WATU 42 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 91 wamejeruhiwa vibaya
baada ya mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha katika
Kijiji cha Mwakata, Kata ya Isaka, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Pamoja na vifo hivyo, nyumba za makazi na majengo ya taasisi mbalimbali,
yamebomolewa na mafuriko yaliyosababishwa mawe kusambaa kijiji kizima.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, aliiambia MTANZANIA kwa simu
jana kwamba zaidi ya kaya 100 zimeathiriwa na mvua hiyo, nyumba 160
zimebomolewa na zaidi ya watu 600 hawana makazi.
“Ndugu
mwandishi naomba mtuombee Mungu kwa sababu hali zetu ni mbaya sana tena
sana, kwani tangu saa 11 alfajiri hadi jioni hii tunavyozungumza
sijapumzika.
“Kwa takwimu tulizonazo ni kwamba watu 42
wamepoteza maisha, mejeruhi ni kama 91, kaya 100 zimeathiriwa, watu
zaidi ya 600 hawana makazi na nyumba zaidi ya 160 zimebomolewa.
“Kwa wale wenzetu waliosalimika tunatarajia kuwahifadhi katika Shule ya
Msingi Mwakata na wengine watachukuliwa na ndugu, jamaa na marafiki zao
wenye nafasi za kuwahifadhi.
“Majeruhi tumewapeleka katika
Hospitali ya Wilaya ya Kahama ila wanne tumewapeleka katika Hospitali ya
Mkoa wa Shinyanga kwa matibabu zaidi.
“Hadi sasa nawashukuru
watu mbalimbali wametoa misaada mingi na tumefanikiwa kupata vyakula
mbalimbali kama maji, sukari, chumvi, viberiti, mishumaa, mikate, mafuta
ya kula, juisi na vitu vingine.
“Tunatarajia kuwagawia
waathirika wote vitu hivyo kwa sababu bila kufanya hivyo hali inaweza
kuwa mbaya zaidi kwa vile hawana hata pa kuanzia,” alisema mkuu huyo wa
wilaya.
Kuhusu vifo vilivyotokea, Mpesya alisema kuna baadhi ya
familia zimepoteza watu wote na nyingine zimepoteza baadhi ya
wanafamilia.
“Kuna familia moja ilikuwa na watu saba wote
wamefariki dunia, familia nyingine ilikuwa na watu watano, wote
wamepoteza maisha na familia nyingine zilipoteza watu kadhaa tu,”
alisema Mpesya.
Katika maelezo yake, Mpesya alisema mvua ya
mwisho kubwa kunyesha mkoani Shinyanga ilikuwa Septemba 4 mwaka jana
ambako mabwawa ya maji katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyankulu yalifurika
maji na kutiririsha maji ya kemikali katika maeneo ya makazi ya
wananchi.
No comments:
Post a Comment