JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanza
kumchunguza Josephine Mushumbusi, ambaye ni mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, anayetuhumiwa kula njama
za kumuangamiza.
Kamishna Kova alisema kuanzishwa kwa uchunguzi huo ni
matokeo ya maelezo ya Khalidi Kangezi, ambaye alikuwa mlinzi wa Dk. Slaa
aliyefikishwa polisi baada ya kuteswa na kutekwa kwa tuhuma za kushiriki
mipango ya kumuua bosi wake huyo.
Alisema, Kangezi baada ya kufikishwa katika Kituo cha
Polisi cha Oysterbay, katika maelezo yake aliwataja Mushumbuzi na mchungaji
mmoja ambaye jina lake halijawekwa hadharani kuwa ndio waliokuwa na mpango huo,
lakini yeye aliuzuia.
Mbali na wawili hao, Kamanda Kova alisema uchunguzi huo
pia utawagusa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula,
ambaye ametajwa na baadhi ya makada wa chama hicho kuwa mmoja wa wahusika wa
mpango wa mauaji ya Dk. Slaa.
Wakati Jeshi la Polisi likitangaza kuanzishwa uchunguzi
huo, wanachama
watatu wa Chadema wanaotuhumiwa kumteka na kumtesa
Kangezi, jana walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kutenda
makosa mawili.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Wakili wa
Serikali, Janeth Kitali, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, majira
ya saa nane mchana.
Wakili Kitali alidai mahakamani hapo kuwa kosa la kwanza
la washtakiwa, Diwani Boniface Jacob (32), Mlinzi Hemedi Sabula (48) na Ofisa
Utawala wa chama hicho, Benson Mramba, ni kumjeruhi Kangezi, kosa ambalo
walilitenda Machi 7, mwaka huu.
Katika shtaka hilo washtakiwa wanadaiwa kwamba tarehe
hiyo wakiwa Makao Makuu ya Ofisi za Chadema zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni
Dar es Salaam, walimjeruhi Kangezi kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili
wake na kumsababishia maumivu makali.
Aliendelea kudai kuwa tarehe na eneo walipofanya kosa la
kwanza, walitenda kosa jingine la kumteka Kagenzi na kumpeleka katika Hotel ya
River View Hotel iliyopo Sinza, Kinondoni, Dar es Salaam, kwa nia ya kumnyima
uhuru wake.
Washtakiwa hao wanaotetewa na Wakili Peter Kibatala na
John Malya, walikana mashtaka yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi
wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kesi iliahirishwa hadi Machi 26 mwaka huu,
itakapotajwa tena.
Hakimu Lema aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili
kila mmoja ambao wanatoka katika taasisi inayotambulika au serikalini isipokuwa
walimu. Wadhamini hao walipaswa kusaini hati ya dhamana ya maandishi ya Sh
milioni 10.
Washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na
kupelekwa gereza la Keko hadi hapo upande wa mashtaka utakapomaliza kufanya
ukaguzi wa barua za wadhamini wao kuona kama wamekidhi vigezo.
Kabla ya kupandishwa kizimbani kwa washtakiwa hao,
Kamishna Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo cha makada watano wa
Chadema cha kumuweka chini ya ulinzi na kumtesa kwa muda wa saa 15 Kangezi ni
kosa kisheria, hivyo Jeshi la Polisi limewafunguliwa shauri la kushambulia hadi
kumjeruhi mlinzi huyo.
Kova alisema Jeshi la Polisi limechukua uamuzi huo
kutokana na maelezo pamoja na majeraha aliyoyapata Kangezi mara baada ya
kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
Alisema, ingawa Wakili wa Chadema, John Malya alimfikisha
Kangezi katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kumfungulia shitaka la kupanga
njama za kumuangamiza Dk. Slaa kwa kumuwekea sumu kwenye maji au chakula,
Kangezi kwa upande wake alitoa maelezo ya kutekwa nyara na makada watano wa
Chadema ambao walimuweka chini ya ulinzi na kumtesa hadi kumuumiza.
“Tumefungua mashauri mawili, la kwanza ni uchunguzi dhidi
ya tuhuma na mpango wa kutaka kumdhuru Dk. Slaa na pili ni uchunguzi dhidi ya
watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia Kangezi na kumsababishia
majeraha mwilini mwake,” alisema Kamishna Kova.
Kamishna Kova alisema kutokana na maelezo ya Kangezi,
Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa waliotajwa na Kangezi kuhusika
kumtesa na kumteka.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali wa mashauri yote
mawili kukamilika, yatapelekwa kwa Wakili wa Serikali ili wote wanaohusika
katika suala hilo wafikishwe mbele ya sheria.
No comments:
Post a Comment