakini katika
tarehe ya kufa, ameweka alama ya kiulizo. Msalaba
huo unaonekana waziwazi, kiasi cha wageni
wanaopita eneo hilo, kudhani ni nyumba ya ibada.

Paul alisisitiza kuwa msalaba huo uliofikisha miaka 14 sasa, ndio utakaosimikwa katika kaburi lake, ambalo anatarajia kulichimba na kulijengea, akikadiria litamgharimu Sh milioni moja, sawa na gharama ya jeneza alilotarajia kulinunua.

“Nilipotafuta mafundi wanitengenezee msalaba huu, wote waligoma wakidai ni uchuro na hawajawahi
kusikia wala kuona mtu akijifanyia maandalizi yake
ya maziko akiwa bado anaishi . “Mama alilia sana
walipomtaarifu, akidai katika ukoo wa baba yangu na wa kwake hakuna aliyewahi kufanya hivyo …Baba
alifariki nikiwa na miaka saba, mwanzoni watu
walidhani nina tatizo la akili na wengine waliamini nimeathirika kwa Ukimwi hivyo nimekata tamaa ya
kuishi, lakini sivyo…“ anasema.

Alieleza kuwa katika maisha yake yote, hakuwahi
kuwa na rafiki wa kike mjini humo kutokana na
kujitengenezea msalaba huo, unaomfanya
wamuogope sana, hadi kuona kuna ulazima wa yeye kwenda kijiji cha mbali na hapo .

“Nilichumbia na kuoa chapuchapu nikihofia mke
wangu mtarajiwa akibaini nimejitengenezea msalaba hatanikubali,“ alieleza.
Mke wa Paul, Paskaria Salvatory (25) akizungumzia
tukio hilo, anasema kama angefahamu, kamwe
asingekubali kuolewa naye.

“Si kawaida mtu kujitayarishia maziko yake mwenyewe akiwa hai. Nilibaini mwezi mmoja baada ya
kuolewa, kwa kweli nilishituka sana, pia wanawake
wenzangu walikuwa wakinibeza na kuniita kwa
majina ya kuudhi, lakini sasa nimezoea na nimezaa 
naye mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili.

Mume wangu ana akili timamu, ni mwenye huruma
na anayejali familia“, alibainisha.

No comments:

Post a Comment