TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU ZOEZI LA KUHAMISHA WAKAZI WA MABONDENI
KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Utangulizi
Nchi yetu ina
kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu wanaishi kinyume
cha sheria, huku wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao. Kutokana
na uhaba wa makazi, hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya Jiji la Dar es
Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.
Serikali za awamu
zote, zimekuwa zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni
wanaoishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria lakini mafanikio yamekuwa si ya
kuridhisha.
Serikali ya Awamu
ya Tano, ambayo moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za nchi, imeanza
jitihada za kuwaondoa wakazi hawa.
Tuliamua kuanza
na Bonde la Mto Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu wengi na athari
kubwa.Sababu zetu kuu za kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde na mito katika
jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka ni:-
Kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo
la Bonde la Mto Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu
tangu mwaka 1949 na baadaye 1979.
Kupanua uwezo wa mito ya Dar es
Salaam ili kupitisha maji
ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa
wakati wa mvua nyingi;Kuzuia milipuko ya magonjwa, hasa ya kipindupindu, hasa
wakati wa mvua;
Kuzuia eneo hilo kuendelea
kutumika kama maficho ya wahalifu
na uhalifu;
Kutoa nafasi kwa Serikali
kuandaa na kuendeleza eneo
hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya nyumba
kubomolewa, taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi
ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali
wowote.
Nyumba ambazo
zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa alama X
kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya hapo, mkazi
hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe.
Kutokana na
utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu
wamekwishaamua kubomoa wenyewe.
Baada ya hapo,
alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika zoezi hili, imebainika kwamba
sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya mabondeni ni wapangaji huku wamiliki
wakikaa sehemu nyingine salama.
Serikali
pia imeweka Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Tathmini ya Zoezi
Jana, terehe 7
Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais; pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii), walifanya mkutano
wa kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es
Salaam.
Mkutano huo
ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali, inayoongozwa na
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ambayo, pamoja na mambo
mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya kubaini makazi yaliyojengwa kinyume
cha Sheria katika Bonde la Mto Msimbazi imekamilika.
Ripoti ilieleza
kwamba, hadi sasa, wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba hizo
kubomolewa. Ilielezwa pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa kuhama, uhakiki
kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa.
Kutokana na
uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119
walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi.
Hawa watu hawakuhamishwa.
Mawaziri walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika
zoezi hilo.
Baada ya tafakuri na mjadala,
Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: –
1.Zoezi la
kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo hatarishi)
litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi;
2.Katika awamu
hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3.Kwa wakati huu,
watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo NDANI kabisa ya bonde,
kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye KINGO za mto;
4.Wale
watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha
na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu
nyingine za kujenga. Na watumishi wa umma waliowamilikisha maeneo hayo
watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria;
5.Serikali, ndani
ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo
ubomoaji umefanyika.
6.Serikali
itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi
wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili taratibu
zinazofuatia zifanyike;
7.Serikali
itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume
na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi,
ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria.
Limeanzishwa
dawati la malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
ajili ya kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hili.
8.Nyumba na
majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa Sheria
zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya
wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo watapewa miongozo ya hatua
za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;
9.Serikali haina
dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo karibu na fukwe
katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya watapewa masharti na miongozo
ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
10.Serikali
inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za
utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.
11.Serikali haina
dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao
bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi waendelee
kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini.
Itakumbukwa
kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza
maisha. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu
zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi
karibuni.
12.
Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya taarifa
za wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude
Rwakatare
Mkutano ulipokea
taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji
Rwakatare. Ilielezwa kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake
pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi
katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na Sheria tatu muhimu.
Pia ilielezwa
kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha zilifanyika na
mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na sababu
mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa
mahakamani.
Wakati kesi
inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila
kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei 2015, aliingia
makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya kuondoa
kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza, kutombughudhi kabisa
Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano hayo
yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015. Mwanasheria huyo
alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na
mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza kufukuzwa kazi,
kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo
alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake
zimekwishafikishwa TAKUKURU.
Vilevile, Ofisi
ya Makamu wa Rais, iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba
“makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu
yalipatikana na njia ya udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29
Disemba 2015.
Kuhusu Karakana ya Mradi wa
Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia
ulijulishwa kuhusu hoja inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika
maeneo ya kuishi mabondeni lakini mradi wa DART umeachwa.
Mkutano
ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya kutolewa
ruhusa kwa miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya
mabondeni, na kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa
miongozo ya namna ya shughuli hizo zinavyoweza kufanyika bila kuathiri
mazingira.
Mradi wa
DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za
hifadhi ya mazingira zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016
No comments:
Post a Comment