Kampuni ya Ujenzi ya Tanpile Ltd ya China inalalamikiwa
na wananchi waishio katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa uchafuzi wa mazingira
na kelele usiku kucha, zinazosababisha washindwe kupumzika.
Kampuni hiyo licha ya kupewa amri ya Mahakama (stop
order) kusitisha shughuli zake za uchanganyaji wa zege katika kiwanda chake
kilichofunguliwa katika makutano ya barabara za Samora, Aggrey na Mosque jijini
hapa, wamekaidi na hivyo kuendelea na uzalishaji nyakati za usiku.
Baada ya kubainika hayo, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry
Silaa, aliamua kufanya ziara ya ghafla kwenda kushuhudia kinachofanyika kiwandani
hapo mwezi uliopita, na kukutana na adha ya kukunjwa shati na Wachina hao.
Silaa ambaye
alikuwa ameongozana na baadhi ya Mgambo wa Manispaa ya Ilala, aliokolewa na
walimzunguka kabla ya kutoa amri kwa Wachina hao kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi,
Dar es Salaam.
Meya
alithibitisha kufanyiwa vurugu na Wachina hao, lakini aliamua suala hilo
liamuliwe kisheria baada ya kufika polisi ambao pia walithibitisha kulipokea na
kwamba wangali wakilichunguza.
Wakazi wa maeneo
hayo wameieleza JAMHURI kuwa kero kubwa wanayoipata ni kukosa usingizi kutokana
na kelele za mitambo ya kuchanganyia zege, malori yanayoingiza mchanga
kiwandani hapo na wafanyakazi wanaopiga kelele usiku kucha.
Wanasema athari nyingine zinazotokana na uchafuzi huo wa
mazingira ni kusambaa kwa vumbi la saruji na kokoto katika makazi yao na
kusababisha wapatwe na maumivu ya vifua na kikohozi.
“Hii ni kero kubwa mno, hatupati usingizi kwa muda mrefu
ni kelele tu za malori yanayoleta kokoto na honi zinapigwa usiku kucha na vumbi
la saruji linaingia katika makazi yetu, Serikali imeziba masikio pamoja
kufikishiwa malalamiko yetu,” anasema Daud Mushi, mkazi wa Mtaa wa Samora
katikati ya jiji.
Mushi anasema wamefikisha malalamiko yao muda mrefu
katika Ofisi ya Kata ya Mchafukoge na Manispaa ya Ilala, lakini hakuna hatua
yoyote iliyochukuliwa hadi sasa na kinachoendelea ni wamiliki wa kiwanda hicho
kufanya uzalishaji wa zege nyakati za usiku.
Anasema kinachoshangaza ni viongozi wa jiji kuruhusu
Wachina kufungua kiwanda cha kuchanganya zege katikati ya jiji na kwenye makazi
ya watu, bila kujali athari za uchafuzi wa mazingira unaotokana na kiwanda
hicho.
Mkazi mwingine wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake
liandikwe gazetini, anasema ni kinyume na sheria za ardhi kubadili matumizi ya
ardhi kwa kuruhusu kiwanda kama hicho kuwekwa katikati ya jiji.
Anasema kinachoshangaza ni wamiliki wa kiwanda hicho
kupuuza amri waliyopewa ya kusitisha shughuli zao za uchanganyaji wa zege
katika eneo hilo.
“Nchi haina utaratibu kabisa, raia wa kigeni wanafanya
lolote wanalotaka na ujeuri wao unatokana na rushwa zinazoendekezwa na
watendaji nchini,” anasema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mchafukoga, Hassan Mkwawa,
anasema uongozi wa kiwanda hicho cha Wachina umekaidi kusitisha shughuli zake
licha ya kupewa amri kufanya hivyo kwa zaidi ya wiki mbili.
Mkwawa ameieleza JAMHURI kuwa uchafuzi wa mazingira
unaofanywa na kiwanda hicho kilichoko katikati ya makazi jijini haukubaliki
kabisa, lakini taasisi zinazohusika zimeshindwa kuchukua hatua dhidi ya kampuni
hiyo ya Tanpile Ltd.
Licha ya kelele na vumbi linaloleta kero kwa wakazi wa
maeneo hayo, Mkwawa anasema barabara zimekuwa zikichafuliwa kwa kokoto
zinazomwagika na kuleta usumbufu mkubwa watu wanaosafisha barabara hizo.
Naye, Ofisa
Mazingira wa Manispaa ya Ilala, Abdon Mapunda, alipohojiwa na gazeti hili
kuhusu kero hiyo ya uchafuzi wa mazingira unayotokana na kiwanda hicho, anasema
wahusika hawana kibali cha kuendesha shughuli zao katika eneo hilo.
Mapunda anasema wamewapa nakala ya amri ya kusitisha
shughuli zao wiki mbili zilizopita, lakini wamekaidi na kuendeleza shughuli zao
za kuchanganya zege katika eneo hilo nyakati za usiku.
“Pamoja na kuwapa
nakala hiyo, bado wanaendeleza uchafuzi wa mazingira unaoambatana na vumbi la
kokoto, saruji na kelele ambazo ni kero kwa wakazi hao, na tunachosubiri ni
hatua zitakazochukuliwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC),”
anasema Mapunda.
Meneja Uhusiano wa NEMC, Ruth Mgwaza, anasema wanakusudia
kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wa kiwanda hicho kwa kuwa hawana kibali
chochote kinachowaruhusu kuweka mitambo ya kukoroga zege katikati ya jiji.
Anasema uchafuzi wa mazingira unaoendeshwa na kiwanda
hicho kinachomilikiwa na raia hao wa nchini China, haukubaliki na kwamba hata
wahusika wanapoitwa wamekuwa wakikaidi wito mara kwa mara.
Imeelezwa kwamba zege linalochanganywa katika kiwanda
hicho linatumika kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kigamboni na jengo la Taasisi
ya Mwalimu Nyerere (MNF) linalojengwa mkabala na Ofisi za Jiji la Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment