Ukimuona huwezi kuamini anachosema lakini ukweli ni
kwamba ana miaka 19 katika muziki wa dansi, anamudu kusimama jukwaani kucheza
na kuimba kwa zaidi ya saa nane bila kuchoka huku akifanya hivyo siku tano kwa
wiki kuanzia Jumatano hadi Jumapili.
Hapa namzungumzia mwimbaji aliyetimiza miaka 16, akiwa
katika bendi ya Twanga Pepeta bila kuhama, naye siyo mwingine ni Luiza Nyoni
Mbutu, mke halali wa mwanamuziki Faijala Mbutu.
Mwananchi ilifanya mahojiano na mwanamama huyo ambapo mbali
na mambo ya muziki alizungumzia zaidi maisha ya kawaida anapokua mama Brian na
mke wa Mbutu.
Luiza anasema kazi yake haimzuii kufanya majukumu yake
kama mke na mama; “ukitaka kulibaini hilo unikute nyumbani, nahudumia wageni,
familia na nyumba kwa ujumla huwezi kuamini kama ndiyo yule anayewasha moto
jukwaani.
Kwa mujibu wa Luiza, anachukia sana baadhi ya wasanii
wanaotumia muda mwingi wakila bata na kusahau majukumu yao katika jamii.
Anasema kula bata ni uamuzi ya mtu lakini kwake yeye kama
mama mwenye mtoto mmoja anahitaji kuwa na muda wa kupumzika na familia yake
badala ya kurandaranda kila kona kwenye kumbi za Starehe.
Anaongeza kuwa kila inapofika siku ya Jumatatu na Jumanne
kukaa na familia yake hatoki nyumbani labda iwe kuna kikao muhimu kazini.
“Ninatumia siku hiyo kumwandalia vitu muhimu mume na mtoto wangu na hiyo ndiyo
siku pekee ambayo tutapata nafasi ya kula pamoja chakula cha jioni kwani
ninakuwa nyumbani,”aliongeza kuwa kwake yeye bata ni pale anapokuwa kazini
kuwahudumia mashabiki wake.
Kuhusu changamoto anazokutana nazo kutoka kwa ndugu wa
mume wake kutokana na kazi yake Luiza anasema hilo linampa wakati mgumu
kutokana na utamaduni wa Watanzania kutoamini wanawake wanaofanya muziki.
“Siyo ya familia ya Mbutu pekee hata yangu pia
ni changamoto, ukiwa mwanamuziki kila mtu anakutafsiri anavyotaka. Na hiyo
ilikuwa changamoto kubwa kwangu ingawa haikunikatisha tamaa nilipambana na
nilihakikisha siachi ibada.
“Hata nitoke kazini usiku wa manane lazima Jumapili saa
tatu asubuhi niwe kanisani, nifanye ibada ndiyo mambo mengine yafuatie,
nimemuomba Mungu mara nyingi awafanyie wepesi wanafamilia kunielewa kuwa mimi
nipo kazini na sifanyi vitu tofauti kama wengi wanavyodhani.”
Hata hivyo, Luiza anasema kuwa anashukuru mume wake Mbutu
kwa kumuelewa na kuikubali kazi yake huku akiwa balozi wa kutangaza sifa za
uaminifu na umuhimu wa yeye kuwa na mwanamke huyo jambo lilomsaidia sana familia zote
mbili kumuelewa.
Anasema unenguaji na muziki ni moja ya njia za kutafuta
ajira kama kwa sekta nyingine hivyo Watanzania wanapaswa kuheshimu fani hiyo
kama ilivyo kwa nyingine.
“Ninachokichukia ni dharau, kejeli, kutokuthamini.
Sipendi watoa hukumu wanavyowahukumu watu kwa makosa wasiyokuwa nayo huku wao
wakishindwa kufanya kazi yao ya kuchunguza na kuubaini ukweli.”alisisitiza.
Luiza anajigamba kuwa yeye ni balozi wa nidhamu na kamwe
hata tumia kazi yake kujidharirisha kama wafanyavyo kwa baadhi ya wasanii
wengine nchini.
“Sijawahi kuacha tumbo wala kitovu wazi kwa miaka yote
niliyokuwa mwimbaji na mnenguaji, nimefanya hivyo nikiwa na mume na hata
nilipokuwa sijaolewa, hivyo unaweza kumuona mnenguaji, mwimbaji tofauti na hili
linawezekana na bado watu wakakubali kazi yako.”
Kuhusu wasanii wanao saliti wapenzi wao, Luiza alisema
anajiheshimu na kumuheshimu mume wake lakini pia anampenda mtoto wake hivyo
hana haja ya kujihusisha na mambo yanayomvunjia heshima.
Luiza ni nani?
“Watu wengi wakisikia Nyoni wanadhani kabila langu ni
Mngoni siotoki Songea, Mimi Mmwera wa Lindi;
Nje ya muziki nina shughuli zangu ambazo si vema kuziweka
wazi hadi muda wa kufanya hivyo utakapofika, lakini ni halali na zinaniingizia
kiasi fulani cha fedha.”alisisitiza
Hata hivyo, Luiza anasema kuwa endapo asingekuwa
mwanamuziki ungekuwa mwelimishaji katika jamii, kwa sababu alipokutana na
changamoto za kuwa mwanamuziki ndani ya ndoa , alitumia kipawa hicho na jamii
na ikamuelewa.
No comments:
Post a Comment