Wednesday, March 25, 2015

BAADHI YA NYUMBA ZINAZOZUIA MAJI KUPITA NA KUSABABISHA MAFURIKO HIVI KARIBUNI HUKO BUGURUNI MNYAMANI KUBOMOLEWA......UZURI NI KWAMBA WOTE MTAKAOBOMOLEWA NYUMBA ZENU MTALIPWA FIDIA

RAIS Jakaya Kikwete ameamuru kubomolewa baadhi ya nyumba zilizojengwa juu ya karavati lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba za wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani, Ilala Dar es Salaam.

Akihutubia wananchi wa eneo hilo jana, Rais Kikwete alisema nyumba hizo zitabomolewa pamoja na karavati hilo kupisha maji kupita na kulijenga upya.

“Kwa sasa tunaendelea kuvuta maji yaliyojaa kwenye makazi ya watu kwa kutumia pampu lakini baadaye itabidi tuvunje nyumba zilizoko juu ya karavati kupisha ujenzi wa karavati jipya,” alisema.

Rais Kikwete ambaye alitembelea maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo jana, alisema wananchi wote watakaobomolewa nyumba zao watalipwa fidia huku akitoa rai kwao kuacha tabia ya kujenga holela bila kuzingatia matumizi ya eneo husika.

Katika hatua hiyo, alisema zipo taarifa za kuwapo uhitaji wa chakula kwa waathirika na tayari uongozi wa wilaya na kamati ya maafa zimeanza kushughulikia tatizo hilo.

Wananchi walioathirika na mafuriko hayo waliiomba serikali kuharakisha hatua ya kutoa maji yaliyojaa kwenye makazi yao na kutoa misaada inayohitajika.


Mvua inayoendelea kunyesha Dar es Salaam imesababisha madhara makubwa vikiwamo vifo vya watu saba na nyumba zaidi ya 200 kuzingirwa na maji katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment