Ukitaka
kufanikiwa katika jambo lolote ni muhimu kuwa na mipango iliyoandaliwa.
Vilevile katika mapambo ya nyumba mipango ni jambo muhimu.
Kama
toka awali
uliweka mipango ya namna utakavyopamba nyumba yako hii ninayoongelea
hapa itakusaidia. Laa haukuweka mpango bado hujachelewa unaweza kuanza leo.
Mpango ninaozungumzia hapa ni wa rangi ya kuta na sakafu za nyumba toka awali.
Ni
kwamba kama ukiwa na kuta na sakafu zenye rangi ambazo haziegemei upande
wowote, unaweza kubadili muonekano wa chumba chochote kirahisi sana kwa
kubadili tu vitupio vya mapambo. Rangi zisizoegemea upande wowote sio lazima tu
ziwe jamii ya nyeupe au krimu bali ni rangi zote nyepesi na zilizotulia ambazo
ni pamoja na kijivu na bluu bahari.
Kama
unataka chumba kiwe sehemu ya kupumzikia unatakiwa utumie rangi zilizopoa.
Rangi zilizopoa ambazo ni bluu, kijani na zambarau maana yake ni kwamba zikiwa
mahali zinaleta hisia ya utulivu. Kama una kuta na sakafu zenye hizo rangi
tulizosema kuwa haziegemei upande wowote, ukiwa na vitupio vya rangi zilizopoa
unabadilisha muonekano kirahisi mno na kwa gharama nafuu sana.
Rangi
za kuwaka ambazo ni nyekundu, njano na rangi ya chungwa zinaaminiwa kuwa
zinaonekana sana na zina nguvu. Unaweza kutumia rangi hizi zenye nguvu kwenye
vyumba vya watoto, na kwenye vitupio vya sebuleni kama vile mito, vesi za maua
na taa za mezani. Kiti kimoja au viwili vyenye rangi za kuwaka vinabadili
kabisa muonekano wa sebule. Pia mito mikubwa ya sakafuni ya rangi hizi inaweza kutumika
badala ya viti na hivyo kupunguza wingi wa viti sebuleni.
Vile
vile rangi hizi zenye nguvu unaweza kuzitumia kwenye vyombo vya jikoni kama
vile kwenye mabakuli ya kufanya chakula kibaki cha moto, vikombe, glasi na
masufuria ya rangi. Kwa upande wa bafuni rangi za kuwaka unaweza kuzitumia
kwenue mataulo na vizulia.
Kwahivyo
kuendana na tamanio lako unaweza kuwa na vitupio vya rangi zilizopoa au za
kuwaka kwa kadri unavyotaka chumba kiwe, au vileviile unaweza kuchanganya vya rangi za jamii zote mbili ili kuweka fenicha
zako maridadi na hai.Unachopaswa tu ni kuangalia hitaji la chumba husika. Ukiwa
na kuta na sakafu za rangi zisizoengemea upande wowote ni rahisi mno kutumia
vitupio kubadilisha muonekano wa chumba kabisa.
Pamoja
na hayo niliyosema bado kuna baadhi ya vitu unatakiwa kukum buka. Cha kwanza ni
kwamba kwenye chumba kidogo, “vingi ni vidogo”. Maana ya msemo vingi ni vidogo
ni nini? Ni kwamba utakavyoweka vitupio vingi kwenye chumba kidogo matokeo yake
ni chumba kuonekana kidogo zaidi.Kiweke kitulie usikijaze vitu ili kuepuka
kuzidi kuonekana kidogo. Halafu, kama una nyumba ndogo weka vitupio vya rangi
za kuendana nyumba nzima.
Utakachopochanganyachanganya sana nyumba itaonekana kuwa na mhemko na itazidi
kuonekana ndogo.Mwisho, katika kila chumba kwenye nyumba yako muonekano wako
unatakiwa ukutambulishe. Unaweza kuwa na chumba au nyumba nzuri sana hapa
Tanzania lakini kama haitaendana na muonekano au staili yako hautaifurahia.
Kama huna uhakika juu
ya namna vitupio vyako vya rangi vitakavyoonekana ndani ya chumba, anza
kidogokidogo na ongeza vitu taratibu. Ukishazijua rangi hizi kama
nilivyoainisha wala haitakupa shida na hakika nyumba yako itavutia. Kanuni
kuu ni kutengeneza mapambo ya nyumba
ambayo wewe na familia yako mtafurahia kuishi humo.
No comments:
Post a Comment