Saturday, March 28, 2015

MAMA WA WATOTO WALIOKUWA WAKIBAKWA NA BABA YAO HUKO KIBAHA APOKEA VITISHO TOKA KWA NDUGU WA MUME


Siku chache baada ya baba aliyedaiwa kubaka watoto wake wawili wakazi wa wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani kutiwa mbaroni na polisi, mama wa watoto waliokuwa wakitendewa unyama huo ameanza kupokea vitisho kutoka kwa  baadhi ya ndugu wa mume wake.

Mama huyo alisema kuwa baada ya ndugu wa mume wake kupata taarifa ya kukamatwa kwa ndugu yao wameanza kumtisha ikiwamo ya kutishiwa kuondolewa eneo analoishi  na kususiwa kuhudumiwa  watoto wake.

Kutokana na vitisho hivyo mama huyo ameomba msaada serikalini ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kutokana na vitisho anavyopokea kutoka kwa ndugu wa mtuhumiwa.

“Nasikia uchungu sana, bado watoto wangu ni wadogo na wote bado wanasoma, tegemezi kuu mimi, naomba wadau wanisaidie nikiendelea kutishiwa  na pia nisaidiwe waendelee kupata elimu, kwa sasa baada ya tukio hili nitakwama kiuchumi maana mtaji umekwisha kwa siku hizi nne tangu tukio limegundulika sijaweza kwenda kwenye biashara zangu za mboga mboga nasimamia familia na hili suala bado tunaendelea nalo polisi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema ofisi yake imepata taarifa za mama huyo kupata vitisho kutoka kwa ndugu wa mtuhumiwa  na kwa sasa jeshi hilo inalifuatilia kwa karibu zaidi ili kuweza kuwabaini wahusika na watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo husika.

“Hao  ndugu wanaomwambia huyo mama kafanya kosa kwenda kuripoti kituo cha polisi  wanakosea sana, maana tukio lenyewe ni la kinyama sana, miaka zaidi ya miwili baba mzazi anawatumia watoto wake tena wadogo kinyumba wao wanaona ni jambo dogo, sasa tunawafuatilia hao na tukiwabaini nao tutawashughulikia,” alisema Matei.

Alisema, “Taarifa imeshakuwa ipo wazi na majibu ya daktari yameshaonyesha wale watoto wamefanyiwa kitendo kibaya na zaidi wameharibiwa kiasi kwamba inasemekana kama wangeendelea zaidi kufanyiwa unyama huo  wangeweza hata kupoteza maisha,kwa hiyo huyo mama alikua sahihi kusema na angesemea wapi zaidi ya kituoni­, kwa hiyo tutawasaka hao ndugu wanaomtishia huyo mama tuwachukulie hatua.”


Naye mwalimu mkuu Shule ya Msingi Miembe, Saba Rajab Chalamila anakosoma mmoja wa watoto hao waliobakwa na katibu wa watoto waishio katika mazingira magumu Mtaa wa Miembe Saba wamesema kwa sasa wanaangalia uwezekano wa kumsaidia binti huyo kupata vifaa vidogo vidogo vya darasani kama kalamu na madaftari wakati huu na anajiandaa na mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
Chanzo Mwananchi

No comments:

Post a Comment