Kikwete aagiza bomoabomoa Dar.
Rais Jakaya Kikwete ametoa maagizo magumu kwa viongozi wa
Halmashauri ya Jijini la Dar es Salaam kwa kuwataka kuzibomoa nyumba zote
zilizojengwa katika kingo za mifereji, mito na mikondo ya kupitishia maji.
Nyumba za wakazi wake zimezingirwa na maji kutokana na
baadhi ya watu kujenga katika mifereji ya kupitisha maji na mabondeni.
Rais Kikwete akiwa eneo la Boko alimuuliza Mkuu wa Wilaya
ya Kinondoni, Paul Makonda na Mhandisi wa Manispaa hiyo, Baraka Mkuya, sababu
za maji kujaa katika nyumba za watu na hatua zilizochukuliwa kuyaondoa.
Makonda alijibu kuwa, Manispaa ya Kinondoni imeandaa
bajeti ya Sh. bilioni 3.5 ili kuondoa maji hayo pamoja na kutengeneza
miundombinu.
Mkuu huyo wa wilaya alieeza sababu za kujaa maji katika
nyumba kuwa imesababishwa na baadhi ya watu kujenga nyumba zao juu ya mifereji
na mikondo ya kupitishia maji yanayoelekea baharini.
“Mkuu wa wilaya na watendaji wako hapa kama mnajua sababu
ni watu kujenga juu ya mitaro bomoeni nyumba zote msitake kumridhisha kila mtu
hamtaweza na hata mtakaowaridhisha hawatawashukuru,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema wale ambao hawataki nyumba zao
zisibomolewe licha ya kujengwa juu ya mifereji watakuwa ni wajinga kwani hata
katika nyumba hizo hawawezi kuishi kutokana na kujaa maji. Aidha, alimwagiza
mkuu huyo wa wilaya na wataalamu wake kutumia pampu 27 za manispaa hiyo
kunyonya maji kutoka katika nyumba ambazo maji yamejaa badala ya kufikiria
kuandaa miradi ya fedha nyingi.
Rais Kikwete aliagiza manispaa hiyo kukaa chini na watendaji
wake ili kupata jawabu la kumaliza tatizo la kujaa maji katika nyumba za watu,
vinginevyo maeneo hayo yatageuka kama maeneo ya kufugia samaki.
“Mhandisi hivi hauna maarifa, kwanini mmefikiria kuandaa
fedha nyingi za kutengeneza miundombinu badala ya kuangalia namna ya kuondoa
maji katika nyumba za watu, tumia maarifa yangu niliyoelekeza, achana na hayo
ya kwako ambayo hayasaidii kumaliza tatizo kwa muda mfupi,” alisema.
Akiwa ofisi za Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es
Salaam (Dawasco), Rais Kikwete, alihoji sababu za maji kujaa katika ofisi hizo
wakati kuna wataalamu wa maji ambao wanaweza kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo, Mhandisi Maro Wambura alimweleza Rais kuwa
maji hayo yanatoka kwenye kiwanda cha saruji cha Wazo ambayo yanatakiwa kuelekea
baharini, lakini yamekuwa yakikwama kwenye ofisi hizo kutokana na baadhi ya
watu kujenga katika mikondo ya kupitishia maji.
Wambura alisema kutokana na tatizo hilo ambalo
linajitokeza kila mwaka kila unapofika msimu wa mvua, wanalazimika kufunga
ofisi na kwamba hawana uwezo wa kuyaondoa bila kushirikiana na manispaa.
Naye Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Mkuya, alisema
awali walimwita mkandarasi wa Kichina kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya
eneo hilo, lakini kazi haikufanyika kwa sababu mkandarasi huyo alikuwa
anahitahi kulipwa fedha nyingi.
Rais Kikwete akiwa eneo la Mkwajuni, Mkuu Wilaya
Kinondoni, Makonda alimweleza kuwa eneo hilo kila mwaka limekuwa likikumbwa na
mafuriko kutokana na bonde na asilimia kubwa ya wakazi wake wamejenga nyumba zao
katika mkondo wa mto Msimbazi.
Makonda alisema kutokanana na hali hiyo, kaya 102
zilipewa viwanja eneo la Mabwepande ili wahame bondeni, lakini kaya 42 kati ya
hizo zimeshikilia maeneo Mambwepande na Mkwajuni.
‘WA MABONDENI HAMENI’
Rais Kikwete aliagiza viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha
watu wote waliojenga nyumba zao bondeni Mkwajuni wanahamishwa kwani suala la
kuzuia mvua lipo nje ya uwezo wa serikali.
“Mlioko mabondeni hatuna namna ya kuwasaidia kwa sababu
mvua zilizonyesha mwaka huu ni nyingi kupita kiasi, hivyo mkubali tu yaishe
muondoke, hakuna jinsi hali hii itandelea kila mwaka na itajirudia,” alisema
Rais Kikwete.
Alisema wananchi watakaokuwa tayari kuhama serikali
itawasaidia kwa kuwapatia viwanja ili waondoke eneo hilo hatari.
Mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam kutokana na
mvua zinazoendelea kunyesha na hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 12, huku
mamia wakikosa makazi kutokana na nyumba zao kuzingirwa na nyingine kujaa maji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki,
ameshatangaza na kusisitiza kwamba mwaka huu hakuna mtu atakayesaidiwa na
serikali kutokana na kukaidi maagizo ya kuhama maeneo ya mabondeni ambayo ni
hatarishi.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment