MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali
kuvuliwa nyadhifa kwa Askofu wa Kanisa la Elim Pentekoste, Dayosisi ya Pwani,
Manaseh Martin na wachungaji wawili, Tito Tunda na Jarome Andrea, kwa sababu ya
kukiuka katiba ya kanisa hilo na kwenda kinyume na mahubiri.
Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mwandamizi wa
mahakama hiyo, Binge Mashabara baada ya kukubali hoja za Baraza la Wadhamini la
kanisa hilo ambalo lilikuwa limefungua shauri hilo dhidi ya askofu na
wachungaji hao.
Akitoa uamuzi huo alisema walalamikiwa hao
wanaondolewa kwenye nafasi zao za uaskofu na uchungaji, pia wanatakiwa
kurudisha mali zote ikiwemo vitabuvya benki, magari waliyokuwa wanashikiri
aidha walalamikiwa wanatakiwa kulipa Sh milioni 10 kama gharama ya usumbufu na
madhara ya jumla.
Hakimu Mashabara alisema nI aibu kwa viongozi wa
dini kugombea madaraka kama wanasiasa au wananchi wa kawaida ambao
wanawategemea kama viongozi wa kiroho pia wameaminiwa na wananchi kuwaongoza
dhidi ya uovu na vurugu katika jamii hivyo walitakiwa wawe mfano bora na
kuibadilisha jamii ili iwe na mwelekeo mwema.
Alisema mahakama imekubali kuwa uamuzi
uliofanywa na walalamikaji kuwaondoa madarakani walalamikiwa ulikuwa sahihi kwa
mujibu wa katiba dhidi ya vitendo vyao ambavyo vinapingana na mafundisho ya
dini yao.
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyofunguliwa
mahakamani hapo na mawakili kutoka Kings Law Chambers Novemba 25, 2011, na
Baraza la Wadhamini la kanisa lilimwondoa madarakani Askofu Manaseh kwa sababu
ya kwenda kinyume namaadili, katiba na mafundisho ya dini hiyo.
No comments:
Post a Comment