Mvutano kati ya
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutaka kubomoa nyumba
anayoishi Mchungaji Getrude Rwakatare umezidi kushika kasi mahakamani.
Hali hiyo
ilitokea jana, baada ya wakili wa familia ya Mchungaji Rwakatare, Emmanuel
Agustino kupinga maombi ya NEMC ya
kutaka kuongezewa muda wa kuwasilisha maombi
ya mapitio ya hukumu ya maridhiano inayozuia baraza hilo kuchukua hatua yoyote
dhidi ya nyumba hiyo.
Hukumu hiyo ya
maridhiano ilitokana na kesi iliyofunguliwa 2012 katika Mahakama Kuu Kitengo
cha Ardhi na Robert Brighton, ambaye ni mtoto wa Mchungaji Rwakatare aliyepinga
kubomolewa kwa nyumba hiyo kwa madai kuwa imejengwa mahali pasiporuhusiwa.
Hukumu hiyo
ilitolewa na Jaji Hamisa Kalombola Mei 11, 2015, pamoja na mambo mengine,
alisema pande zote zilikubaliana kuwa, NEMC na wadau wake wasimbughudhi
Brighton katika makazi hayo.
Hata hivyo, Desemba
29, 2015, NEMC ilifungua tena maombi ya kutaka kupatiwa kibali cha kuongezewa
muda wa kuwasilisha maombi ya kufanya mapitio ya hukumu hiyo.
Katika maombi
hayo namba 825 ya mwaka 2015, NEMC inadai kutoitambua hukumu hiyo na kwamba,
uamuzi huo ulifikiwa na mwanasheria wake ambaye hakupatiwa idhini na NEMC.
Hata hivyo,
wakati maombi hayo yalipotajwa mahakamani hapo Jumatatu wiki hii, Wakili
Agustino kwa niaba ya mjibu maombi (Brighton), aliwasilisha hati ya kiapo
kinzani dhidi ya hati ya kiapo cha NEMC kilichoapwa na Mkurugenzi wake
Mtendaji, Bonaventure Baya akipinga maombi hayo ya NEMC.
Jaji John Mugeta
anayesikiliza shauri hilo, aliamuru watoa maombi wawasilishe mahakamani hapo
majibu ya kiapo kinzani cha mjibu maombi kabla ya Januari 20 na akapanga
kusikiliza maombi hayo Januari 21, 2016.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment