WANAJESHI wawili waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa
baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa ndugu
wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira, wamekata rufaa kupinga adhabu
hiyo.
Wanajeshi hao ambao ni ndugu , MT 75854 Koplo Ally
Ngumbe wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na
MT 85067 Koplo Mohamed Rashid (JKT Mbweni), wamewasilisha rufaa hiyo katika
Mahakama ya Rufani.
Katika rufaa yao, wanajeshi hao wana hoja tatu wakipinga
hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa Novemba 20, 2012 na Jaji Zainab Mruke
wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika hoja zao, wanajeshi hao wanadai Jaji
alikosea kisheria kutoa uamuzi kwa kutozingatia kanuni za kuthibitisha mashitaka
pasipo kuacha shaka yoyote, ambalo ni jukumu la upande wa mashitaka.
Aidha, wanadai Jaji alikosea kisheria kwa kutoa
hukumu inayoegemea ushahidi wa kimazingira, bila kuzingatia ushahidi wa utetezi
wa wakata rufaa. Katika hoja nyingine wanadai alishindwa kuchanganua itirafu
katika majina kwenye taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo.
Awali, wakati hukumu hiyo inatolewa walihukumiwa
washtakiwa watatu akiwemo aliyekuwa MT 1900 Sajenti Roda Robert wa Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni, ambaye alifariki dunia mwaka jana mkoani
Dodoma wakati akisubiri utekelezwaji wa hukumu hiyo.
Katika hukumu hiyo, Jaji Zainab alisema upande wa
mashitaka umethibitisha kesi yao bila shaka na hivyo Mahakama imeona kuwa
washitakiwa wote wana hatia na walimuua marehemu Fundikira kwa
kukusudia.
Hata hivyo, alisema hakuna shahidi aliyethibitisha
kuwa aliwaona washitakiwa wanavyomuua Swetu, bali mashahidi watatu
walithibitisha kuwaona washtakiwa wakiwa na Swetu kabla ya kukutwa na
mauti.
Alisema anawatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu
kunyongwa hadi kufa kwa kuwa ushahidi wa mazingira umeowanyooshea kidole
washitakiwa kuwa wanahusika na mauaji hayo.
Ilidaiwa Januari 23 ,2010 katika eneo la Kinondoni,
Dar es Salaam, washtakiwa hao walidaiwa kumuua marehemu Fundikira.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment