AKIWA
katika maadhimisho ya kuanza mwaka wa pili wa utume wake katika kuongoza Kanisa
Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis, ametoa kauli kuashiria kuwa huenda
asidumu katika wadhifa huo kwa muda mrefu
ujao.
Alisema
hayo juzi katika mahojiano ya ana kwa ana na kituo kimoja cha televisheni cha
Mexico, Televisa News, baada ya kutangaza kuwa Desemba mwaka huu, Kanisa
Katoliki litaadhimisha Mwaka Mtakatifu.
Mwaka
huo Mtakatifu utaanzia Desemba 8, mwaka huu na kuisha Novemba 20, mwakani.
Inaelezwa kuwa kuzinduliwa kwa Mwaka Mtakatifu au Jubilee, kunaendana na
maadhimisho ya 50 ya kufungwa kwa Baraza la Pili la Vatican, ambalo hukusanya
maaskofu ambao huzungumzia mambo ya baadae ya kanisa.
Mwaka
huo Mtakatifu utakuwa wa 29 tangu utaratibu huo ulivyoanza mwaka 1300. Kwa
kawaida Mwaka Mtakatifu huadhimishwa kila baada ya miaka 25.
Ukomo
wake Katika tamko hilo, Baba Mtakatifu Francis mwenye umri wa miaka 78, ameweka
wazi kuwa hataadhimisha miaka mingine mitakatifu katika siku zijazo. “Nina
hisia kwamba utume wangu utakuwa wa muda mfupi, kama miaka minne au mitano;
sijui inaweza hata kuwa miwili au mitatu lakini miaka miwili imeshapita,”
alitabiri katika mahojiano hayo.
Hata
hivyo, hakutaka kuweka wazi kama atafuata nyayo za mtangulizi wake, Baba
Mtakatifu mstaafu Benedict XVI, ambaye ameweka historia ya kuwa Baba Mtakatifu
wa kwanza kustaafu katika miaka 600 iliyopita, baada ya kuchukua hatua hiyo
mwaka 2013.
Alipoulizwa
swali mahususi kama atafuata nyazo za Baba Mtakatifu mstaafu, Benedict XVI,
alijibu; “Huenda Benedict XVI akabakia kuwa Baba Mtakatifu mstaafu pekee kwa
miaka mingi ijayo, na huenda akapata mwenzake,” na kuongeza kuwa Baba Mtakatifu
mstaafu “ameonesha njia.”
Hii si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francis
kuzungumzia ukomo wake, kwa kuwa amewahi kusema kustaafu kwa Baba Mtakatifu
Benedict XVI mwaka 2013, kusichukuliwe kuwa tukio la pekee.
Pia,
alisema hakuchukia kuteuliwa kuwa Baba Mtakatifu, lakini aliweka wazi kwamba
katika wadhifa huo, amejikuta akipoteza uhuru wake. “Natamani tena kuwa na
uwezo wa kutoka nje siku moja bila mtu yeyote kunifuatilia na kunitambua
nikajinunulie mahitaji yangu,” alisema na kutabasamu.
Lengo
la mahojiano hayo na kituo hicho cha Televisa News, lilikuwa kujadili maisha
yake ikiwemo mawasiliano yake na baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakimwandikia
barua kumshirikisha katika huzuni zao na kupata ushauri wake.
Umasikini,
wahamiaji Baba Mtakatifu pia alizungumzia hali ya uhamiaji duniani na kuibuka
kwa wimbi la wakimbizi wanaokimbia umasikini, njaa na vita katika nchi zao za
kuzaliwa.
Katika
mahojiano hayo yaliyochapishwa katika kurasa 17, Baba Mtakatifu Francis alisema
kwa kuwa yeye ni Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka Bara la Amerika ya Kusini,
analazimika kuzungumzia wahamiaji na watu masikini kwa sababu babu zake
walihama kutoka Italia kwenda Argentina kutafuta kazi.
Chanzo Habari Leo
No comments:
Post a Comment