Umati wa watu wakiwa karibu na kituo cha redio na
televisheni vya taifa RTNB, Mei 13 mwaka 2015.
Nchini Burundi, aliyekua mkuu wa majeshi Jenerali
Godefroid Niyombare ametangaza Jumatano Mei 13 kuwa rais wa nchi hiyo Pierre
Nkurunziza amepinduliwa madarakani.
Hayo yanajiri wakati Pierre Nkurunziza anashiriki
Jumatano wiki hii mkutano wa kikanda wa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuhusu mgogoro unaoendelea nchini Burundi.
Burundi imekua ikishuhudia maandamano ya raia wakipinga
muhula wa tatu wa Pierre Nkurunziza. Kwa muda wa majuma kadhaa mitandao ya
kijamii imekua imefungwa, lakini baada ya mapinduzi hayo mitandao hiyo
imefunguliwa.
Kituo cha redio RPA ambacho kimekua kimefungwa tangu
maandamano hayo yaanze, kimeanza kupeperusha matangazo yake baada ya mapinduzi
hayo, hata redio za kibinafsi mbili ambazo ni Bonesha Fm na Isanganiro, ambazo
matangazo yake yalikua hayasikiki mikoani na katika baadhi ya maeneo ya nchi
jirani, kwa sasa matangazo ya redio hizo yanasikika.
Mapema Jumatano asubuhi, raia kutoka wilaya zote za mji
wa Bujumbura walikua wakijaribu kuingia mjini kati Bujumbura, bila mafaanikio.
Lakini kuna kundi la wanawake na wasichana ambao wamefaulu kuingia kwenye eneo
la Uhuru mjini Kati Bujumbura.
Hata hivyo Ikulu ya rais imetangaza kupitia akaunti yake
ya twitter kuwa mapinduzi hayo yamefeli, baada ya jeshi kuingilia kati na
kudhibiti hali ya mambo. Hata hivyo raia wameingia kwa wingi mjini kati
Bujumbura baada ya kusikia tangazo hilo, huku askari polisi wakionekana kuingia
katika makambi yao.
Wakati huo huo wanajeshi wengi wameonekana wakiizingira
redio na televisheni vya taifa pamoja na uwanja wa ndege wa Bujumbura.
RFI
No comments:
Post a Comment