1.
Weka
malengo
Malengo
ni muhimu kwani yanatufanya tushikilie kwenye fikra zetu kile tunachotaka
kukamilisha. Malengo yako ya kuondoa mrundikano ni binafsi, lakini yanaweza kuwa
katika mfumo wa sentensi kama hivi. Nitaondoa mrundikano na kuweka mpangilio
kwenye chumba changu cha kulala ili iwe rahisi kupata kitu na kiwe nadhifu kukitazama. Au nitaondoa
mrundikano kwenye kabati langu la nguo ili iwe rahisi kujua ni zipi za kugawa.
Au nitakunja nguo zangu
vizuri ili zisiporomoke zote pale ninapochukua moja.
Umuhimu wa malengo ni ile sehemu ya kusema unaenda kufanya nini na kwa nini.
Kumbuka kuchukua picha kabla hujaanza malengo yako ya kuondoa mrundikano mahali
au chumba fulani.
2.
Weka vifaa vyako pamoja
Vifaa
vya kuondoa mrundikano ni vya kawaida. Unahitaji vikusanyio vinne ambapo
mchanganuo wake ni kikusanyio cha uchafu, cha vitu vya kugawa au kuuza, cha
vitu vya kuhifadhi na cha vitu vya kuweka mbali. Unaweza kuweka majina kwenye
vikusanyio hivi na vinaweza kuwa mifuko, maboksi, matenga au chochote kile
kitakachokuwezesha kutenganisha mafungu haya manne ya vitu. Hivi ndio vifaa
pekee ambavyo unahitaji.
3.
Chagua chumba au eneo
Sasa
ni wakati wa kuchagua chumba au eneo la kuanza kufanyia zoezi lako la kuondoa
mrundikano. Unayeijua nyumba yako zaidi ni wewe. Kama hujawahi tena kufanya
zoezi hili, chumba kizima kinaweza kukuwia ngumu. Chagua eneo moja, kwa mfano
kama umeamua wiki hii unaondoa mrundikano jikoni, basi jumatatu anza na droo za vijiko, uma na visu. Weka
jumanne kiporo kwa ajili ya masufuria na vikaangio. Endelea jumatano na
vikontena. Endelea kidogokidogo na maeneo mengine na hadi umalize wiki jiko
lote linakuwa limekamilika.
4.
Tafuta Muda
Inaweza
kuwa ngumu kupata muda. Kila mtu ana pilika. Kupanga muda wa kuondoa mrundikano
ndani ya nyumba kuna wakati inahusisha hata kujua muda wa wanafamilia wengine. Kwa mfano, huwezi
kufanya zoezi la kuondoa mrundikano ukiwa na mtoto mdogo kabisa kwani atakuwa
na kazi ya kusambaza upya vitu ulivyotenganisha. Wakati mzuri ni akiwa amelala
au vinginevyo kuwe na dada anamwangalia na kaka naye eneo la mbali na
unapofanyia zoezi lako. Kama unafanya kazi siku tano kwa wiki basi siku za
mwisho wa wiki zinaweza kukufaa zaidi kwa zoezi hili. Unaweza kupanga siku
nzima maalum kila baada ya miezi michache kwa ajili ya kuondoa mrundikano. Au
unaweza kuchukua dakika chache ndani ya siku kuondoa mrundikano, kwenye raki ya
viatu tuseme vyako na vya watoto wako wadogo haikuchukui zaidi ya dakika 20
hasa kama haupotezi muda kwenye kufanya uamuzi.
5.
Anza Kuchambua
Kuondoa
mrundikano kunaanza sasa kwa kuchambua vitu eneo ulilochagua na kuviweka katika
yale makundi manne. Fungu la vya kutupa/takataka unaweka vitu ambavyo wewe wala
yeyote hatavitumia tena. Inapendeza pale vifaa vingi vinapotumbukia kwenye
fungu hili. Fungu la vya kugawa au kuuza ni lile la vitu ambavyo hutavitumia
tena nyumbani kwako lakini bado vina thamani. Kuwa makini usiweke vitu vingi
kwenye fungu hili ambapo huenda ungevitazama kwa mara ya pili ni kwamba
unavihitaji. Fungu la tatu ni la vitu wa kuhifadhi mbali. Hivi ni vile ambavyo
hutumii mara kwa mara lakini kuna wakati unavitumia. Mfano mzuri ni kwenye
nguo. Kuna majira mavazi ya baridi kama sweta yanahitajika sana na kuna majira
ya joto ambapo huhitaji sweta. Kwahivyo unahifadhi mbali pindi unapohitaji
unachukua na kutumia tena. Kwa kawaida fungu hili huwa ni dogo. Fungu la nne na
la mwisho ni la vile vitu unavyotumia kila siku ambapo ndio vya kuhifadhi
karibu.
6.
Weka kila kitu panapostahili
Baada
ya kufanikiwa kuchambua kila kitu kwenye fungu lake anza kuondoa na kutupa vile
vya fungu hilo.Vitupe haraka sana ili usije ukabadili mawazo. Ule uamuzi wa
mwanzo ndio uamuzi sahihi. Beba vitu vya kugawa au kuuza na vipeleke
kunakostahili. Vile vya kuhifadhi mbali weka kwenye maboksi au mabegi na
masanduku kwa ajili ya kuhifadhi. Na vya kutumika mara kwa mara vihifadhi vinapostahili
kuwepo. Usipoteze muda kwani vitu vinaweza kujichanganya na ukashangaa unaanza
kuchambua tena.
7.
Furahia mafanikio yako
Ni
wakati wa kupiga picha na kutuma kwa wale unaowapenda ili wafurahi na wewe. Kaa
na utazame hicho chumba ulichoondoa mrundikano. Umefanya kazi nzuri unahitaji
muda wa kujipongeza.
8.
Anza tena
Ukiwa
umemaliza eneo moja unajipanga upya kwa ajili ya wakati mwingine na kuchagua
tena chumba au eneo lingine na kufanya zoezi lilelile la mwazo. Sasa unakuwa
umeshajua mbinu kwa hivyo inakuwa rahisi.
No comments:
Post a Comment