Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta
Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi
wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda. Alisema tukio hilo ni la saa 8 usiku wa kuamkia
Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo
hakuwepo wakati huo.
Akielezea zaidi, Kamanda Mwaruanda alisema usiku
huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama
yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza
kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia mtoto huyo,
mwenye ulemavu wa ngozi.
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo
walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi
ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili
wake na kumjeruhi vibaya … “Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba
hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja
cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana,”
alibainisha.
Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi
wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini
humo.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, mtoto huyo amelazwa
katika katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa
matibabu akiwa pamoja na mama yake mzazi.
“Watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa,
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi
kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo hicho cha kiganja
cha mkono wa mtoto Baraka,” alisisitiza Kamanda.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment