Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mgwira amesema
chama hicho hakina matatizo na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na hata sasa
kinasubiri majibu ya barua yao waliyoituma kwa umoja huo kuomba kuunganishwa.
Mgwira alitoa kauli hiyo wakati chama hicho kilipofanya
ziara ya kutembelea hospitali ya mkoa ya Mt Meru kugawa zawadi mbalimbali
katika wodi ya kinamama ikiwa ni njia ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu
kuanzishwa kwake.
Alisema ACT-Wazalendo wanaunga mkono muungano wowote wa
vyama vya upinzani nchini ulio halali.
“Hatuna matatizo na Ukawa tunaunga mkono muungano wowote
wa upinzani ulio halali,” alisema kiongozi huyo
Alisema tangu waandike barua ya kuomba mwongozo wa namna
ya kujiunga na Ukawa, bado hawajapata mrejesho.
“Tunatamani kuunganisha nguvu katika siasa za vyama vya
upinzani na sasa tunasubiri majibu ya barua yetu ya kuomba kuingia Ukawa,”
alisema.
Alisema kuwa chama hicho kimepokewa vizuri na wananchi wa
mikoa mbalimbali nchini na katika ziara ya awamu ya kwanza walifanikiwa
kuingiza jumla ya wanachama wapya 700.
“Tumepokewa vizuri mikoani tumefanikiwa kuingiza
wanachama wapya na hoja ya umoja na uzalendo watu wameipokea vizuri,”
alisisitiza Mgwira.
Akipokea misaada katika hospitali hiyo Muuguzi Mfawidhi,
Sifael Masawe alisema kwamba misaada hiyo itasaidia kupunguza shida za
wagonjwa.
waliofika hospitalini hapo na kuwataka wengine kujitokeza
kuwaunga mkono.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment