NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amenusurika kuuawa na mlinzi wake.
Hilo limebainika baada ya kitengo cha ulinzi cha chama hicho kutibua mpango
unaodaiwa kuratibiwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TIS), wa kumuua
kiongozi huyo kwa kumtumia mlinzi wake binafsi (PSU), Khalidi Kagenzi.KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amenusurika kuuawa na mlinzi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati
Kuu ya chama hicho, Mabere Marando, alisema Kagenzi akiwa mlinzi binafsi wa Dk.
Slaa katika kipindi cha miaka miwili, amebainika kutumiwa na vyombo vya usalama
vya nchi pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuvujisha siri za chama hicho,
na kupewa kazi ya kumuua katibu huyo wa Chadema.
Akielezea tukio lililombaini mlinzi huyo, Marando alisema lilitokea Ijumaa
iliyopita baada ya mashushushu wa chama hicho kumwona mlinzi huyo akipanda gari
lenye namba za usajili T 213 ARS linalodaiwa kutumiwa na Ofisa Usalama wa Taifa
wa Kinondoni.
“Baada ya kuonekana ndipo mashushu wa Chadema walichukua jukumu la kumkamata na
kumfanyia mahojiano ambapo walifanikiwa kumpekua katika simu zake mbili
zinazotumia mitandao ya Vodacom, Airtel na Tigo.
“Katika simu hizo, walikuta ujumbe mfupi wa maneno uliokuwa ukitoka kwa …,
aliyempigia mara tatu na kumtumia fedha kati ya Desemba 4, mwaka jana na Julai
14, 2014. Namba nyingine zilizokutwa zilikuwa za maofisa Usalama wa Taifa,”
alisema.
Aliongeza kuwa baada ya upekuzi huo katika ‘Note book’ na simu zake, waligundua
kuwa kigogo mmoja wa ngazi za juu wa CCM alimtumia muda wa maongezi wa Sh
50,000 kwa namba ya simu 0764 …222 Julai 14, 2014 na Desemba 4, 2014 alimtumia
Sh 150,000.
Marando alisema katika upekuzi wa kwenye simu, walibaini mazungumzo yake yote
yalikuwa yakitumia muda usiopungua saa mbili hadi tatu, na mara zote ni wakati
ambao Chadema walikuwa wakifanya mikutano yao ya ndani.
“Alikuwa akitumia simu yake kurekodi kila kilichokuwa kikizungumzwa kwenye
mikutano yetu na kusambaza kwa CCM, na iligundulika akiwasiliana na maofisa wa
Usalama wa Taifa waliofikia 22,” alisema.
Marando aliongeza kwa kusema kuwa kama isingekuwa suala la kutolewa kwa uhai wa
Dk. Slaa, wasingezungumzia suala hilo na pia anazungumziwa huenda akachaguliwa
kuwa mgombea wa urais wa Ukawa.
Alisema kuwa jana chama hicho kimetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kuchukua
hatua za kisheria ambao ndio wanaweza kutaja majina ya maofisa usalama wa
waliohusika na mpango huo.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu afya ya Dk. Slaa, alisema
hadi jana alikuwa salama ingawa bado hajapima kubaini hilo.
Marando alisema baada ya kugundulika kufanya hujuma hizo, Ijumaa iliyopita
walimsimamisha majukumu yake ya kumlinda kiongozi huyo hadi pale uchunguzi
dhidi yake utakapokamilika.
Ingawa chama hicho hakikueleza kiasi cha fedha ambacho mtuhumiwa alipewa
kufanyia shughuli hiyo, lakini kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa kwa Idara ya
Ulinzi wa chama hicho, alionyesha ndani ya simu yake kiasi cha Sh milioni 7
ambazo zilikuwa muda wa maongezi kwa muda wa miaka miwili.
MTANZANIA ilimpomtafuta kigogo wa CCM aliyetajwa, hakupatikana ofisini kwake
Lumumba wala Dodoma, na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila
kupokewa.
Pamoja na jitihada hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ‘SMS’ hakuweza
kujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kuwa tangu Ijumaa baada ya
kugundulika kwa mpango huo walinzi wa chama hicho walikuwa wakimsulubu kwa
kipigo Kagenzi ili kuweza kupata ukweli.
Huku akiwa anapigwa, Kagenzi alilazimika kutaja majina ya watu wote waliokuwa
wakifanya kazi hiyo ikiwamo kuandika taarifa maalumu ikiwamo shughuli binafsi
za Dk. Slaa.
POLISI WAZUNGUMZA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillus Wambura,
alithibitisha kufikishwa mtuhumiwa huyo katika Kituo cha Polisi Oysterbay
ambapo alisema wanaendelea na mahojiano naye ili kujua ukweli wa tuhuma
zinazomkabili.
“Tumempokea leo (jana) mtuhumiwa, tumeanza kuwahoji waliomleta na baadaye
kumhoji muhusika ili tuweze kubaini ukweli kuhusu tuhuma dhidi yake,” alisema
Kamanda Wambura.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania
No comments:
Post a Comment