Wapenzi, nimekutana na makala hii ambapo inajibu dukuduku la wengi la kuwa ni biashara gani wafanye. Naamini ukiisoma japo ni ndefu na nimejitahiji kuipunguza kwa kukuchujia kile cream hutatoka patupu.
Imeandikwa na Makirita Amani
Biashara moja inaweza kuwa nzuri kwa watu wengine ila ikawa mbaya
sana kwako. Unaweza kuona watu wanapata faida kwenye biashara fulani ila
ukaingia wewe na ukapata hasara kubwa sana.
Hivyo kujua ni biashara gani ufanye ni kitu ambacho unatakiwa
kukifikiria kwa kina na sio kuiga au kuamua tu kufanya chochote.
Katika makala hii ya leo tutaangalia vitu viwili, jinsi ya kujua
biashara ambayo itakulipa na jinsi ya kupata wazo bora la biashara.
1. Ni biashara gani inaweza kukulipa?
Jibu la swali hili haliwezi kuwa sawa kwa watu wote, linategemea
na mtu na ili kuweza kupata jibu la swali lako wewe mwenyewe unatakiwa
kujiuliza na kujipa majibu sahihi maswali haya matatu;
a) Ni kitu
gani unapendelea kufanya?
Katika maisha yako kuna vitu fulani ambavyo unavipenda sana au
unapendelea kufanya. Inawezekana unapenda mitindo, inawezekana unapenda
michezo, inawezekana unapenda magari au kusafiri na kadhalika. Kwa kuangalia
mambo haya unayopenda sana kufanya unaweza kufikiria ni jinsi gani unaweza
kuyageuza kuwa biashara. Kwa mfano kama unapenda sana kusafiri unaweza
kuanzisha biashara ya usafirishaji. Kama unapenda sana mifugo au wanyama
unaweza kuanzisha biashara ya ufugaji. Ni vizuri sana kufanya biashara unayoipenda
kwa sababu utakuwa na shauku ya kujifunza zaidi na hutokata tamaa mapema hasa
mambo yanapokuwa magumu.
b) Una
uzoefu au taaluma gani?
Swali hili ni muhimu na litakuwezesha kujua kitu ambacho unaweza
kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kumbuka ili kufikia mafanikio kwenye
jambo lolote ni lazima uweze kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kama kuna
kitu ambacho umekisomea na una taaluma nacho ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi
sana ambayo unayajua kuhusu kitu hicho. Na kama una uzoefu wa kitu au jambo
fulani ni rahisi kwako kufikia mafanikio kwenye kulifanya kuliko anayeanzia
mwanzo kabisa. Hivyo fikiria ni vitu gani umevipata kupitia taaluma yako na
angalia ni jinsi gani unaweza kuvitumia kwenye ujasiriamali na biashara. Pia
jiulize ni uzoefu gani ambao tayari unao na jinsi gani unaweza kuutumia kwenye
biashara unayoweza kuanzisha. Kwa mfano kama umeajiriwa kwenye kampuni ya
wanasheria hii ina maana kwamba tayari wewe una taaluma ya sheria na pia una
uzoefu wa kuendesha kesi, kutafuta wateja na hata uendeshaji wa kampuni.
Unaweza kutumia taaluma yako hii na uzoefu ulioupata kwenye kampuni uliyofanyia
kazi na kwenda kuanzisha kampuni yako mwenyewe ambayo itakupatia mafanikio
makubwa sana kama ukiweza kuisimamia na kuiendesha vizuri.
c) Ni kitu
gani ambacho kina uhitaji mkubwa.
Swali la tatu na muhimu kujiuliza ni kitu gani ambacho kina
uhitaji mkubwa kwa eneo ambalo unafikiri kufanyia biashara. Angali ni kitu gani
ambacho tayari kina soko au unaweza kukitengenezea uhitaji ili uweze kupata
wateja pale utakapoanzisha biashara yako. Pia angalia ni jinsi gani unaweza
kulifikia soko hilo kulingana na bidhaa au huduma ambayo unatarajia kuitoa.
Kama ukiweza kujiuliza na kujipa majibu sahihi kwenye maswali hayo
matatu utapata aina nzuri ya biashara ambayo utaifanya kwa moyo na utaweza
kufikia mafanikio makubwa. Njia nzuri ya kufanya hivi ni wewe kuchukua kalamu
na karatasi kisha kuorodhesha vitu vyote vinavyohusiana na maswali hayo matatu
na kisha kuoanisha na kuona ni kitu gani ambacho kinaweza kuingia kwenye sehemu
zaidi ya moja.
Usichukue ushauri wa biashara kwa sababu tu kwamba watu wengi
wanafanya au inaonekana kulipa. Ni muhimu biashara utakayokwenda kufanya iwe
inatoka ndani yako kweli ndio utaweza kufikia mafanikio makubwa kupitia
biashara hiyo.
2. Njia ya kupata wazo bora la biashara.
Mara nyingi watu wamekuwa wakiniuliza ni biashara gani inalipa
ambayo wanaweza kufanya na wakapata mafanikio. Jibu langu ni kwamba kila
biashara inalipa, ndio maana kuna biashara mbalimbali zinazofanyika kila kona
na watu wanapata faida. Ili biashara iweze kufanikiwa na upate faida ni lazima
upende biashara unayofanya na uwe na ubunifu wa kutosha.
Hata baada ya kujua biashara itakayokulipa ni ile unayopenda
kufanya bado kuna changamoto ya kuja na wazo zuri la biashara. Nina hakika
umewahi kuwa na fedha kidogo na kutamani kuiweka kwenye biashara ila ukashindwa
kujua ufanye biashara gani. Changamoto kubwa za biashara zinatokana na kosa
moja kubwa ambalo wajasiriamali na wafanyabiashara wengi wanalifanya. Tatizo
hili ni kuiga vitu vinavyofanywa na wengine bila ya kujua vinafanyaje kazi
kwao.
Hapa nitazungumzia jinsi ya kuja na wazo la biashara ambapo watu
watakukimbilia kukupa fedha. Kwa kutumia njia hizi ninazoshauri utaweza
kutengeneza biashara yenye thamani na itakayodumu na hutokuwa na haja ya kuiga
kila kitu kutoka kwa wengine.
Jua
tatizo linalosumbua watu na tafuta njia ya kulitatua.
Biashara zote kubwa duniani zimejengwa kwenye msingi mmoja tu,
kutatua matatizo yanayosumbua watu. Watu walikuwa na tatizo la kushindwa
kuwasiliana na wenzao wa mbali ndipo biashara za mawasiliano na usafiri
zikaanzishwa na kukua kwa kasi.
Kama umewahi kuumwa au kuwa na mgonjwa utakuwa unaelewa vizuri
kwamba hata kama mtu ana shida ya fedha kiasi gani linapokuja tatizo la afya
atatafuta kila njia ili aweze kulitatua. Hivyo hata watu wawe na shida ya fedha
kiasi gani wako tayari kulipia kitu ambacho kitawaondolea tatizo
linalowasumbua. Hapa ndipo penye wazo kubwa la biashara.
Kwa kuwa inabidi ufanye biashara ambayo unaipenda na kwa kuwa
unahitaji ubunifu ili biashara yako iweze kukua fikiria wazo lako la biashara
kutokana na matatizo ya watu. Angalia vitu ambavyo unapenda kufanya kutokana na
vipaji vyako. Pia angalia ujuzi ambao unao na elimu uliyopata kwenye kada
fulani. Kisha angalia ni matatizo gani watu wanayapata na unaweza kuyatatua.
Jinsi ambavyo tatizo ni kubwa ndivyo thamani ya biashara inavyozidi kuwa kubwa.
Kwa njia yoyote ile kuna bidhaa au huduma unaweza kuitoa na ikatatua matatizo
ya watu.
Wakati
mwingine watu hawajui tatizo mpaka waone suluhisho.
Sio kila mara watu watakuwa wanajua matatizo yao, kuna wakati
mwingine watu wanakuwa hawajui kama wana tatizo mpaka waone kuna njia rahisi ya
kufanya mambo, hii inaitwa ujinga wa soko.
Hivyo kama wewe unaona kuna njia bora ya kuboresha maisha
ya watu tengeneza biashara yako na washawishi watu. Kama wakitumia na kuona ina
faida kwao watakuwa wateja wako na watawaambia wengine pia. Hivi ndivyo
mitandao ya kijamii kama facebook na twitter ilivyoteka soko. Mwanzo hakuna mtu
alidhani kuna uhitaji mkubwa wa mitandao ya aina hii, kabla ya kuanza kwa
facebook sikuwahi kuona watu wakilalamika kwamba wanahitaji facebook. Ila baada
ya mitandao hii kuwepo na watu wakaanza kuitumia imewawia vigumu kuacha
kuitumia. Kila siku tunashuhudia ni jinsi idadi ya watumiaji wa mitandao hii
inavyoongezeka.
No comments:
Post a Comment