KATIKA hali isiyo ya kawaida, mahabusu 12 waliokuwa
wakipelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, jana waligoma
kushuka katika gari la polisi wakidai mahakama imeshindwa kusikiliza malalamiko
yao.
Tukio hilo limetokea jana
ambapo baadhi ya mahabusu waliozungumza na waandishi wa habari kwa
nyakati tofauti wakiwa wamelala ndani ya gari la polisi, waliwatupia lawama
baadhi ya wanasheria wa Serikali wanaosimamia kesi hiyo.
Mahabusu hao ambao wanakabiliwa na Kesi ya Jinai namba 83
ya mwaka 2009 inayohusiana na unyang'anyi wa kutumia silaha katika Mgodi wa
Dhahabu wa Resolute, walisema, kesi hiyo ina miaka saba hadi sasa, lakini bado
haijasikilizwa hivyo kusababisha usumbufu kwao na ndugu zao.
Waliutaka mhimili huo, kusikiliza kesi zote za zamani
haraka iwezekanavyo na kuzitolea hukumu.
Mshtakiwa mmojawapo katika kesi hiyo, Edward Bunela
alisema mahakama inapaswa kuwatendea haki kwani wamekaa mahabusu muda mrefu na
kumuomba Jaji Mkuu Othumani Chande, kuingilia kati kesi hii ili hatua
iliyosalia ikamilike kwa muda stahiki.
"Tunamuomba Jaji Mkuu aingilie kati kesi hii ambayo
imedumu miaka saba bila kutolewa hukumu...upande wa Jamhuri unatusumbua wakati
sisi tunataabika gerezani, bora hukumu itoke tujue hatima yetu," alisema
Bunela.
Mshtakiwa mwingine, Shaabani Amour, alisema kuwa hawajui
hatima yao kwani mwenendo wa kesi hiyo haufahamiki na kuziomba mamlaka za juu
kuwasaidia ili kutekeleza agizo la Jaji Mkuu ambalo alizitaka Mahakama zote nchini
kuharakisha usikilizwaji wa kesi mbalimbali zilizokaa muda mrefu bila kutolewa
hukumu.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo ambaye anasikiliza kesi
hiyo; Spraphine Nsana, alisema tatizo ni wakili wa washtakiwa namba 14, 15 na
16 ambaye ana kesi katika Mahakama ya Rufaa; hivyo hakuweza kuhudhuria kwenye
shauri hilo.
Alisema wakili huyo aliwasilisha barua ya taarifa
mahakamani, hivyo shauri hilo litasomwa Mei 25, mwaka huu.
Baadhi ya ndugu wa washtakiwa, wameutupia lawama upande
wa Jamhuri kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kesi hiyo kuchukua
muda mrefu na hakuna kinachoendelea.
Hivi karibuni, Jaji Chande alipofanya ziara ya kikazi
mkoani humo, aliwataka Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya, Mkoa na Mahakama
Kuu kuhakikisha wanamaliza kesi ambazo zina miaka saba hadi miwili ili
kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani katika mkoa huo.
MAJIRA
No comments:
Post a Comment