Sehemu
kubwa ya uzuri wa muonekano wa nyumba ni rangi yake. Haijalishi ukubwa wa eneo
unalotaka kupaka rangi bali kupata fundi sahihi itaokoa muda, nguvu na pesa
zako kwa kipindi kirefu kitakachofuata.
Nimeongea
na Mkandarasi Kassim Ally na amesema kabla hujampa kazi ya kupaka rangi fundi
au mkandarasi anayekidhi vigezo vyako, hakikisha yafuatayo:
·
Uzoefu. Ni muda gani
fundi huyo amekuwa katika kazi hiyo? Hakikisha kuwa unampa kazi fundi ambaye
ameshakuwa kwenye kazi hiyo kwa miaka miwili na zaidi.
·
Wafanyakazi. Je huyo fundi/mkandarasi
unayetaka kumpa hiyo kazi ana wafanyakazi wake? Kazi ya kupaka ukuta rangi inahitaji hatua nyingi za
maandalizi ya ukuta kabla ya rangi ya mwisho kwahivyo inahitaji nguvu kazi
kubwa na ifanyike kwa muda mfupi ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea
kwa mfano ujio wa mvua na kadhalika.
·
Leseni. Ni vyema
kuhakikisha fundi unayetaka kumuajiri kwa ajili ya kazi yako ya rangi ana
leseni ya kazi hiyo. Hii ni muhimu sana hasa pale itakapotokea ajali kwa mfano
mfanyakazi wake anaweza kuanguka na kuumia vibaya au hata kusababisha kifo kama
ameanguka toka juu jingo refu. Leseni itamlinda yeye na wewe kisheria kwani
kazi inafanyikia kwenye eneo lako.
·
Rufaa: Fundi rangi
unayemtaka anaweza kukupa orodha ya watu kadhaa alowafanyia kazi ya rangi
kabla? Wapigie na hata ikiwezekana watembelee ongea nao na angalia kazi fundi
husika aliyofanya kabla hujaamua kumpa fundi huyo kazi yako.
·
Taaluma: Je fundi husika
anaweza kupendekeza ni malighafi zipi zitafaa zaidi kwa ajili ya kazi yako? Awe
ni mtaalam anayeenda na wakati, anayejua ni rangi na teknolojia gani mpya zaidi
iliyopo sokoni kwa wakati huo. Ashauri rangi na nakshi mbalimbali. Uzoefu hapa
unahusika.
·
Makadirio rasmi. Hakikisha fundi
unayetaka kumpa kazi anaweza kukupa makadirio ya muda na vifaa vyote vinavyohitajika
vikiwa kwenye maandishi.
·
Garantii. Mbali na
garantii zinazotolewa na viwanda vya rangi, fundi rangi anatakiwa aweze kukupa
garantii ya kazi yake. Maana yake ni nini? Ni kwamba fundi atapaka rangi
kipindi cha kiangazi, anamaliza kazi yake na inaonekana kuvutia kabisa machoni.
Lakini mvua zikianza mwezi mmoja au wiki kadhaa baadaye unaweza kushangaa ukuta
wa nje ulioloa maji ya mvua rangi yake inavimba malengelenge na inabanduka eneo
kubwa. Sasa hapo sababu inaweza kuwa huenda fundi hakusimamia wafanyakazi wake
vizuri na kwa hivyo wakapaka rangi ukuta wenye vumbi. Ama wakati wa kuchanganya
malighafi zinazohitajika vipimo havikuzingatiwa matokeo yake rangi inabanduka
chini ya mwezi mmoja. Kwa swala kama hili ndipo tunaposema ni vyema kuwa na
fundi mwenye uwezo wa kugarantii kazi yake hata kama ni kwa miezi mitatu tu.
·
Gharama. Kwa asili,
gharama ni swala linalotiliwa mkazo kwenye kazi nyingi. Kupata fundi wa bei nafuu
kisiwe ni kigezo chako namba moja. Unataka kupata fundi mwenye ujuzi, uzoefu,
leseni, makini kwenye swala la usalama na mchapa kazi. Ni ukweli kuwa mtu wa
hivi hatakuwa wa bei chee. Na hatahivyo hatakiwi kuwa wa gharama ya juu zaidi
kwamba eti ndio atafanya kazi nzuri. Cha muhimu tu hakikisha haumpi fundi rangi
kazi kwa kuangalia bei yake. Tafuta
gharama za mafundi watatu tofauti ili ulinganishe.
Angalia picha nzima, inasikitisha kusikia
mwenye nyumba anampa kazi saidia fundi. Rahisi ni gharama.
Msomaji wangu kama ulishawahi kusimamia kazi ya kupaka rangi nirushie picha tuone nyumba ilivyopendeza na tuambie ulimpataje fundi. Ukishea ujuzi unajisikia vizuri, kila tunachofahamu leo kuna mtu wa mwanzo alishea..Nawe karibu ushee na sisi..Piga/Whatsapp 0755 200023
No comments:
Post a Comment