MKUU wa Majeshi wa zamani nchini Malawi, Jenerali Henry
Odillo amekamatwa akihusishwa na vitendo vya rushwa vya mamilioni ya dola.
Jenerali Odillo na aliyekuwa makamu wake,
Luteni Kanali
Clement Kafuwa, wanashutumiwa kupanga mkataba wa kuingizwa kwa vifaa vya
kijeshi nchini Malawi, vifaa ambavyo havikuwasilishwa nchini humo.
Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini Malawi (ACB),
inawashikilia viongozi hao wa kijeshi wa zamani ikiwa ni sehemu ya uchunguzi
unaofanywa ndani ya Serikali kuhusu kashfa ijulikanayo kama ‘Cashgate.’
Viongozi hao wa kijeshi hawakuzungumzia lolote kuhusu
shutma hizo.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),
mjini Blantyre amesema watumishi kadhaa wa umma wameshutumiwa kuhusika kwenye
kashfa ya ‘Cashgate.’
Kashfa hiyo imebainisha kuwepo kwa matumizi ya fedha bila
huduma kutolewa.
Taarifa inasema kuwa Jenerali Odillo na Luteni Kanali
Clement Kafuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia ofisi vibaya, uzembe wa
ofisa wa uma katika kuhifadhi fedha na biashara haramu ya fedha.
Uchunguzi umebaini kuwa Jeshi lililipa kiasi cha dola
milioni 4.4 kwa ajili ya vifaa hewa.
Kashfa ya ‘Cashgate’ ilijitokeza kwa uchache Septemba
2013, baada ya jaribio la mauaji dhidi ya Mkurugenzi wa Bajeti wa Wizara ya
Fedha, Paul Mphwiyo.
Siku kadhaa kabla, mtumishi mmoja wa Serikali alikutwa na
zaidi ya dola 300,000 kwenye gari lake.
Fedha zaidi zilizuiliwa kutoka mikononi mwa wafanyakazi
wa Serikali walizokuwa wamezificha nyumbani na kwenye magari.
Nchi wahisani wa Malawi walizuia kiasi cha dola
milioni150 kushinikiza uchunguzi zaidi kufanyika.
No comments:
Post a Comment