Wednesday, March 25, 2015

HE HE HE HE.........mahaba mahabani.......SHOGA, NDOA USIICHEZEE MDAKO....

Najua umenisubiri kwa hamu kubwa bi shosti, ni mimi yuleyule mtambo wa kurekebisha tabia nimeingia kama upepo wa kimbunga.  Kwa vile nia ya kona hii ni kutibu si kubembeleza watu wala kuangalia sura zao. Unajua kuna baadhi ya wanawake wanatia kichefuchefu kufanya utani katika ndoa na
kuzifanya ndoa za siku hizi zipoteze maana na kushindwa kutofautisha yupi kaolewa na yupi kahaba.

Nimebahatika kuhudhuria kicheni pati nyingi nikiwa kama mgeni mwalikwa, nashukuru Mungu kila aliyenialika alikubali ushauri wangu. Siku zote nimekuwa nikiwaeleza kuwa anayejua ladha ya kitu ni yule aliyekionja hata akikielezea atakielezea kwa ufasaha zaidi tofauti na yule asiyeijua ladha atabahatisha kwa vile alisikia tu muonjaji akielezea utamu na uchungu wa kitu kile.

Kwa kweli bado nalia na maadili mabaya katika ndoa za watoto wetu wa karne hii, wewe mzazi unaalika watu kuja kumfunda mwari wakiwa hawajui nini maana ya ndoa kwa vile wamesikia basi ndiyo wanatoa mafundisho kwamba ndoa inatakiwa hiki na hiki, kwa kukisikia na si kwa uhalisia ndiyo maana wanakaa uchi mbele ya mwari sasa wamekuja kumfundisha mema au maovu?

Leo nataka kuzungumza na kina mama wakosa haya wasiyojua vibaya, inawezekana kabisa ndoa yako inawaka moto kutokana na ujinga wako kiburi kujisikia humjali mume unataka kila kitu ukipate usipopata mumeo humpi haki ya ndoa. Leo hii wewe unamcheza mwanao na kuwaita wakosa haya wenzako mje mumfunde mwari.

Mtamfundisha nini kama siyo wewe kuwa chanzo cha kuiharibu ndoa ya mwanao? Hao mashoga zako wanatoa nasaha za aibu mbele ya binti yako anayetaka kuolewa nawe upo pembeni unapiga vigelegele mtoto kaolewa kesho kaachika mbaya nani?

Japokuwa kicheni pati si sehemu sahihi ya kumfunda mwari, basi tutafute watu waliodumu kwenye ndoa zao kwa muda mrefu ili waweze kutoa nasaha halisia wala si za kuhisia. Hata mavazi yao ni somo tosha kwa mwanao kuonesha mwanamke anatakiwa kustiri maungo yake kwa vile mhusika wa kuyaona ni mumewe tu.

Mbele unamsimamisha mwanamke 
mwenye sifa ya kuchanganya wanaume kama zege nguo alizovaa mwili wote upo nje na yeye anakueleza eti ndoa ni ngumu mheshimu mumeo. Wakati yeye pengine ameachika ndoa zaidi ya tatu.

Siku zote mfano mzuri ni wa vitendo si wa maneno, anayekufunda ukimuangalia kweli anachokisema ndicho anachokifanya. Kwako unamchukulia kama mfano wako katika maisha ya ndoa, ili ukiteleza basi umkimbilie mara moja  kukupa mungozo wa ndoa yako ili ujue umejikwaa wapi na ufanye nini.

Kingine wazazi sisi ndiyo tunatakiwa kuwa viongozi wa watoto wetu waipende ndoa kupitia maisha yetu ya ndani ya wewe na mumeo. Ndani ya nyumba hamzungumzi au mama anamdharau baba. Pale unamfundisha nini mwanao ina maana na yeye atajua kumbe kumdharau mwanaume ni jambo la kawaida na ni haki ya msingi.

Kama kweli tuna nia nzuri na watoto wetu basi sisi ndiyo walimu wa kwanza kuhakikisha ndoa zao zinadumu. Tujiepushe kuwashirikisha watu wasiojua thamani ya ndoa, kila aliyeionja ndoa ataielezea kwa ufasaha zaidi ili muolewaji basi apate faida na kujiandaa vizuri katika ndoa yake.

Wazo langu jipya ambalo najua litakushtua lakini kama wazazi mtalifanya hili basi nina imani watoto wenu wa kike watapata faida kubwa katika ndoa zao.

Muda ukikaribia mtoto wako wa kike kuolewa kama hakupitia unyago mweke chini ukiwa na shoga zako waliodumu kwenye ndoa zao kwa muda mrefu mwelezeni ndoa ni nini, utamu na uchungu wa ndoa ambao wote umebebwa na upendo, heshima, adabu, huruma na uvumilivu.


Nina imani somo hili likifanyiwa kazi, tutafanya ndoa zipate heshima kuliko kuwaita wahuni kutukana mbele yamwari wetu.
Chanzo: Global publishers

No comments:

Post a Comment