Nimetafiti maeneo mbalimbali na kuongea na wadau kuhusu
mwelekeo wa mapambo ya nyumbani utakavyokuwa 2016 kwa nyumba za Watanzania
walio wadau wa mapambo ya nyumbani. Kuna mawazo mengi ya nini kitashamiri mwaka
huu, na kwa hivyo si rahisi kuorodhesha kila kitu na kwahivyo nimekuwekea
maeneo 6 kuonyesha mwelekeo utakavyokuwa.
Karatasi za ukutani yaani wallpaper – Kwa mwaka 2015
karatasi hizi zimekuwa kivutio sana na hasa zile zenye michoro ya mawe ya mtoni na
vitofalitofali. Pamoja na kwamba michoro
hii imevuma sana kwa mwaka jana, mwaka huu inaelekea wallpaper za maua za aina
ya 3D ndio zitashika kasi. Hii ni kwa ajili wenye nyumba wengi wameshaanza kuwa
na wasiwasi kwamba hizi mbili za 2015 ziko walau kwenye kila nyumba yenye
wallpaper.
Kuepuka mimea kugusana na nyumba - Wengi wa wadau wa eneo
hili wanabainisha kuwa bustani za kushikana na ukuta wa nyumba zinaenda kupotea
kuanzia mwaka huu na kuendelea. Hii ni kwa
vile wenye nyumba wa kisasa wamegundua bustani hizi zinachangia kuchafua
na kuozesha eneo la chini la ukuta wa nyumba. Badala yake sasa, ukanda huu wa
kuzunguka nyumba umetengwa kama kawaida ila badala ya kuoteshwa mimea na maua
unawekwa vitu kama mawe meupe ya mapambo ama wapo wanaoweka vigae na wengine
wanaweka marumaru za nje. Wachache bado wanaweka maua ila ni ya kwenye vyungu
vichache vilivyo mbalimbali. Vyungu hivi vimewekwa juu ya sakafu ngumu na kwa
mantiki hiyo hakuna udongo unaogusana na ukuta.
Meza za marble kuzidi kushamiri - Meza za marble hasa zile za chakula zilianza
kushika kasi toka mwaka jana na mwaka huu kasi yake inaongezeka. Hii
imechangiwa na uimara wake na kuwa za gharama nafuu na urahisi wa kusafisha na
kuzitunza. Vilevile meza hizi ni ndogo ambapo zimewavutia wengi ambao hawana
eneo kubwa la kulia chakula. Na hata wale wenye eneo kubwa bado wamevutiwa
kwakuwa wanataka sehemu ya nyongeza ya kuweka kabati la vyombo kwenye chumba
cha chakula. Kupanda sana kwa gharama ya mbao ngumu nayo ni sababu ya meza za
marble kushika kasi.
Hitaji la vitanda vya chuma kuongezeka – Vitanda vya
chuma na baadhi ya fenicha nyingine za chuma zina mwelekeo wa kushika kasi sana
mwaka huu. Vitanda hivi vimekuwa mkombozi wa karibia kila mtu kuanzia vijana
waliotoka vyuoni wanaoanza maisha hadi familia changa. Sababu ni zilezile kuwa
ni imara, bei nafuu na utunzani usiokuwa na changamoto nyingi.
Marumaru za mapambo – Kama tujuavyo sakafu za marimaru
zimejipatia umaarufu kwa nyumba za watanzania walio wengi wenye uwezo wa
kuzinunua. Tegemea kuona marumaru zenye maua kwa wingi ambapo nyingine zinabuniwa
kama vile ukiona kwa mbali utafikiri ni zulia lakini ukikanyaga kumbe ni
marumaru. Mwaka huu kutakuwa na ongezeko la marumaru za maua hasa kwenye sakafu
za sebuleni.
Vitendea kazi jikoni
- Mwaka huu tegemea vitendea kazi
vingi vya jikoni kuongezeka. Licha ya kipasha na kisaga chakula, maisha ya
jikoni yanazidi kurahisishwa kwa vitendea kazi vipya mbalimbali kama vile
kitendea kazi cha kuchanganya na kukanda unga wa chapati na maandazi, kitendea
kazi cha kusaga vitunguu swaumu, kitendea kazi cha kuchoma mahindi, mishikaki
na kadhalika
Naamini maelezo haya yamekupa mwelekeo wa baadhi ya mapambo
ya nyumbani kwa mwaka huu mpya wa 2016.
Vivi ni mshauri wa mapambo ya nyumba na bustani. Kwa
maswali au maoni piga/whatsapp 0755200023
No comments:
Post a Comment