KESI za kulawiti watoto mashuleni imeelezwa kuwa
wanaofanya ukatili huo wa kijinsia kwa watoto hao baadhi yao ni walimu
wanaowafundisha na kwamba kutokana na walimu hao kuhitajika shuleni hapo baadhi
ya uongozi wa shule umekuwa ukishindwa kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na
kushindwa kuripoti katika dawati hilo.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa
Dawati la Jinsia mkoani Kilimanjaro, Prisca Maganga aliwaambia waandishi wa habari wa
mikoa ya Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha waliotembelea dawati hilo
mwishoni mwa wiki kuwa kwa mwezi Januari hadi Februari mwaka huu wamepokea kesi
10 za kutelekeza familia zikiwemo kesi 2 za kubaka.
Alisema kesi mbili hadi tatu za kulawiti
wanafunzi wa shule za msingi mkoani Kilimanjaro zimeripotiwa kwa mwezi Januari
hadi Februari mwaka huu katika dawati la jinsia mkoani humo ambapo katika kesi
10 zilizoripotiwa katika dawati hilo zilikuwa zikiongozwa na kesi za kutelekeza
familia.
“Kesi za ukatili wa majumbani kama kutelekeza
familia zinaongoza kwa mkoa wetu, tunapokea kesi 10 hadi 15 kwa mwezi chimbuko
likiwa ni kiuchumi na changamoto za maisha na akina mama wengi wanatelekezwa kwa
sababu ya utegemezi na sababu nyingine wanaume kuwa na tamaa na kuoa mke
mwingine,” Alisema mkaguzi huyo wa Polisi.
Akielezea ukatili mwingine wa majumbani, alisema
wazazi wengi wamekuwa wakitoa adhabu za viboko na vipigo vinavyokithiri kwa
watoto wao kwa lengo la kuwakanya kitabia bila kujua kwamba zipo sheria
zinazomlinda mtoto huyo dhidi ya ukatili huo na wakati mwingine wazazi hao
kulazimika kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Baba mmoja alikuwa akimpiga mtoto wake kwa
mjeledi na kuacha alama mbaya mwilini mara kwa mara na kuathiri masomo na
makuzi yake na kumpiga mama wa mtoto huyo kumbe wazazi hao ni waathirika wa
ugonjwa wa Ukimwi, tunashukuru walimu wa shule aliyokuwa akisoma mtoto huyo
kutupa taarifa na ushirikiano hadi mtoto huyo kuendelea na masomo yake mpaka
sasa,” alisema.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment