Watu hao wameuawa wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe na kusababisha vijiji vyao kukabiliwa na tatizo la ukame.
Katika tukio la kwanza, watu watano waliuawa katika kijiji cha Park
Nyigoti wilayani Serengeti mkoa wa Mara usiku wa kuamkia jana.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ernest Kimola, akizungumza na
NIPASHE jana kwa simu, alisema watu hao ambao hata hivyo hakuwataja
majina waliuawa na wanakijiji wenzao wakiwatuhumu kuzuia mvua isinyeshe,
hivyo kusababisha ukame kijijini hapo.
Kimola alisema juzi wakazi wa kijiji hicho waliitisha mkutano na
kuanza kutafakari sababu za kijiji chao kukumbwa na ukame uliosababisha
mito na mashamba ya mimea yaliyolimwa msimu huu kuanza kukauka na
kuelezana kuwa hali hiyo imetokana na ushirikina unaofanywa na baadhi ya
wenzao.
Alisema kufuatia hali hiyo walianza kuwataja kwa majina watuhumiwa
hao na hivyo siku iliyofuata asubuhi walianza kuvamiwa nyumba zao na
kuwashambulia kwa kipigo na kuwaua.
“Wananchi waliwachomoa katika nyumba zao watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia kwa silaha za jadi hadi kuwaua,” alisema.
Kimola alisema Jeshi la Polisi limeendesha msako mkali na
kuwakamata watu sita kwa tuhuma za mauaji hayo huku likiwasaka wengine.
Katika tukio lililotokea mkoani Dodoma, watu watatu waliuawa kwa kuchomwa moto nao wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema tukio
hilo lilitokea Machi 1 mwaka huu katika kijiji cha Msinyeti wilayani
Kongwa.
Alimtaja aliyeuawa kuwa, Saidia Chakutwanga (80) anayedaiwa kuwa
ni mganga wa jadi maarufu kama sangoma kwa kupigwa kwa kitu kizito
kichwani na kutobolewa macho.
Alisema mauaji hayo yalitokea kwenye Kitongoji cha Golani baada ya
wakazi wa eneo hilo kumtuhumu Chakutwanga kuzuia mvua isinyeshe.
Misime alisema katika tukio la pili mume na mke, wameuawa katika
kijiji cha Ihanda wilayani Kongwa wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe.
Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Peter Kaluli (85) na mke wake, Kaila Kaluli (80).
Alisema uchunguzi uliofanywa na polisi umebaini watu hao waliuawa
kutokana na imani za kishirikina wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe
kijijini hapo.
Alisema siku ya tukio Kaluli na mkewe wakiwa wamelala kwenye nyumba
yao ya tembe walivamiwa na kundi la watu ambao walibomoa ukuta wa kisha
kuichoma moto nyumba hiyo na kusababisha vifo vyao. Aliongeza kuwa
katika tukio hilo, nguruwe mmoja aliuawa huku ng’ombe mmoja akikatwa
katwa miguu.
Misime alisema watu wanne, akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji na Wazee wa
Kimila wawili wa Kijiji cha Ihanda (majina yanahifadhiwa), wamekamatwa
wakihusishwa na tukio hilo.
Alisema viongozi hao wanashikiliwa na polisi kwa sababu kabla ya
mauaji hayo kulifanyika kikao ambacho kiliibua masuala hayo ya tatizo la
mvua. Chanzo Nipashe
No comments:
Post a Comment